Baadhi ya madiwani wa Tunduru wakifuatilia kwa makini taratibu za uchaguzi huo, ambao ulifanyika kwenye ukumbi wa Klasta ya walimu Tunduru mjini. (Picha zote na Steven Augustino) |
Na Steven Augustino,
Tunduru.
MADIWANI wa Halmashauri ya wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma
wamemchagua kwa mara ya pili, Diwani wa Kata ya Mchoteka wilayani humo, Mkwanda
Sudi kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi(CCM) kuwa makamu wa Mwenyekiti wa
halmashauri hiyo.
Diwani huyo aliweza kupata kura za ushindi 42 ambazo ni za ndiyo
baada ya diwani mwenzake Rashid Omary, kujitoa katika kinyang’anyiro hicho.
Matokeo hayo yalitokana na mgombea wa nafasi hiyo, ambaye
ni wa kutoka chama cha upinzani, kupitia tiketi ya Chama cha Wananchi CUF alijiondoa
kwa hiari yake.
Akitangaza matokeo hayo Katibu wa uchaguzi huo, Mkurugenzi
mtendaji wa halmashauri ya wilaya Tunduru, Albart Nehatta alisema kuwa idadi ya
wapiga kura ilikuwa 48, ambapo kura zilizoharibika zilikuwa 2, kura za hapana 4
na kura za ndiyo zilikuwa 42 ambazo zilimfanya mgombe huyo wa CCM apate ushindi.
Akitangaza matokeo ya kamati ya elimu ambayo wapiga kura
walikuwa 16, kamati hiyo ilimchagua Diwani wa Kata ya Mbati Burhan Nakanje
aliyepata kura 9 na kumshinda Diwani wa Kata ya Nandembo Bi. Idaya Lweso aliyepata
kura 7 .
Nehatta alieleza kuwa upande wa kamati ya uchumi, ujenzi na mazingira
wao walimchagua Diwani wa Kata ya Majengo Athuman Nkinde kwa kura 6 baada Diwani
Fadhili Mshamu aliyepata kura 3, Anita Komba kura 5 na kura 2 ziliharibika.
Upande wa kamati ya maadili katika halmashauri ya Wilaya hiyo
wajumbe hao walimchagua Diwani wa Kata ya Kidodoma Seifu Yusuph ambaye alipita bila kupingwa.
No comments:
Post a Comment