Waziri Mkuu Mizengo Pinda, akiwa katika kazi za ujasiriamali. |
Na Kassian Nyandindi,
Nyasa.
WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mizengo Pinda
leo anaendelea na ziara yake mkoani Ruvuma, ambapo kwa sasa yupo wilaya ya
Nyasa na atapokea taarifa ya maendeleo ya wilaya hiyo, katika kata ya Lituhi
wilayani humo.
Mkuu wa wilaya hiyo Ernest Kahindi akizungumza na mwandishi
wa habari hizi, alisema baada ya Waziri huyo kusomewa taarifa hiyo, ataelekea
katika kata ya Kihagara na kuweka jiwe la msingi kituo cha afya Kihagara,
kilichopo wilayani humo.
Vilevile Pinda baada ya hapo atafungua skimu ya mradi wa
umwagiliaji Lundo na jengo la Karakana lililopo katika mji wa Mbamba bay
wilayani Nyasa, ambalo linatumika kwa ajili ya kutengenezea boti za kisasa.
Kadhalika Kahindi alisema akitokea hapo ataelekea katika eneo
maalum ambalo limeandaliwa katika mji huo, kwa ajili ya kufanya uzinduzi wa
wilaya ya Nyasa ambapo uzinduzi utaenda sambamba na kuzindua boti moja kubwa, ambalo
litatumika kwa ajili ya shughuli za uvuvi.
Pamoja na mambo mengine Waziri Pinda baada ya kumaliza ziara
yake ya kikazi katika wilaya ya Nyasa, ataelekea wilaya ya Mbinga ambako
ameandaliwa kwa ajili ya mapumziko.
Siku inayofuata kiongozi huyo ataelekea mkoani Mtwara kwa
ajili ya shughuli ya kikazi, na atarejea tena wilayani Mbinga.
Mkuu wa wilaya ya Mbinga Senyi Ngaga, alisema Waziri Pinda ataendelea
na ziara yake wilayani Mbinga ifikapo siku ya Jumapili, Julai 21 mwaka huu kuanzia
majira ya saa nne asubuhi.
Atakapokuwa wilayani humo atasomewa taarifa ya maendeleo ya
wilaya na kuendelea na ziara yake, atatembelea na kwenda kuweka jiwe la
msingi katika kituo cha kuzalisha umeme wa maji, ambacho kinamilikiwa na mzawa ambaye ni mkazi
mmoja wilayani humo, aitwaye Menas Andoya.
Pia ataweka jiwe la msingi katika ujenzi wa stendi ya kisasa
ya mabasi ambayo inaendelea kujengwa mjini hapa, na baadaye kutembelea eneo la
kituo cha kufua umeme(TANESCO Power House) na hatimaye atahutubia wananchi.
No comments:
Post a Comment