Mama Tunnu Pinda. |
Na Steven Augustino,
Tunduru.
WAZAZI
na walezi wilayani Tunduru mkoani
Ruvuma, wamehimizwa kupeleka watoto wao katika Kituo cha maendeleo KIUMA ili
waweze kupata elimu na kuwawezesha kujiendeleza.
Wito
umetolewa na mke wa Waziri mkuu Mama Tunnu Pinda, wakati akiwasalimia wananchi
wa kijiji cha Milonde wilayani humo, muda mfupi baada ya Waziri mkuu wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa chuo cha ualimu ngazi
ya Diploma ambacho kinajengwa na taasisi
hiyo.
Mama
pinda alieleza kwamba endapo watapeleka vijana wao kupata elimu katika taasisi
hiyo, pamoja na mafanikio watakayo yapata pia watalisaidia taifa la watanzania
kwa kuongeza idadi ya wataalamu watakao toa huduma katika maeneo yao.
Alisema
kitendo hicho kadhalika wananchi hao watakuwa wametoa mchango mkubwa wa
maendeleo katika wilaya yao na mkoa kwa ujumla tofauti na sasa ambapo wilaya
yao inakabiliwa na changamoto lukuki za kukosa wataalamu katika idara mbalimbali
zinazotoa huduma katika jamii.
Awali
akisoma taarifa ya kituo hicho, Mkurugenzi wa kituo hicho Dkt. Matomora
Matomora alisema kituo hicho ambacho kinamilikiwa na Kanisa la Upendo wa Kristo
Yesu masihi, kilijengwa mwaka 1996 kwa lengo la kutoa huduma mbalimbali katika
eneo hilo, hadi sasa kimefanikiwa kujenga hospitali yenye vitanda 100 na
kufanikiwa kuokoa maisha zaidi ya wanawake 150 kila mwaka ambao hujifungua kwa
njia ya upasuaji.
Dkt.
Matomora alibainisha kuwa huduma nyingine zinazopatikana katika kituo chake kuwa
ni pamoja na chuo cha ufundi kinachotoa mafunzo na sasa zaidi ya mafundi 200 wa
ujuzi wa aina mbalimbali hutolewa kwa mwaka, kinamiliki pia shule ya sekondari
yenye kidato cha kwanza hadi cha sita, chuo cha uuguzi, chuo cha kilimo na
mifugo na sasa kinajenga chuo hicho cha ualimu ngazi ya diploma kinacho
tarajiwa kufunguliwa mapema Agosti 2014 mwakani, kwa kuanza na wanafunzi 320 huku
uongozi husika ukiwa na malengo ya kupanua majengo yake na kuongeza idadi hiyo
mara mbili zaidi kuanzia mwaka 2015 na kufikia wanafunzi 640.
Akifafanua
upande wa huduma za hospitali Dkt. Matomora alisema kuwa taasisi hiyo pia
imejipanga kuhakikisha kuwa inaongeza idadi ya vitanda vyake kutoka 100 hadi
200 ili kuongeza ufanisi na kuboresha upatikanaji wa huduma bora za afya katika
wilaya hiyo.
No comments:
Post a Comment