Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida Baraza la Madiwani,
Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, limesitisha zoezi la mgawanyo wa
mali kati ya wilaya hiyo na wilaya mpya ya Nyasa, kutokana na zoezi hilo
kuonekana kuingiliwa na vitendo vinavyoashiria kuwepo kwa upendeleo wa upande
mmoja, na wenye kulenga njia za siri na ujanja ujanja.
Aidha usitishaji huo umefuatia Madiwani hao kubaini kuwa
aliyekuwa Mkurugenzi wa wilaya ya Mbinga Shaibu Nnunduma, ametumia mbinu za
ujanja katika kutengeneza makabidhiano(Handing Over) kwa Mkurugenzi mpya wa
wilaya hiyo Hussein Ngaga, ambayo yanalenga asilimia kubwa ya mali zilizopo
Mbinga zipelekwe Nyasa.
Hali hiyo imejitokeza leo katika kikao cha baraza hilo
kilichoketi kwenye ukumbi wa Jumba la maendeleo uliopo mjini hapa, kikao
ambacho ni cha kawaida chenye kulenga kujadili maendeleo mbalimbali ya wilaya
hiyo.
Mbunge wa Jimbo la Mbinga, Gaudence Kayombo akichangia hoja
katika kikao hicho alisema, endapo uongozi wa wilaya hiyo na mkoa huo kwa
ujumla utaendelea kulifumbia macho suala la mgawanyo halali wa mali za
halmashauri za wilaya ya Mbinga na Nyasa, baraza la madiwani la wilaya ya
Mbinga lipo tayari suala hili kulifikisha mahakamani ili haki iweze kupatikana.
Alisema jambo hili hata yeye binafsi linamsikitisha kwa jinsi
lilivyofanyika, hivyo hakubaliani nalo na sasa tayari amekwisha ongea hata na uongozi
wa makao makuu ya Tawala za mikoa na serikali za mitaa(TAMISEMI) ili waweze
kuja na kulifanyia kazi.
“Kuhusu mgawanyo huu wa mali hata mimi unanisikitisha,
nimeongea na mkoa na TAMISEMI wamesema wanakuja kushughulikia suala hili, na
kwa kweli nasema jambo hili linaonesha kuna ujanja ujanja umefanyika na sisi
kama madiwani wa Mbinga, hatutakubali kuona linaendelea”, alisema Kayombo.
Mbunge huyo alisisitiza akisema, mali hizo ni vyema
zigawanywe kwa uwiano ulio sawa, huku akiongeza kuwa pasipo kufanya hivyo
itakuwa ni ulafi ambao unadhihirisha wazi kwamba, mtu mmoja anataka kujilimbikizia
mali nyingi wakati Mbinga nayo inabidi isonge mbele kimaendeleo.
Kadhalika Diwani wa Kata ya Utiri Hyasint Ndunguru, naye
alinyoshea kidole suala hilo alisema, kuna siri kubwa imejificha juu zoezi hilo
la mgawanyo wa mali huku akieleza kuwa kamati ya mgawanyo wa mali anamashaka
nayo haikutenda haki wakati ilipoketi ikifanya mchakato wa zoezi hilo.
“Mheshimiwa mwenyekiti, mimi binafsi ninamashaka katika
ugawaji wa mali hizi, magari mengi wameyachukua lakini cha kushangaza madeni wametutupia
sisi peke yetu huku Mbinga tuyalipe na wao wasiyalipe, mimi siwezi kuunga mkono
jambo hili, vizuri lifanyiwe kazi upya kwa kufuata taratibu nzuri”, alisema
Ndunguru.
Naye Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga, Allanus
Ngahi aliunga mkono kwa kusema kuanzia sasa wanasitisha kazi ya mgawanyo wa
mali kati ya wilaya hizo mbili, (Mbinga na Nyasa) hadi kamati husika
itakapoketi na kuridhia uhalali wa mgawanyo huo.
Pamoja na mambo mengine, hoja hii ya mgawanyo wa mali katika
baraza hilo la Madiwani la halmashauri ya wilaya ya Mbinga ililetwa na madiwani
hao katika baraza hilo, ikiwa katika mfumo wa hoja binafsi ili iweze kujadiliwa
na kusitishwa mara moja kwa mgawanyo huo hadi hapo baadaye Kamati husika, itakapoketi
na kufanya tena upembuzi yakinifu juu ya mgawanyo wenye uwiano sawa ambao
hautaweza kuleta mtafaruku miongoni mwa madiwani wa wilaya ya Mbinga na Nyasa.
No comments:
Post a Comment