Katibu wa CWT wilayani Mbinga, Samwel Mhaiki. |
Na Mwandishi wetu,
Mbinga.
KATIKA hali inayoonesha kuwa ni matumizi mabaya ya madaraka
na ukiukaji wa taratibu na sheria za utumishi wa umma, Katibu wa Chama Cha Walimu
Tanzania(CWT) tawi la Mbinga mkoani Ruvuma, Samwel Mhaiki ananyoshewa kidole na
wanachama wa chama hicho wilayani humo, akidaiwa kutowalipa baadhi ya wanachama
fedha zao zinazotokana na asilimia 15 ya
makato yatokanayo na mishahara yao ya kila mwezi.
Wamezungumza na mwandishi wetu kwa nyakati tofauti wilayani
hapa, wakisema Katibu huyo amekuwa akifanya kitendo hicho, kwa kushirikiana na
Mwenyekiti wake wa wilaya hiyo Batson Mpogolo.
Pia wanachama hao wengi wao wametishia kujiondoa uanachama katika
umoja huo na kusema wakisha kamilisha mchakato huo wa kujitoa, wapo tayari
kwenda kufungua kesi Mahakamani dhidi ya Katibu wao wa wilaya hiyo na
Mwenyekiti, ili waweze kulipwa fedha zao wanazodai.
Vilevile viongozi hao wa CWT wamekuwa wakilalamikiwa kwamba,
ni zaidi ya miezi 20 sasa walimu wengi waliopo wilayani Mbinga hawajalipwa
fedha hizo.
Kadhalika muda mwingi wamekuwa wakionekana wakiwa safarini
kuelekea Manispaa ya Songea hususani kwa siku za mapumziko yaani Jumamosi na
Jumapili kwa kutumia wakati mwingine gari la chama la wilaya hiyo.
Kitendo hicho cha kusafiri mara kwa mara katika siku za kazi
na kwenda huko, walieleza wakidai kuwa wanamashaka na safari zao wanazozifanya
na huenda wakawa wanafuja fedha hizo kwa kufanya starehe au kwa manufaa mengine
binafsi.
“Hizi safari za mara kwa mara zinatutia mashaka, huenda huko
wanakula bata kwa kutumia fedha zetu hizi za makato ya kila mwaka lakini
viongozi wetu wa CWT mkoa na taifa wapo kimya wameziba masikio hakuna hatua
iliyochukuliwa licha ya sisi wanachama kulalamika kwa muda mrefu”, walisema.
Aidha walimu hao walifafanua kuwa viongozi hao wamekuwa muda
mwingi wakipita katika matawi yao mashuleni huko vijijini, na kufanya usanii wa
danganyatoto kwa kuonyesha wanawapenda wanachama wao
matawini pale wanapowatembelea.
Wakati mwingine wanapopita huko matawini wanadaiwa kupita
kuhamasisha migomo isiyokuwa na msingi wowote, ambayo hujenga ugombanishi kati
ya serikali na mwajiri wao.
Pamoja na mambo mengine walieleza kuwa wamechoshwa na vitendo
hivyo na kuahidi kwamba wanachohitaji ni kuona makato yao yanarejeshwa kwa mujibu
wa taratibu za chama zinavyosema na sio vinginevyo.
Hata hivyo Mwandishi wetu hivi karibuni, alipomuuliza Katibu
wa CWT wa wilaya ya Mbinga Samwel Mhaiki ili aweze kutolea ufafanuzi juu ya
tuhuma hizo alisema, yeye hakuna mwalimu anayemdai na malipo kwa wanachama wake
yamekwisha lipwa lakini pia alipotafutwa Mwenyekiti wake Batson Mpogolo,
hakuweza kupatikana na simu yake muda mwingi ilikuwa imefungwa.
No comments:
Post a Comment