Waziri wa elimu na mafunzo ya ufundi, Shukuru Kawambwa. |
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
SERIKALI imeombwa kumchukulia hatua za kinidhamu afisa
taaluma wa elimu ya msingi katika Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani
Ruvuma, Bw. Rashid Pilli kufuatia kutajwa kuwa ni kikwazo kikubwa cha
maendeleo katika sekta ya elimu wilayani humo, licha ya serikali ya
wilaya hiyo kufanya juhudi zake za kuongeza kiwango cha taaluma.
Pilli anadaiwa kuwa chanzo cha vurugu na migogoro ya
muda mrefu isiyokwisha ambayo inaendelea kufukuta katika idara ya elimu
ya msingi kwa kuendesha mapambano dhidi ya afisa elimu ya
msingi Bw. Mathias Mkali, na hata kufikia hatua ya
kumchonganisha kwa serikali pamoja na walimu mashuleni jambo
ambalo linamvunja moyo utendaji wa kazi wa afisa elimu huyo katika jitihada
zake za kuinua kiwango cha elimu wilayani humo.
Habari zinasema licha ya matukio hayo ya mara kwa mara
ambayo kwa sasa yamekuwa ni kero kwa watumishi wengine inadaiwa kwamba kuna
baadhi ya vigogo wa halmashauri hiyo na hata watendaji wa serikali ya
wilaya ya Mbinga, akiwemo mtumishi wa idara nyeti ya serikali wilayani humo, ambao wanamkingia kifua Pilli kwa maslahi
yao binafsi.
Katika kikao cha tathimini ya elimu kilichoketi hivi
karibuni mjini hapa chini ya Mwenyekiti wake mkuu wa wilaya hiyo Senyi
Ngaga, baadhi ya wadau wa elimu na madiwani wa halmashauri ya wilaya hiyo
waliitaka serikali kutomfumbia macho afisa huyo kutokana na kusababisha
migogoro ya mara kwa mara ambayo haina tija katika jamii.
Akizungumza kwa masharti ya kutotajwa jina lake, mmoja wa
wadau hao alisema Pilli ndiyo kikwazo namba moja cha elimu
katika wilaya ya Mbinga, lakini anashangaa hadi sasa serikali imekaa kimya licha
ya wadau wa elimu kutaka aondolewe wilayani humo kwani mambo hayo anayoyafanya
ni sumu kubwa katika maendeleo ya sekta hiyo muhimu.
Kwa upande wake afisa elimu ya msingi Bw. Mathias Mkali
alikiri kuwepo kwa mgogoro huo, ambao alisema sasa ni wa muda mrefu na kueleza
kuwa hayo yote yanafanyika kwa vile kuna vigogo wa wilaya na hata mkoa ambao
wamekuwa wakimkingia kifua Bw. Pilli ili asichukuliwe hatua za kinidhamu.
Bw. Mkali aliongeza kuwa, chanzo cha mgogoro huo ni
kutokana na maslahi binafsi waliyonayo vigogo hao akiwemo aliyekuwa Mkurugenzi wa
wilaya hiyo ambaye sasa amehamishwa kwenda wilaya mpya ya Nyasa Shaibu
Nnunduma, Mwenyekiti wa halmashauri ya Nyasa Oddo Mwisho na baadhi ya maafisa (majina tunayo)
ambao pia wanatajwa kushiriki katika mgogoro huo.
Alipotafutwa kuzungumzia tuhuma hizo, afisa taaluma Bw.
Pilli alikanusha vikali kuwepo kwa mgogoro huo na kuongeza kuwa kilichopo
ni tofauti za kawaida kati yake na bosi wake, hivyo haoni kama ni vurugu ambazo
zinachangia kukwamisha maendeleo ya elimu wilayani humo.
No comments:
Post a Comment