Watoto wakichambua korosho. |
Na
Steven Augustino,
Tunduru.
SERIKALI imeahidi kufanya uchunguzi wa kina katika viwanda
10 vilivyo jengwa kwa ajili ya kubangulia korosho za wakulima nchini, ikiwa ni
juhudi ya kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa kero ya kukosekana kwa soko la uhakika
la zao hilo.
Sambamba na ahadi hiyo ya serikali pia imewahakikishia
wakulima wanaozalisha zao hilo kote nchini, kuwa itatoa fedha katika kipindi cha miezi
miwiIi ijayo baada ya utafiti huo
kufanyika, ili kuviwezesha viwanda hivyo
kununuaa mitambo mipya ya kisasa ambayo itarahisisha kazi ya ubanguaji wa
korosho.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mizengo
Pinda alisema hayo wakati akizungumza na wananchi wa wilaya ya Tunduru mkoani
Ruvuma, na kuongeza kuwa serikali imebaini kuwa kuna changamoto lukuki ambazo
wakulima wa zao la korosho wamekuwa wakikabiliana nazo na kurudisha nyuma
maendeleo yao.
Pia alieleza kuwa serikali imebaini kuwa utaratibu wa
kutumia stakabadhi ghalani ambao uliwekwa kwa ajili ya kuwalipa fedha zao wakulima
wa zao hilo katika awamu tatu kutoonesha mafanikio na hata ukiachwa uendelee
kwa muda mrefu hautawaletea tija wakulima hao.
Aidha katika hotuba hiyo pia Waziri pinda akaeleza
kuwa katika kuonesha kuwa maamuzi hayo siyo nguvu ya soda, alisema kuwa serikali
imejipanga kutoa fedha katika viwanda hivyo na kuviwezesha kununua vyenyewe korosho
kutoka kwa wakulima ili kukata mirija ya unyonyaji kwa kuwaondoa wakulima hao
katika mikono ya wanyonyaji.
Katika taarifa hiyo Waziri huyo alisisitiza kwamba
kufuatia hali hiyo tayari serikali imekwisha unda kikosi kazi cha watu watano
kitakachosimamiwa na Katibu mkuu wa kutoka katika Ofisi yake, na kwamba kazi ya
kwanza itakuwa ni kupita katika viwanda hivyo na kuchunguza kwa kina matatizo yanayokwamisha
visiweze kuendelea.
Hata hivyo Pinda ambaye alikuwa akihutubia wananchi katika uwanja wa Tunduru mjini,
alisema fedha zitakazotolewa na serikali katika kukuza maendeleo ya viwanda
hivyo, zitaelekezwa zaidi katika ununuaji wa mitambo mipya ya kubangulia
korosho za wakulima.
Waziri
Mkuu Mizengo Pinda leo ameondoka wilayani Tunduru, akiendelea na ziara yake
mkoani Ruvuma akielekea sasa wilayani Namtumbo.
No comments:
Post a Comment