Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
MAPYA yameibuka juu ya sakata la Padre mmoja wa Kanisa Katoliki
hapa nchini, Peramiho Seminari jimbo la Songea mkoani Ruvuma, Xavery Kazimoto
Komba ambaye alikamatwa na kuwekwa mahabusu, leo amepandishwa kizimbani katika
Mahakama ya wilaya ya Mbinga mkoani humo, kwa tuhuma ya kutoa hongo ya shilingi
milioni 1 kwa Mkuu wa wilaya hiyo Senyi Ngaga, kwa lengo la kumshawishi asichukuliwe
hatua kwa makosa aliyofanya ya kuwatapeli baadhi ya wakulima wa kahawa wilayani
humo.
Padre huyo anatuhumiwa kufanya utapeli huo kwa kutumia
kampuni yake ambayo hujishughulisha na kununua kahawa, inayofahamika kwa jina
la Songea network Company Limited ambayo yeye ndiye Mkurugenzi wa kampuni hiyo.
Inadaiwa kuwa Kasisi huyo wa kanisa Katoliki alikamatwa na
kuswekwa mahabusu katika Kituo kikuu cha Polisi wilayani humo, mapema Julai 19
mwaka huu majira ya mchana, kufuatia kutoa hongo ya fedha hizo kwa kutumia utaratibu
wa M – pesa kwenda namba ya simu ya Mkuu wa wilaya hiyo ambazo mahakamani hapo
hazikutajwa.
Ilidaiwa Mahakamani hapo na Mwendesha mashtaka wa Taasisi ya
Kuzuia na Kupambana na Rushwa(TAKUKURU) mkoani Ruvuma, Bi. Maria Mwakatobe mbele
ya Hakimu mkazi mfawidhi wa wilaya ya Mbinga, Geofrey Mhini kuwa Xavery Kazimoto
Komba anadaiwa kufanya kosa hilo Mei 20 mwaka huu na Mei 26 mwaka huu katika
majira tofauti.
Mwakatobe aliendelea kudai kwamba Padre huyo anatuhumiwa
mnamo Mei 20 mwaka huu alituma kiasi cha shilingi 400,000 na Mei 26 mwaka huu
alituma tena shilingi 600,000 kwenda namba ya simu ya Mkuu wa wilaya ya Mbinga Senyi
Ngaga, akiwa na lengo la kumshawishi mkuu wa wilaya hiyo asimchukulie hatua
kufuatia shauri ambalo lilikuwa kisheria katika ofisi yake.
Mwendesha mashtaka huyo wa TAKUKURU aliieleza mahakama kwamba
upelelezi wa shauri hili umekamilika, hivyo dhamana kwa mshtakiwa ipo wazi na
kuitaka mahakama ifuate mkondo wake wa kisheria.
Kabla ya Hakimu mkazi wa mahakama hiyo kutoa masharti ya
dhamana upande wa utetezi wa mshtakiwa uliomba kupewa nafuu ya dhamana ambapo, hakimu
mkazi mfawidhi, Mhini alisema dhamana kwa mshtakiwa Xavery Kazimoto Komba ipo
wazi kwa masharti ya mdhamini mmoja mwaminifu mwenye uwezo wa kuweka “bondi” ya
shilingi milioni 3.
Ambapo baada ya tukio hilo mdhamini aliyeandaliwa na ndugu wa
mshtakiwa kwa ajili ya kumdhamini, alijitokeza Mahakamani hapo na
kujitambulisha kwa jina la Prosper Mahay, akiwa na barua za utambulisho kutoka
kwa Mwenyekiti wa mtaa anaoishi hapa Mbinga mjini na vielelezo vingine vya umiliki
wa nyumba yake moja, iliyopo kitongoji cha Manzese hapa Mbinga mjini.
Mdhamini huyo baada ya kutoa vielelezo hivyo, mahakama
iliriridhia na kutoa dhamana kwa mshtakiwa, na kupanga tena siku ya shauri hilo
ambalo litakuja kwa ajili ya kusomwa maelezo ya awali mahakamani hapo Agosti 12
mwaka huu.
No comments:
Post a Comment