Na Muhidin Amri,
Ruvuma.
BAADHI
ya askari polisi kituo kikuu Mbinga mjini, wamemtuhumu Mkuu wa
polisi wa wilaya hiyo(OCD) Justine Joseph, kuwa ni mtu anayetumia madaraka
yake vibaya kwa kuendesha manyanyaso dhidi ya askari wa vyeo vya chini
na kumuomba Mkuu wa Jeshi hilo hapa nchini Said Mwema, kumchukulia hatua za kinidhamu.
Askari wengine ambao hakutaka majina yao yatajwe katika mtandao huu walisema ni vyema kama kuna uwezekano, ahamishwe na kupewa kituo kingine cha kazi kabla hali
haijawa mbaya.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, askari hao
wamelalamikia kuwa OCD huyo amekuwa hana ushirikiano na baadhi ya askari wenzake na wakati mwingine hutoa lugha za dharau, na hata
zisizopendeza kwao hali inayowavunja moyo wa kufanya kazi katika
wilaya hiyo.
Walisema iwapo
jeshi litashindwa kumchukulia hatua za kinidhamu huenda kukatokea sintofahamu na hawatoweza kuvumilia vitendo vinavyoendelea kufanywa na afisa huyo ikiwemo hilo la kuwatolea lugha za kihuni ambazo walidai kuwa ni sawa na kuwadhalilisha.
Aidha
wameshauri hata maafisa wengine katika wilaya hiyo wanatakiwa kuondoka
kwani wameshakaa Mbinga kwa muda mrefu, hivyo ni vyema wakapelekwa katika
maeneo mengine hapa nchini.
Walisema kitendo cha maofisa hao kukaa muda mrefu katika kituo cha Mbinga wamekwisha jenga mazoea makubwa na raia, hivyo huwafanya washindwe kutimiza majukumu yao ya kazi ipasavyo.
Wamelalamikia wakidai kuwa OCD Justine ni mtu ambaye hapendi kushirikisha wenzake wakiwemo maafisa wa ngazi ya chini jambo linalomfanya kutengwa na kujikuta yuko pekee.
"Huyu
mkuu wetu ni tatizo ni vyema sasa serikali ikaangalia upya namna ya kutatua tatizo hili lililopo sasa hapa Mbinga, vinginevyo viongozi wa ngazi ya juu wakiendelea kulifumbia macho askari tutashindwa kufanya kazi zetu ipasavyo", walisema askari hao.
Kwa
upande wake Mkuu huyo wa polisi wilaya ya Mbinga Justine Joseph alipohojiwa hivi karibuni ofisini kwake na mwandishi wa habari hizi alikanusha tuhuma hizo na kuziita kuwa ni unafiki
unaofanywa na askari wachache waliozoea kula rushwa hasa kwa
waendesha pikipiki jambo ambalo yeye hataki kusikia katika uongozi wake.
“Hizi
tuhuma sio za kweli, zinafanywa na baadhi ya askari wangu hasa wale wala
rushwa, nimekwisha elekeza wakikamata pikipiki waje na faini hapa au mmiliki
wake sio kuleta pikipiki hatuna eneo la kupaki kwani hizi tulizonazo ni
nyingi na hatuna sehemu ya kuzipeleka”, alisema Justine.
Naye
Kamanda wa polisi mkoa wa Ruvuma Deusdedith Nsimeki alikiri kuwepo kwa
malalamiko hayo ya askari wa vyeo vya chini kituo cha Mbinga mjini, dhidi ya OCD wao na kuahidi kuwa
atashughulikia tuhuma hizo ili kupata ukweli wa jambo hilo.
"Askari hatufanyi mambo kwa kukurupuka lazima tufanye uchunguzi ili
tujiridhishe, unajua ukishakuwa kiongozi unatakiwa kuwa makini hasa
katika maamuzi ili usifanye mambo kwa kumuonea mtu, lazima utende haki
kila wakati”, alisema Nsimeki.
No comments:
Post a Comment