Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
MAKAMPUNI yanayojishughulisha na ununuaji wa kahawa katika
msimu wa mwaka huu wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, yameaswa kufuata taratibu
zilizowekwa katika mchakato wa utekelezaji wa zoezi hilo wilayani humo.
Mkuu wa wilaya hiyo Senyi Ngaga alitoa agizo hilo katika
kikao cha Wadau wa zao hilo kilichoketi jana Julai 12 mwaka huu, kwenye ukumbi
wa Jumba la maendeleo uliopo mjini hapa.
“Nawaasa tufuate taratibu zilizowekwa, tusiwakope wakulima
kahawa ninachohitaji hapa tuwalipe fedha zao taslimu, atakayekiuka hili tusije
tukaonana wabaya”, alisisitiza Ngaga.
Sambamba na hilo Ngaga alisema hataki kuona biashara ya
Magoma ikiendelea kufanyika wilayani Mbinga, na endapo atalibaini hilo yupo
tayari kumchukulia hatua za kisheria mfanyabiashara ambaye atahusika kufanya
hivyo.
Alisema biashara za mtindo huo hazina tija kwa mkulima wa
kahawa, badala yake zimekuwa zikirudisha nyuma maendeleo ya mkulima husika.
Kadhalika Mkuu huyo wa wilaya alitangaza bei ya kununua
kahawa wilayani Mbinga, ambapo alisisitiza kwamba mtu yeyote asinunue kahawa
mbivu chini ya bei ya shilingi 500 kwa kilo moja.
Vilevile kwa upande wa
kahawa kavu ambayo imekobolewa kwenye mitambo, inunuliwe kwa shilingi 2533 na
kwa ile ambayo imekobolewa nyumbani kwa mkulima(Home Parchment) inunuliwe kwa
shilingi 1900 kulingana na bei elekezi, iliyotolewa na Bodi ya kahawa Tanzania(TCB).
Ngaga aliongeza kuwa uchumi wa wilaya ya Mbinga kwa asilimia
80 unategemea zao la kahawa, hivyo uongozi wa wilaya hiyo unasisitiza wadau wa
kahawa kuzingatia kanuni au sheria zilizowekwa katika kuliendeleza zao hilo,
ili liweze kuwa endelevu kwa faida ya vizazi vya sasa na vijavyo.
Pamoja na mambo mengine Ngaga alifungua rasmi msimu wa
kununua zao hilo wilayani humo, na kwamba hivi sasa makampuni yote yaliyokubaliwa
kufanya biashara ya zao hilo wilayani Mbinga, sasa ni ruksa kupita kwa wakulima
vijijini kununua kahawa.
No comments:
Post a Comment