Mkuu wa Wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Senyi Ngaga. |
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
KIGOGO mmoja wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma,
anadaiwa kuhusika katika vitendo vinavyofanywa na baadhi ya wafanyabiashara wa
zao la kahawa wilayani humo, la utoroshaji wa zao hilo kwa lengo la kukwepa kulipa ushuru jambo
ambalo linasababisha halmashauri hiyo kukosa mapato.
Wakizungumza na waandishi wa habari kwa nyakati tofauti mjini
hapa, wafanyabiashara hao walitoboa siri hiyo kwa kumtaja jina kuwa ni, Mshauri wa
zao la kahawa wilayani humo Gotham Haulle ambaye ni mmoja kati ya maofisa
kilimo amekuwa akijihusisha na biashara ya ununuzi wa kahawa vijijini kwa
kuwatumia wafanyabiashara wajanja ambao huwarubuni wakulima kwa kununua zao
hilo kwa bei ya chini.
Aidha walisema tukio la kukamatwa kwa mfanyabiashara Madawa
Mwaijande la utoroshaji wa kahawa kavu tani 10 yenye thamani ya shilingi
milioni 28 Agosti 21 mwaka huu majira ya usiku katika kijiji cha Kitai, Haulle
anahusishwa katika tukio hilo kwa kile kinachodaiwa kuwa ofisa kilimo huyo
amekuwa akishirikiana kufanya biashara hiyo na mfanyabiashara huyo.
Mfanyabiashara huyo
alikamatwa akitorosha kahawa hiyo kuelekea Jijini Mbeya kwa lengo la kukwepa
kulipa ushuru akiwa na gari lenye namba za usajili T 856 CFL mali ya Medson Ulendo mkazi wa mjini hapa.
Vilevile baadhi vigogo wa halmashauri hiyo ambao majina yao
hawakutaka yatajwe katika mtandao huu, wamemnyoshea kidole mtumishi mwenzao wakisema,
muda mwingi amekuwa hakai ofisini kutokana na kukabiliwa na shughuli ya biashara
hiyo ya kahawa badala ya kutekeleza majukumu yake ya msingi aliyopewa na
serikali.
“Hii kahawa tuliyoikamata juzi tumefanya utafiti na kubaini
kwamba huyu mfanyakazi mwenzetu anahusika kwa kiasi kikubwa na biashara hii,
lakini tupo katika hatua ya kuchukua maamuzi sahihi ambayo yatasaidia kudhibiti
vitendo hivi viovu vinavyolenga kuikosesha halmashauri mapato yake”, alisema
mmoja kati ya vigogo wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga.
Pamoja na mambo mengine Waandishi wa habari walipofanya
mahojiano na Mshauri huyo wa zao la kahawa wilaya ya Mbinga Gotham Haulle juu
ya kuhusishwa na tuhuma za kushirikiana na wafanyabiashara kutorosha kahawa kwa
lengo la kukwepa kulipa ushuru huo, alikana huku akisema yeye anazobiashara zake zingine
ambazo huzifanya na kumuingizia kipato.
“Mimi kwa kifupi nina hela nyingi sana, haya maneno
yanayozungumzwa ni kutaka kumchafua mtu tu, na hii ni kawaida kwa vijana wahuni
wakitaka kumharibia mtu lazima wamhusishe
na matukio maovu”, alisema Haulle.
Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo Hussein
Issa Ngaga alipoulizwa na waandishi wa habari alithibisha kuwepo kwa tukio hilo na
kusema, anazotaarifa kuwa baadhi ya watumishi wake wamekuwa wakijihusha na
biashara ya ununuzi wa kahawa huku wakishirikiana na wafanyabiashara wengine
wilayani humo kuhujumu mapato ya halmashauri hiyo.
Ngaga alisema katika kukabiliana na hali hiyo tayari kuna
kamati husika imeundwa ambayo hufanya kazi ya kufuatilia vitendo hivyo viovu na wale
watakaobainika, watachukuliwa hatua stahiki za kisheria na kwamba alikemea
kitendo cha watendaji kuacha shughuli za kiutumishi na kupoteza muda mwingi
kufanya shughuli zao binafsi, huku kazi za utumishi wa umma walizoajiriwa nazo
zikiendelea kuzorota.
No comments:
Post a Comment