Monday, July 29, 2013

WAFANYABIASHARA SOKO KUU SONGEA WACHARUKA, WAPINGA MPANGO ULIOWEKWA NA MANISPAA HIYO

Kulia ni Mwenyekiti wa Umoja wa Wafanyabiashara wa Masoko Manispaa ya Songea(UWABIMASO) Karim Matumla, akiwa na Makamu Mwenyekiti wa Uwabimaso Leonard Chiunga wakifuatilia hoja mbalimbali kutoka kwa wanachama wa Uwabimaso.

Wanachama wa Uwabimaso wakifuatilia kwa makini kikao hicho chenye lengo la kupinga ongezeko la kodi la Vibanda vya Soko Kuu, na Kupinga tangazo la Zabuni lililotangazwa hivi karibuni.


   
Na Stephano Mango, 
Songea.
          
WAFANYABIASHARA katika Soko Kuu la Halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, wamepinga ongezeko la pango kwa asilimia 100 na tangazo la Zabuni  la ukodishaji wa vibanda hivyo lililotolewa na halmashauri hiyo hivi karibuni.
Akitoa maazimio ya kikao cha Umoja wa Wafanyabiashara Masoko ya Manispaa ya Songea(UWABIMASO) kilichofanyika mjini hapa kwenye ukumbi wa Saccos ya Walimu Songea vijijini, Mwenyekiti wa Uwabimaso Karim Matumla alisema kuwa wafanyabiashara wamepinga kwa nguvu zote mpango huo ambao waliuita kuwa ni wa kifisadi, ulioletwa na viongozi wa  halmashauri hiyo wa kuongeza kiwango cha kodi kwa asilimia 100 na tangazo hilo la Zabuni.
Matumla alisema kuwa mipango ya halmashauri kuhusu masoko yake haina ushirikishwaji wa pamoja kutoka pande zote mbili, jambo ambalo limekuwa likisababisha wanyabiashara hao na uongozi wa halmashauri hiyo kujenga migogoro mara kwa mara.
Alisema kuwa kwa muda mfupi wamepokea barua mbili zenye malengo tofauti ndani ya kipindi cha mwezi mmoja, hivyo inaleta mashaka kwao na kuwataka viongozi wa halmashauri hiyo kufanya kazi zao kwa weledi ikiwemo ushirikishwaji katika jamii.
Imeelezwa kuwa kitendo cha mkurugenzi kutoheshimu wala kutimiza makubaliano yao yaliyomtaka kuondoa kero wanazopata wafanyabiashara waliopo katika Masoko ya halmashauri hiyo ni kitendo cha dharau kwao.
“ Tulimtaka mkurugenzi katika vikao vyetu kuondoa mashimo na kuboresha mifereji na miundombinu mingine ndani ya masoko, wauza matunda watafutiwe eneo maalumu la biashara zao kwani kwa sasa wanazuia mizigo kuingia ndani na wateja wanapata kero ya kuhudumiwa, unyanyasaji unaofanywa na ofisa masoko uachwe na pia tulimuomba atukutanishe na viongozi wa halmashauri ili tutoe kero zetu, lakini yeye amekaidi”, alisema Matumla.
Alisema kuwa mnamo Mei 22 mwaka huu halmashauri ya Songea ilileta barua Uwabimaso ikitoa taarifa ya ongezeko la kodi ya pango kwa asilimia 80 kulingana na ukubwa wa chumba cha biashara kuanzia Julai 1 mwaka huu, kabla hawajaanza kuitekeleza, Julai 9 mwaka huu waliletewa barua nyingine yenye kutangaza zabuni ya ukodishaji wa vibanda hivyo, baada ya Uwabimaso kupinga ongezeko la pango la asilimia 80.
Vilevile kumekuwepo na mgongano wa kimaagizo kutoka katika Ofisi ya mkurugenzi wa halmashauri hiyo, kitendo ambacho kinaibua maswali mengi, hivyo Uwabimaso imeamua kwenda kwa Mwanasheria ili aweke zuio la mpango wa upandishaji wa kodi na utangazaji wa zabuni yenye lengo la kuwaondoa wafanyabiashara wote wa maduka katika soko hilo.
Akizungumza na Mwandishi wetu kwa njia ya simu mkurugenzi wa Manispaa hiyo Zakaria Nachoa alisema, halmashauri imekusudia kuongeza mapato yake kupitia miradi yake, hivyo mfanyabiashara ambaye hataki kuendana na utaratibu huo aache kibanda ili mfanyabiashara mwingine achukue, na baadaye alikata simu.

No comments: