Tuesday, August 20, 2013

WALIOFARIKI DUNIA KATIKA AJALI YA GARI WATAMBULIWA MAJINA YAO

Na Kassian Nyandindi,
Nyasa.



WATU wawili wamefariki dunia na wengine 40 wamejeruhiwa vibaya, kufuatia ajali ya gari iliyotokea majira ya usiku katika milima ya Burma wilayani Nyasa mkoa wa Ruvuma.

Tukio hilo limetokea Agosti 19 mwaka huu majira ya saa 3 usiku na kwamba, waliofariki dunia wametambuliwa kwa majina ya Lumanyama Sanga na Issa Adamu wakazi wa Songea mjini, huku baadhi ya majeruhi wakiwa wamelazwa katika hospitali ya wilaya ya Mbinga.

Aidha majeruhi wengine ambao hali zao ni mbaya, wamesafirishwa kwenda hospitali ya mkoa Songea na Peramiho zilizopo mkoani humo.
Imeelezwa kuwa waliopoteza maisha katika ajali hiyo ni wafanyabiashara ambao wanaishi Songea mjini, na kwamba uongozi wa wilaya ya Mbinga umeweza kufanya taratibu za kusafirisha maiti hizo pamoja na majeruhi, ambao walipewa rufaa kwa ajili ya kwenda kupatiwa matibabu zaidi katika hospitali hizo.

Gari lililopata ajali ni aina ya fuso lenye namba za usajili T. 807 AVH ambalo lilikuwa likiendeshwa na Lehani Mohamed Makunganya mkazi wa Songea mjini, ambapo dereva huyo naye ana hali mbaya.

Kwa mujibu wa vyanzo vya uhakika vya habari, vimedai kuwa ajali hiyo ilitokana na gari hilo, kuwa katika mwendo kasi na kupakia mizigo mingi ya nguo ambazo zilikuwa zikipelekwa Mbamba bay wilayani Nyasa, kwa ajili ya kwenda kufanya biashara ya kupiga mnada.

Hata hivyo Kamanda wa polisi wa mkoa wa Ruvuma Deusdedith Nsimeki amethibitisha kutokea kwa tukio hilo, ambapo amesema polisi wanaendelea na uchunguzi juu ya tukio hilo.

No comments: