Waziri mkuu wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Mizengo Pinda. |
Na Dustan Ndunguru,
Tunduru.
WAZIRI mkuu Mizengo
Pinda amesema kazi ya ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kutoka Namtumbo
hadi Tunduru ,yenye urefu wa kilometa 193 itaanza Oktoba mwaka huu ambapo
kukamilika kwake kutasaidia wananchi waepuke kero mbalimbali wanazokabiliana
nazo kwa sasa.
Akiongea mara baada ya
kukagua ujenzi wa chuo cha ualimu Kiuma kilichopo katika kijiji cha Milonde
tarafa ya Matemanga wilayani humo, na ambacho kinamilikiwa na taasisi ya Dkt. Matomora
alisema ujenzi wa barabara hiyo kimsingi ungekuwa unaendelea vizuri lakini
ulikwamishwa na mkandarasi aliyepewa kazi hiyo awali Progressive kutoka India.
Alisema serikali
inalifahamu tatizo hilo kubwa kwa wananchi wa mkoa huo hususani katika wilaya
za Namtumbo na Tunduru hasa baada ya mkandarasi huyo kusuasua kuijenga barabara
hiyo kwa wakati na kwamba kutokana na hilo kampuni hiyo imenyang'anywa kazi
hiyo na kupewa mtu mwingine ambaye atafanya kazi hiyo kwa uaminifu.
"Naomba wananchi
msiwe na wasiwasi serikali yenu itahakikisha barabara kutoka Namtumbo hadi
Tunduru inakamilika kwa kiwango cha lami kama ilivyopangwa,naomba msiwasikilize
wale ambao wanapita huku na kuwadanganya kuwa serikali imewasahau", alisema
Pinda.
Kwa mujibu wa waziri
mkuu fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo zipo na kwamba pia barabara
kutoka Tunduru hadi Mangaka yenye urefu wa kilometa 140 itajengwa kwa kiwango
cha lami, ambapo kukamilika kwa ujenzi wa barabara hizo kutapelekea wananchi wa
wilaya hiyo kuongeza hata uzalishaji wa mazao mbalimbali ya biashara kutokana
na ukweli kwamba watakuwa na uhakika wa kusafirisha kiurahisi kwenda kwenye
masoko.
Katika hatua nyingine
Pinda alisema serikali itaendelea kutambua michango mbalimbali inayotolewa na
taasisi binafsi, ikiwemo katika sekta ya elimu kwani jukumu la kuwaelimisha
watanzania ni la wote na kwamba kuiachia serikali pekee ni kuitwisha mzigo.
Akizungumza mara baada
ya kuweka jiwe la msingi katika ujenzi wa chuo cha ualimu Kiuma ambacho kwa
mwaka wa kwanza baada ya kukamilika kitachukua wanafunzi 300 wa diploma ya ualimu,
alisema kujengwa kwa chuo hicho ni mfano mzuri wa kuigwa kutokana na ukweli
kwamba wahitimu wake watasaidia kuondoa changamoto ya uhaba wa walimu kwa shule
za msingi na sekondari hapa nchini.
Pinda aliwataka watu
binafsi na taasisi zote nchini kuendelea kushirikiana na serikali yao katika
kuwaletea maendeleo watanzania na kwamba kamwe wasiwaunge mkono wale wote ambao,
siku zote wamekuwa wakibeza kila linalofanywa na serikali kwa wananchi wake.
Kuhusu zao la korosho
alisema ili kuepukana na tatizo la ukosefu wa soko la uhakika mipango
inafanyika ili badala ya kuwategemea wanunuzi binafsi kununua kwa wakulima
kiwanda cha kubangua zao hilo kipewe jukumu la kununua moja kwa moja kwa
wakulima jambo ambalo litapelekea wakulima waondokane na adha wanayoipata sasa.
Alisema wakulima
hawapaswi kukata tamaa ya kuendelea kuitunza miti ya mikorosho kwani serikali
yao ipo imara kuhakikisha hali hiyo ambayo ilijitokeza inakwisha na kwamba
wataalamu wa kilimo waendelee kutoa elimu kwa wakulima ili hatimaye waweze
kuzalisha mazao bora ambayo yatapelekea wapate bei nzuri sokoni.
Alisisitiza juu ya
kuimarisha mfumo wa stakabadhi ya mazao ghalani ambapo kwa kufanya hivyo
mkulima atakuwa na uhakika wa kupata mkopo wakati huo mazao yake yapo ghalani
yakisubiri bei nzuri na kwamba wakulima wenyewe wajiunge pamoja na kuanzisha
vikundi na kuimarisha vyama vyao vya ushirika hali ambayo itawafanya wauze
mazao yao kwa pamoja.
No comments:
Post a Comment