Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Kassim Majaliwa. |
Na Kassian Nyandindi,
Ruvuma.
HATIMAYE Baraza la Madiwani katika
Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, limemaliza mzizi wa fitina kwa kumkataa aliyekuwa Ofisa elimu
wa wilaya hiyo Hanji Yusuph Godigodi na kusema kuwa hawataki kumuona ndani ya
wilaya hiyo, akiendelea kufanya kazi za utumishi wa umma.
Kukataliwa kwa Ofisa huyo kumefuatia
baraza hilo kuketi kama kamati kwa muda wa nusu saa kujadili suala hilo, likizingatia tamko
lililotolewa na Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Ofisi ya Waziri Mkuu
Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Kassim Majaliwa, Februari 7
mwaka huu wakati alipokuwa katika ziara yake ya kikazi wilayani humo.
Jukumu la kuketi kama kamati lilifuatia
kuwepo kwa mchezo mchafu ambao ulikuwa ukisukwa chini kwa chini na baadhi ya
vigogo wa ngazi ya mkoa huo na wilaya, kwa lengo la kutaka kumrejesha
madarakani Ofisa huyo ili aendelee na kazi yake kama kawaida.
Majaliwa alitoa tamko la kumvua
madaraka kwa kumshusha cheo Ofisa huyo
wa elimu sekondari wilayani humo, na wenzake sita ambao ni walimu wakuu wa
shule za sekondari, kufuatia kushindwa kutekeleza majukumu yao ya kazi na
kufanya ubadhirifu wa zaidi ya shilingi milioni 268 za maendeleo ya elimu ya
sekondari.