Gari lenye namba za usajili T. 856 CFL mali ya Medson Ulendo mkazi wa Mbinga mjini, lipo chini ya ulinzi katika kituo kikuu cha polisi wilaya Mbinga, ambalo lilikuwa likitumika kutorosha kahawa tani 10,000 kutoka kijiji cha Langiro wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma. Gari hilo lilikamatwa katika kijiji cha Kitai kwenye geti la kukagua mazao ya maliasili wilayani humo.(Picha zote na Kassian Nyandindi)
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
HALMASHAURI ya wilaya ya Mbinga
mkoani Ruvuma, imemkamata mfanyabiashara mmoja maarufu, ambaye alikuwa
akitorosha kahawa tani 10 yenye thamani ya shilingi milioni 28 kutoka wilayani
humo kuelekea mkoani Mbeya, kwa lengo la kukwepa kulipa ushuru wa halmashauri
hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari,
Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya hiyo Allanus Ngahi alisema kahawa hiyo
ilikamatwa Agosti 21 mwaka huu kijiji cha Kitai wilayani humo, majira ya saa
tano usiku katika geti la kukagua mazao ya maliasili ikiwa inasafirishwa kwenye
gari aina ya Scania lenye namba za usajili T. 856 CFL mali ya Medson Ulendo
mkazi wa mjini hapa.
Ngahi alisema kahawa hiyo
iliyokamatwa ni mali ya mfanyabiashara Madawa
Mwaijande ambaye ni wa Mwanjelwa mkoani Mbeya, ambapo wakati anakamatwa alikuwa
na dereva aliyekuwa akiendesha gari hilo aliyemtaja kwa jina la Julius Kinunda.
Alifafanua kuwa kukamatwa huko
kunatokana na halmashauri ya wilaya ya Mbinga, kuendelea kupambana vikali na
wafanyabiashara wajanja ambao wanatabia ya kuhujumu ushuru wa halmashauri hiyo
kwa njia za kutorosha mazao yanayozalishwa wilayani humo.
“Wafanyabiashara hawa wamekamatwa na
kahawa hii, wakiwa wanatokea Kata ya Langiro hapa wilayani, hivyo kahawa
iliyokamatwa ni magunia 200 yenye jumla ya kilo 10,000”, alisema.
Hata hivyo Mwenyekiti huyo alieleza
kuwa kahawa hiyo imechukuliwa na halmashauri hiyo na itauzwa hapo baadaye,
baada ya taratibu husika za kisheria kufuata mkondo wake.
|
No comments:
Post a Comment