Mwenyekiti wa CWT Taifa, Grattian Mukoba. |
Na Kassian Nyandindi,
VIONGOZI wa Chama Cha Walimu Tanzania (CWT) tawi la Mbinga mkoani
Ruvuma, wanalalamikiwa na walimu ambao ni wanachama wa chama hicho wilayani
humo, kwa kutowalipa fedha za marejesho ya asilimia 15 kutoka kwenye makato ya
mishahara yao.
Nionavyo kwa hakika hii ni dharau na dhuluma ni vyema sasa
wahusika wachukuliwe hatua kwa kutotimiza wajibu wao ipasavyo kwa wanachama hao.
Nahoji, Katibu wa CWT na Mwenyekiti wako mnafanya nini, hizi fedha
mmezipeleka wapi? tunaomba sasa tupate majibu ili tuweze kujiridhisha juu ya
malalamiko haya.
Ni malalamiko ambayo sasa yamedumu kwa muda mrefu, wanachama
nimezungumza nao baadhi yao kwa nyakati tofauti wanasikitika wakisema wengine
ni zaidi ya miezi 24 hadi 30 fedha zao wengi wao bado hawajalipwa.
Hii ni dhambi jasho la mtu huwa halipotei bure ni vyema sasa
tukawa wastaarabu kwa kuchukua hatua mapema, katika kunusuru hali hii ambayo
mbele tunaweza tukatengeneza shimo la kutumaliza wenyewe.
Uongozi wa namna hii haufai katika jamii, kila kukicha wanachama wamekuwa
wakikinyoshea kidole CWT Mbinga, ni dhahiri sasa tunaonesha udhaifu katika
utendaji wetu wa kazi, yatupasa sasa tubadilike !
Zama za watu kudanganywa na kupigwa danadana zimepitwa na wakati, kwa
hili la marejesho ya makato ya mishahara ya walimu ni vyema tukae mezani na
kulifanyia kazi haraka.
Nimeambiwa na wanachama wengi kwamba endapo suala hili litaendelea
kuwa sugu, wametishia kujitoa uanachama, nasema endapo itakuwa hivyo hili litakuwa
ni pigo kubwa kwa uongozi wa chama cha walimu Mbinga, na jamii sasa itatucheka
na kutuzomea hata tutakapokuwa tukipita barabarani.
Kumekuwa na hata tabia ya kupakana matope na kumchafua ofisa elimu
wa wilaya hiyo Mathias Mkali, kuwa anahamasisha walimu wajitoe, nimefanya mahojiano
na baadhi ya walimu wanasema wao ni waelewa na wana akili timamu hawawezi
kuhamasishwa na mtu mmoja juu ya kujitoa katika chama hicho, bali wanachohitaji
ni kulipwa madai yao ya makato ya mishahara yao kila mwezi.
Wengine walisema huyo ofisa elimu tangu amekuja hapa wilayani
ameweza kuhakikisha stahili zao za msingi ikiwemo uhamisho, likizo, matibabu na
masomoni wamelipwa kwa wakati; tofauti na siku za nyuma walikuwa wakipata shida.
Wengine wamefafanua kwamba Mkali amekuwa ni mtu msikivu pale wanapokuwa na shida zao za msingi, na
amekuwa akihimiza utendaji bora wa kazi mashuleni.
Wanasema leo wanashangaa kuona maneno hayo yanatoka wapi, kwa
ujumla viongozi wa CWT Mbinga wamepoteza mwelekeo na malengo ya chama hicho,
sasa wanahangaika kuziba jua kwa ungo, ukweli upo bayana tunachohitaji hapa
walimu walipwe madai yao ya msingi.
Wahenga walisema, Cheo ni dhamana hivyo hatuna budi kuihudumia
jamii iliyotuweka madarakani, kwa misingi ya utawala bora ili tuweze kuondoa
malalamiko na mitafaruku isiyokuwa na tija.
Katibu wa CWT uliopo Mbinga, sote tunafahamu ndiyo mtendaji mkuu
wa kuliongoza jahazi hili la chama hapa Mbinga, sasa kama matatizo haya
yanaendelea kweli tutafika?.....tubadilike.
Yawezekana viongozi wa ngazi ya mkoa na taifa, mmefumbwa macho na uongozi
wa CWT wilaya ya Mbinga ! ndio maana hakuna hatua zinazoonesha kuzaa matunda
licha ya malalamiko haya kudumu kwa kipindi kirefu sasa. Ama kweli tunaweza
kusema ufisadi upo kila kona !
Nashauri kilio hiki cha wanachama wa chama hicho hapa wilayani ni
vyema kikafanyiwa kazi haraka, ikiwezekana hata viongozi wa ngazi ya juu
serikalini ingilieni kati suala hili ili wanachama husika waweze kupata haki
zao za msingi, vinginevyo tukiendelea kufumbia macho hatutawatendea haki
wanakondoo hawa wa Mbinga, ambao kilio chao kimedumu kwa muda mrefu sasa……..
tuchukue hatua.
Mungu ibariki Mbinga na Tanzania kwa ujumla,
Mwandishi wa makala haya anapatikana kwa simu namba 0762578960.
No comments:
Post a Comment