Na Mwandishi wetu,
Singida.
BAADHI ya wananchi mkoani Singida wamempora askari polisi bunduki aina
ya Sub Machine Gun (SMG) na risasi zake 30 baada ya kumshambulia askari
huyo, kwa mawe na fimbo.
Kutokana na tukio hilo watu 18 wanashikiliwa na Jeshi la
Polisi kwa tuhuma za kupora silaha hiyo na risasi na bunduki hiyo ambayo ina namba za
usajili 14300650.
Kamanda wa Polisi mkoani Singida, Geofrey Kamwela alisema
tukio hilo lilitokea majira ya saa 11:15, askari aliporwa silaha hiyo katika kijiji
cha Milade, kata ya Iguguno, tarafa ya Kinyangiri wilayani Mkalama.
Kamanda Kamwela alifafanua kwamba askari wawili walikwenda
kwenye kijiji hicho kwa lengo la kuchukua ng'ombe watano kama ushahidi
ambao waliokuwa wameibwa katika kijiji cha jirani cha Mukulu wilayani
Iramba.
Alisema kwamba baada ya ng'ombe hao kuibwa wananchi
walifanikiwa kuwakamata pamoja na kumkamata mtuhumiwa Ramadhan Mohamed
katika kijiji cha Milade na kumpeleka kwenye kituo kidogo cha polisi cha
Iguguno.
Ng'ombe hao ni mali ya Samwel Mlata (71) mkazi wa kijiji
cha Mukulu.
Lakini katika jambo la kushangaza polisi hao walipokwenda
kwenye kijiji cha Milade, hawakuwakuta ng'ombe hao.
Baada ya kutowakuta askari hao na uongozi wa kijiji
waliwafuatilia ng'ombe hao ili wakiwapata wawarejeshe mpaka kituo cha
polisi kwa ajili ya kufuata taratibu.
Lakini baada ya kufanikiwa kuwapata ng'ombe hao wananchi waligoma kuwaachia ng'ombe hao.
Wakati wakiendelea na majadiliano mwananchi mmoja alimrukia askari wenye silaha katika miguu yake na kumwangusha chini na wananchi wengine walimshambulia kwa mawe na fimbo na kuangusha silaha chini.
Mwisho, wananchi walichukua silaha na ng'ombe na kuondoka.
No comments:
Post a Comment