IGP Said Mwema. |
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
PADRE wa Kanisa Katoliki Xavery Kazimoto Komba, amekamatwa na
kuwekwa mahabusu katika kituo kikuu cha polisi wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma,
kwa tuhuma ya kuwatapeli wakulima kahawa yenye thamani ya shilingi milioni 95.
Habari zinaeleza kuwa mchungaji huyo ambaye ni wa Seminari
kuu Peramiho jimbo la Songea, amesota mahabusu kwa siku tatu ambapo anadaiwa kuchukua kahawa ya wakulima hao na
kutokomea nayo kusikojulikana.
Komba anatuhumiwa kukusanya kahawa kilo 25,000 yenye thamani
ya fedha hizo, katika vikundi vitano vya wakulima, msimu wa mavuno wa mwaka
2012 na 2013 kwa lengo la kwenda kuuza na baadaye aweze kurejesha malipo halali
ya wakulima hao.
Vikundi ambavyo alikusanya kahawa na kutokomea nayo bila
kurejesha malipo yao ni Lutondo, Muungano Lituru, Jaribio Lunoro, kipando na
Otmary vilivyopo wilayani Mbinga.
Imeelezwa kuwa Padre huyo amekuwa akifanya biashara ya zao
hilo kupitia kampuni yake ya Songea network, lakini cha kushangaza baada ya kukusanya
kahawa ya vikundi hivyo, hadi leo hii hajarejesha fedha hizo kwa wakulima wa
vikundi hivyo.
Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Ruvuma Deusdedith Nsimeki, amethibitisha
kuwepo kwa tukio hilo na kwamba alieleza kuwa yupo bado mahabusu wakati wowote kuanzia
leo atafikishwa Mahakamani baada ya uchunguzi kukamilika, ambao unafanywa na
kitengo cha Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(TAKUKURU) wilayani Mbinga.
Nsimeki alisema anafanyiwa uchunguzi chini ya kifungu kikuu namba
15 cha sheria ya kuzuia na kupambana rushwa cha mwaka 2007.
Hata hivyo alipotafutwa Kamanda wa TAKUKURU mkoani Ruvuma
Daud Masiko, ili aweze kutolea ufafanuzi juu ya tukio hilo hakuweza kupatikana
na simu yake ilikuwa ikiita muda mrefu bila kupokelewa.
No comments:
Post a Comment