Gaudence Kayombo, Mbunge wa jimbo la Mbinga. |
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
WITO umetolewa kwa wananchi katika wilaya ya Mbinga
mkoani Ruvuma, kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo na kutoa
mawazo yao mapya ambayo yataijenga upya wilaya hiyo na kuendeleza shughuli za
kiuchumi kwa faida ya kizazi cha sasa na kijacho.
Pia wametakiwa kuwa mstari wa mbele na kuacha malalamiko
yasiyokuwa na manufaa kwao kwani hayatasaidia kuongeza uzalishaji
au kuleta maendeleo katika jamii hivyo endapo watafanya hivyo wanaweza
kuirudisha nyuma wilaya hiyo ambayo ni tegemeo kubwa kwa uchumi mkoani Ruvuma.
Kauli hiyo ilitolewa na Mbunge wa jimbo la Mbinga Gaudence
Kayombo wakati alipokuwa akizungumza katika kikao cha dharula cha baraza la
Madiwani kilichoketi kwenye ukumbi wa jumba la maendeleo uliopo mjini hapa.
Kayombo alisema kila mmoja anaowajibu mkubwa kutoa
mawazo au michango mbalimbali kwa viongozi na watumishi wa halmashauri ya
wilaya hiyo, ili wasaidiane katika kuijenga wilaya badala ya jukumu hilo kuliacha
kwa watu wachache huku akisisitiza viongozi kutanua wigo katika
kuwahudumia wananchi na kuacha tabia ya kujifanya Miungu watu.
Vilevile Mbunge huyo amewakumbusha watumishi na
wataalamu wote katika halmashauri hiyo kutimiza wajibu wao katika kushauri na
kujenga ubunifu kwa kubuni hata vyanzo vya mapato ambavyo vitasaidia kupata
fedha za kutosha ambazo zitawahudumia wananchi katika kutekeleza miradi
mbalimbali ya kimaendeleo.
Kadhalika alisisitiza kuyahudumia makundi mbalimbali maalum
yenye kuhitaji mahitaji muhimu katika kuishi, kama vile walemavu, wajane,
vijana na yale mengine ambayo yanahitaji kujinasua katika kuondokana na
lindi la umasikini unaowakabili miongoni mwao.
Alisema
kwa muda mrefu makundi hayo yamesahaulika hivyo muda umefika kwa viongozi
kuyaangalia kwa lengo la kutaka kuyapunguzia mzigo wa matatizo waliyonayo na
sio kuyaacha pekee.
Amewaagiza madiwani kuwa mstari wa mbele katika
mapambano dhidi ya umasikini na kwenda kuongeza umakini katika usimamizi
na ufuatiliaji wa fedha za miradi mbalimbali ya maendeleo vijijini, ili
fedha zinazopelekwa na serikali huko ziweze kufanya kazi iliyokusudiwa.
Kayombo amewasihi wanaporudi katika maeneo yao kwenda
kuwashirikisha wananchi kwa kila jambo la maendeleo na wawe wabunifu.
No comments:
Post a Comment