Kamanda wa polisi mkoa wa Ruvuma, Deusdedith Nsimeki. |
Na Kassian Nyandindi,
Namtumbo.
WATOTO wa nne wa familia moja kijiji
cha Ligunga Kata ya Lusewa tarafa ya Sasawala wilayani Namtumbo mkoa wa Ruvuma wamefariki
dunia kwa kile kinachodaiwa kuwa baada ya kula chakula chenye sumu.
Kufuatia tukio hilo, aidha wengine
12 wamelazwa katika hospitali ya mkoa huo iliyopo Songea mjini, na wengine katika
kituo cha afya Lusewa wilayani Namtumbo kwa madai ya kula chakula hicho.
Waandishi wa habari wamezungumza na katibu
tarafa wa Sasawala Fred Maliyao alisema wanafamilia hao walikula vyakula karibu
aina tatu na baadaye kupatwa na matatizo hayo.
Maliyao alifafanua kuwa katika siku
ya sikukuu ya Idd wanafamilia hao walikula ugali na samaki, mbogamboga na
utumbo wa kuku ambao unasadikika ulikuwa umechemshwa mchuzi wa samaki huku
wengine walikula ugali kwa mboga ya mbaazi.
Alieleza kwamba walikuwa wakila
vyakula hivyo wakiwa kwa baba yao mdogo na mkubwa kwa zamu, ambapo
walikuwa wakisherehekea sikukuu hiyo ya Idd.
Kwa upande wake mwanafamilia mmoja Bilahi
Mumba alisema kuwa tukio hilo lilitokea Agosti 9 mwaka huu majira ya saa 5 asubuhi
hadi majira ya mchana, baada ya watoto hao kula chakula hicho chenye sumu.
“Nasisi tunashangaa tuliona muda mfupi baada
ya kula chakula hicho walianza kuanguka na wengine kutapika huku tukijitahidi
kuokoa maisha ya watoto hao, lakini wanne wameweza kufariki na wengine
tuliwakimbiza kituo cha afya cha Lusewa”, alisema.
Mumba aliwataja watoto hao waliokufa
kuwa ni Zidane Mumba[25] Tazamio Mumba[9] Selemani Mumba[7] na Zahara Mumba[2] wakiwa
wote wa familia moja.
Naye muuguzi wa kituo cha afya Lusewa
Edrisa Ndauka alisema kuwa walipokelewa wagonjwa 16 katika kituo hicho, na
wanne walifariki watano walikimbizwa hospitali ya mkoa Songea na kuwa wengine
walibaki kituoni hapo.
Hata hivyo mkuu wa wilaya ya
Namtumbo mkoani Ruvuma, Abdula Lutavi ambaye naye alishuhudia tukio hilo,
alisema kuwa tatizo hilo ni kubwa hivyo serikali wilayani humo, italifanyia
uchunguzi wa kina.
Lutavi alisema licha ya watalamu
kuchukua matapishi na mabaki ya vyakula hivyo kwa kwenda kuvipima, lakini
taarifa za awali zinaonyesha kuwa sumu iliwekwa kwenye samaki.
Mkuu huyo wa wilaya ametoa onyo
kwa baadhi ya watu wa kijiji hicho, ambao huvua samaki kwa kutumia
sumu mbalimbali ikiwemo za zao la Tumbaku, kwa ajili ya kujipatia kitoweyo, sasa
waache mchezo huo badala yake watumie a bora zinazokubalika katika uvuvi.
Kamanda wa polisi mkoani Ruvuma
Deusdedith Nsimeki amethibitisha kutokea kwa tukio hilo, na kwamba hivi sasa mtu
mmoja anayejulikana kwa jina moja la
Salum anashikiliwa kwa mahojiano zaidi kuhusiana na tukio hilo.
No comments:
Post a Comment