Kaminyoge
Mhamerd akiwaelekeza Mameneja mitambo juu ya kahawa inayostahili kupokelewa
mtamboni mara baada ya kuchumwa kutoka shambani.
|
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
VIONGOZI wanaosimamia mitambo ya kukoboa kahawa vijijini,
wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, wametakiwa kuwa makini katika utekelezaji wa
majukumu yao ya kazi ili kuweza kuongeza ubora, wa uzalishaji wa kahawa wilayani humo.
Sambamba na hilo Mameneja waliopo katika mitambo hiyo ambao ndio
wasimamizi wakuu juu ya uendeshaji wa mitambo, hivyo nao wameshauriwa
kufanya
kazi kwa ukaribu na wakulima wanaozalisha zao hilo.
Rai hiyo imetolewa na mtaalamu wa mimea na udongo Kaminyoge Mhamerd
wa Kampuni ya Sustainable Harvest, kutoka wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro
ambayo hujishughulisha na uboreshaji wa zao la Kahawa, katika mafunzo ya siku
moja yaliyoshirikisha Mameneja wa mitambo ya kukobolea kahawa wilayani Mbinga, ambayo
yamefanyika kwenye ukumbi wa Kilicafe uliopo mjini hapa.
Alifafanua kuwa Mameneja hao wasipozingatia majukumu yao
ipasavyo, ubadhirifu katika mitambo hiyo unaweza ukatokea na kusababisha kuua
vyama vya ushirika na vikundi ambavyo hupeleka kahawa mbichi katika mitambo
hiyo, kwa ajili ya kukobolewa.
“Ndugu zangu uwazi kati ya mameneja na wahasibu wa mitambo
inatakiwa uzingatiwe ili kuepukana na vitendo vya wizi wa kahawa, jengeni
ushirikiano na uaminifu tuweze kuendeleza ubora wa zao hili”, alisisitiza
Kaminyoge.
Aidha aliongeza kuwa uhai wa vikundi katika mitambo ni
makusanyo ya kahawa bora, na watendaji wa vikundi husika kufanya kazi kwa
kutumia ubunifu wa hali ya juu, ili kuepukana na malalamiko yasiyokuwa ya
lazima miongoni mwa jamii.
Pia alieleza kwamba vibarua wanaofanya kazi mitamboni
inatakiwa wasimamiwe kikamilifu kwa kuhakikisha wanafanya kazi kwa muda
waliopangiwa, na kwamba Meneja aliyekuwa katika mtambo husika kila siku
ahakikishe anapofunga kituo cha mtambo anatakiwa awe anafanya kikao na
wasaidizi wake, kwa kutoa taarifa za utendaji wa kazi iliyofanyika kwa siku
nzima.
Pamoja na mambo mengine Mameneja walioshiriki katika mafunzo
hayo walitoka katika vikundi vinavyozalisha kahawa bora wilayani Mbinga,
ambavyo ni Unango, Lumeme, Jikwamue, Chemichemi, Mikalanga, Bagamoyo, Jitahidi
na Ukombozi.
No comments:
Post a Comment