Dokta Harrison Mwakyembe. |
WAZIRI wa Uchukuzi, Dkt. Harrison Mwakyembe amesema anajitoa mhanga
kuhakikisha Wizara yake inawatia mbaroni watu wanaojihusisha na
usafirishaji wa dawa za kulevya kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa
Mwalimu Julius Nyerere (JNIA).
“Nitajitoa mhanga juu ya biashara hiyo na siogopi vitisho vya watu,
maana mimi nilishakufa siku nyingi, hatuwezi kuidhalilisha nchi yetu
kiasi hicho,” alisema.
Alisema hayo juzi, wakati akieleza mkakati wa Wizara yake kudhibiti
wanaosafirisha dawa hizo kupitia uwanja huo uliopewa heshima ya kuitwa
jina la Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere wakati wa maadhimisho ya
Siku ya Vijana Duniani yaliyofanyika jijini hapa juzi.
“Dawa za kulevya sasa zinasafirishwa kupitia kiwanja cha ndege, ambacho
kimepewa jina la mtu muhimu katika nchi yetu, Mwalimu Nyerere, ni aibu
kwa nchi yetu na Taifa letu, kuona uwanja huo unatumika kwa biashara
hiyo, nipeni muda, mimi ndiye Waziri wa Uchukuzi, hatutakubali hali
hii,” alisema na kuongeza: “Pale uwanjani kuna ofisi nne, Polisi,
Uhamiaji, Usalama wa Taifa na watu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege, wote
nimewaagiza wanipe taarifa, walikuwa wanafanya nini hadi dawa hizo
zinapita uwanjani hapo?”
Alisema anawapa notisi watu wote wanaosafirisha dawa za kulevya kupitia
uwanjani hapo, watambue kuwa alishajitoa mhanga kupambana na dawa za
kulevya, maana ni biashara inayodhalilisha Taifa.
Mwakyembe alipata kuugua kiasi cha kukatisha tamaa ambapo ilikuja
kubainika kuwa aliwekewa sumu iliyosababisha mwili wake kuharibika na
nywele kunyonyoka huku kucha zikibadilika rangi, lakini alipona
alipopelekwa kwa matibabu zaidi India.
Alivitaka viwanja vyote vya ndege nchini, kuhakikisha vinaweka mikakati
ya kisayansi kubaini watu wanaosafirisha dawa hizo kupitia kwenye
mipaka yao.
“Na kwa hili, niviagize viwanja vyote vya ndege nchini vihakikishe kuwa
vinadhibiti wasafirishaji wa dawa za kulevya kwa kushirikiana na vyombo
vingine vya Dola vilivyo katika viwanja hivyo,” aliongeza.
Alitaka viongozi wa dini washiriki kujenga amani nchini huku akionya
vijana dhidi ya kushabikia vitendo vinavyoweza kuipeleka nchi katika
migogoro ya kivita na wajifunze mifano kwa baadhi ya nchi zilizoingia
kwenye vita.
Alisema uzoefu unaonesha, kuwa nchi zilizoingia katika migogoro ya
kivita imekuwa vigumu kurudia hali ya kawaida na zimeendeleza vita vya
wenyewe kwa wenyewe.
“Afrika Kusini, Congo DRC ni nchi ambazo zimejaaliwa kuwa na rasilimali
nyingi za madini, lakini kutokana na kukosa amani kwa muda mrefu,
imekuwa vigumu rasilimali kufikia wananchi wote,” alisema.
Alitaka vijana kubadili tabia na mtazamo kwa kuwa ndiyo njia pekee ya
kujikomboa kiuchumi na kifikra na kuacha kutumiwa na wanasiasa.
Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba, Deus Kibamba ambaye alikuwa Mwezeshaji
Mkuu katika tamasha hilo, alitaka viongozi wa madhehebu ya dini nchini
waendelee kujenga amani iliyopo kwa ajili ya vizazi vya sasa na vijavyo.
“Mimi huwa naamini kuwa amani hujengwa, haiombewi, hivyo naomba
viongozi wa dini mshiriki kuijenga amani nchini, kwa manufaa yetu sote,”
alisema na kutaka vijana waache kulalamika bila kufanya kazi.
Mkurugenzi wa Shirika lisilo la Serikali la Jitambue Foundation, Isaac
Mwanahapa, alisema kuwa Jitambue iliandaa tamasha hilo la vijana kwa
lengo la kuwaleta pamoja ili kujadili mambo ya msingi ya Taifa.
Alisema kwa maadhimisho hayo, shirika lake liliadhimisha siku hiyo kwa
kuchagua kaulimbiu ya “Tetea Amani, Okoa Kizazi Kijacho”, kutokana na
nchi kugubikwa na matukio ya uvunjifu wa amani, yakiwamo ya watu kupigwa
mabomu na kumwagiwa tindikali, kwenye maeneo ya ibada na hata kwenye
mikutano ya kisiasa. (Kwa hisani ya Jukwaa huru)
No comments:
Post a Comment