Wednesday, July 24, 2013

CHAMA CHA WALIMU MBINGA MKOANI RUVUMA, CHATUPIWA MFUPA ULIOMSHINDA FISI

Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu.





















Na Mwandishi wetu,

Mbinga.

VURUGU na migogoro ya hapa na pale inayoondelea kudaiwa kufanywa na baadhi ya vigogo wa Chama Cha walimu Tanzania(CWT) Tawi la Mbinga mkoani Ruvuma, mapya yameibuka juu ya sakata hilo, mtandao huu umeelezwa.

Wadau wa elimu wilayani humo wametoboa siri hiyo nzito kwamba, chanzo cha vurugu na migogoro hiyo, kinatokana na Katibu wao wa CWT wilayani Mbinga Samwel Mhaiki kukosa busara na utulivu katika utendaji wake wa kazi.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Mwandishi wetu, walifafanua kuwa Mhaiki ni mtu wa kupenda kuendekeza migogoro kazini na  tabia hiyo hajaanzia hapa Mbinga, bali tokea alipokuwa akifanya kazi ambako alianzia Ukatibu wake mkoani Mtwara.

Kana kwamba haitoshi, wameeleza kuwa huko alikuwa akiendesha migogoro na migongano kwa watumishi wenzake, wakiwemo hata viongozi wa serikali.

Waliendelea kueleza kuwa baada ya kuonekana Mhaiki ni tatizo na mwiba katika jamii, akahamishiwa wilaya ya Tunduru nako anadaiwa kuendeleza malumbano hayo, na hata kufikia hatua ya kukosa maelewano na viongozi wa wilaya hiyo.

“Kufuatia hali hiyo na mambo mengine yasiyoelezeka, chama cha walimu kilichukua jukumu la kumhamishia hapa Mbinga, hivyo yanayoendelea leo hapa wilayani ni mwendelezo wa historia yake na sasa inadaiwa kaungana na Katibu wake wa mkoa kuendeleza malumbano haya”, alisema Mwalimu mmoja ambaye hakutaka jina lake litajwe.

Kadhalika Wadau hao wa elimu wilayani humo wameeonesha masikitiko yao juu ya migogoro hiyo wakisema, tabia hii haifai kuigwa katika jamii kwa kile walichoeleza kuwa maendeleo katika sekta ya elimu hususani kwa shule za msingi wilayani hapa, yanaweza kurudi nyuma endapo vitendo hivyo vitaendelea kufumbiwa macho.


“Mimi binafsi nawasihi walimu wenzangu wa shule za msingi na sekondari hapa Mbinga, tufanye kazi tuache majungu na tuachane na tabia za Katibu huyu wa CWT, vinginevyo tukiendekeza migogoro hii kazini tutavuna mabua”, alisema.

Aidha Wadau hao wa elimu wilayani Mbinga waliendelea kupigilia msumari wa moto wakisema, Mhaiki ni kiongozi ambaye amekuwa kikwazo pale viongozi wa serikali wa wilaya hiyo wanapopanga mipango ya kimaendeleo katika sekta ya elimu, yeye hupita mashuleni kwa walimu na kuhamasisha migogoro ikiwemo migomo baridi isiyokuwa na tija kwa kile walichoeleza kwamba, anawahamasisha walimu wasifanye kazi kwanza ya kufundisha hadi pale wanapolipwa maslahi yao.

Walisema ukipita mashuleni kumejaa mabarua ya Katibu huyo wa CWT ambayo yanahamasisha walimu wagome na yanashawishi migogoro kati ya walimu na mwajiri wao, yanayobeza serikali na viongozi wake huku mengine akiwa ameyaandika na kuyapeleka katika ofisi za serikali ngazi ya mkoa na Taifa(nakala tunazo) ambayo yanalenga kuchafua utendaji wa kazi wa viongozi wa sekta ya elimu wilayani Mbinga.

Mwandishi wetu alipomtafuta Katibu wa CWT wilayani Mbinga, Samwel Mhaiki hivi karibuni, alikiri kutoelewena na baadhi ya viongozi wa wilaya hiyo hususani wa sekta ya elimu huku akisema kwamba migogoro hii, inatokana na vigogo wa wilaya hiyo kutompa ushirikiano kati yake na uongozi wa chama hicho.

Hata hivyo kuhusu suala la kuandika barua zenye mrengo wa kushoto ambazo zinaharibu sifa za utendaji kazi kwa viongozi wilayani humo, nalo alikiri kuziandika huku akizungumza kwa ujasiri kuwa anachokiandika sio cha uwongo ana uhakika nacho.

No comments: