Friday, August 30, 2013

BAADHI YA WATUMISHI WA IDARA YA KILIMO MBINGA WADAIWA KUHUSIKA NA UTOROSHAJI WA KAHAWA

Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Said Thabit Mwambungu.

 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
 
MTANDAO wa kuhujumu mapato ya Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, kupitia utoroshaji wa zao la kahawa umezidi kubainika kufuatia kuwepo kwa baadhi ya watumishi wa wilaya hiyo kuhusika na biashara ya zao hilo.

Utoroshaji huo wa kahawa kavu umekuwa ukifanyika kwa kasi kubwa tangu kuanza kwa msimu wa mavuno Julai mwaka huu, ambapo baadhi ya wafanyabiashara kwa kushirikiana na watumishi kutoka idara ya kilimo wamekuwa wakisafirisha kahawa hiyo kwenda wilayani Mbozi mkoa wa Mbeya kwa lengo la kukwepa ushuru.

Kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa na mtandao huu umebaini kuwa watumishi hao (majina tunayo) ambao wapo watatu mpaka sasa ndio wamekuwa vinara wa kuhujumu uchumi wa Mbinga kupitia biashara ya zao hilo na kwamba tayari uongozi wa ngazi ya juu wa wilaya hiyo umeunda timu ya kufanya uchunguzi juu ya suala hilo.

Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga Allanus Ngahi amekiri kuwepo kwa baadhi ya watumishi wa iadara hiyo kuhusika na utoroshaji wa kahawa, ambapo alisema watumishi hao wanafahamika hivyo hapo baadaye taarifa rasmi itatolewa na hatua zitachukuliwa dhidi yao.

Ngahi alisema mpaka sasa zaidi ya tani 20 za kahawa zimekamatwa katika maeneo mbalimbali wilayani humo, ambazo zilinunuliwa kwa wakulima kwa bei ya chini kinyume na taratibu husika huku ununuzi huo ukiwahusisha watumishi hao na wafanyabiashara ambao wamekuwa wakishirikiana nao.

Kwa upande wake Meneja wa kiwanda cha kukoboa kahawa Mbinga(MCCCO) Jonas Mbunda aliwaeleza Waandishi wa habari kuwa kiwanda hicho kinatarajia kukoboa tani 7500 za kahawa msimu huu lakini huenda wakashindwa kufikia malengo kutokana na vitendo vinavyofanywa na wafanyabiashara vya utoroshaji wa kahawa.

Mbunda alizitaja athari za utoroshaji huo kwamba kiwanda kinakosa kahawa ya kukoboa, halmashauri ya Mbinga inakosa mapato na huku ajira zilizokuwa zikitolewa kiwandani hapo kwa wananchi kukosekana kutokana na kutokuwepo kwa uwingi wa kahawa.

Alikemea kuwepo kwa hali hiyo na kuwataka viongozi katika halmashauri hiyo kujenga ushirikiano wa dhati katika kupambana na vitendo hivyo ili kunusuru mapato yatokanayo na zao hilo kutokana na ukweli kwamba wilaya hiyo kwa kiasi kikubwa uchumi wake hutegemea uzalishaji wa zao hilo.

              

No comments: