Waziri Mkuu Mizengo Pinda akisisitiza jambo. |
Na Mwandishi wetu,
Tunduru.
MSAFARA wa Waziri Mkuu Mizengo Pinda, wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania umeingia dosari baada ya gari lililobeba askari polisi lenye namba
za usajili PT 1437 kusababisha ajali, ambayo ilipelekea magari matatu yaliyokuwa
mbele yake kugongana na mwandishi mmoja wa Radio Maria kupata maumivu mwilini.
Habari zinaarifu kuwa tukio hilo lilitokea majira ya asubuhi
katika kijiji cha Kilimasela wilayani Tunduru, wakati msafara huo ukitokea Tunduru
kuelekea wilayani Namtumbo.
Gari hilo la polisi lilisababisha ajali ya kuligonga gari
lililokuwa mbele yake lenye namba DFP 6627 ambalo nalo liligonga gari lenye
namba STK 7919.
Wakati gari lenye namba za usajili STK 7919 likigongwa, nalo
liligonga gari ambalo lilibeba Waandishi wa habari lenye namba DFP 8706 ambalo
lilikuwa mbele yake na kusababisha mmoja kati ya waandishi waliokuwemo kwenye
gari hilo Moses Konala, kupata maumivu ambayo mwili wake umetetereka kidogo.
Katika msafara huo kwa ujumla, hali za watu waliopatwa na
mkasa huo katika eneo hilo wilayani Tunduru wanaendelea vizuri, na msafara umeingia
wilayani Namtumbo na Waziri Mkuu anaendelea na ziara yake ya kikazi wilayani
humo.
Mizengo Pinda akiwa Namtumbo ameweza kuweka jiwe la msingi
ujenzi wa hospitali ya wilaya hiyo ambayo imegharimu fedha za kitanzania
shilingi milioni 600, machinjio ya kisasa yenye thamani ya shilingi milioni 800
na jengo la shirika la ugavi wa umeme (TANESCO) “Power house station” nalo
ambalo limegharimu ujenzi wake shilingi milioni 800.
Pianda akihutubia wananchi wa wilaya hiyo aliziagiza halmashauri
za Wilaya, Manispaa na Majiji nchini, kuhakikisha watendaji wake wakiwemo (Wakurugenzi)
kuhakikisha wanasimamia ipasavyo miradi ya wananchi pamoja na kujengwa kwa viwango
vinavyokubalika.
Kadhalika alionya kwamba mtendaji husika atakayebainika kuhusika
na utoaji wa tenda kwa njia ya rushwa na upendeleo, atachukuliwa hatua za
kisheria ili iwe fundisho kwa wengine wenye tabia kama hiyo.
“Tenda za ujenzi wa miradi mbalimbali ya wananchi, wapeni makandarasi
ambao wana uwezo, na wananchi hamasisheni kuchangia miradi yao ya maendeleo”,
alisisitiza Pinda.
Alibainisha kuwa hivi sasa serikali imejiwekea mkakati kwamba
maeneo mengi ya mikoa na wilaya hapa nchini yataunganishwa na umeme wa gridi ya
taifa, ikiwa ni lengo la kukuza na kuharakisha maendeleo ya wananchi yaweze
kukua kwa kasi.
Hata hivyo Waziri Mkuu Pinda kesho ataendelea na ziara yake
wilayani Nyasa ambako miradi mbalimbali ya maendeleo ya wananchi nayo ataweka
mawe ya msingi na kuikagua kama imejengwa kwa viwango vyenye ubora.
No comments:
Post a Comment