Wednesday, December 5, 2012

AFARIKI DUNIA BAADA YA KUNYWA GONGO


Na Mwandishi maalum,
Tunduru.

MTU mmoja mkazi wa Tunduru mjini mkoani Ruvuma, amefariki dunia wakati akiendesha mkokoteni ambao huutumia kubebea mizigo ya aina mbalimbali ya wateja wake, baada ya kunywa pombe haramu aina ya gongo.

Aliyefariki hufahamika kwa jina la Rashid Mpembu kwa jina maarufu “Wamunyama”(43) ambapo kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na mashuhuda wa tukio hilo, walisema kuwa Mpembu alianguka ghafla na kupoteza maisha wakati akisukuma mkokoteni huo.

Walisema tukio hilo lilitokea wakati akiwa amebeba viroba viwili vya mahindi ambayo inadaiwa kuwa alikuwa akiwapelekea wateja wake, kukoboa na kusaga katika mashine mojawapo mjini Tunduru.


Mashuhuda hao waliendelea kueleza kuwa mzigo huo ambao ulishushwa katika maeneo ya benki ya NMB mjini humo aliuchukua kwa madhumuni hayo lakini kwa bahati mbaya hakuweza kuufikisha mzigo huo katika mashine iliyo lengwa, baada ya kukaa chini kwa lengo la kupumzika na kufariki dunia wakati
akiwa katika eneo la Amazon Bar.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na mganga aliyeufanyia uchunguzi mwili wa marehemu huyo, Dkt.Vitaris Lusasi alieleza kuwa chanzo cha kifo hicho kilisababishwa na unywaji wa Pombe nyingi bilaa kula.

Wakiongea kwa nyakati tofauti baadhi ya wasukuma mikokoteni wenzake kwa masharti ya kutotajwa majina yao, walisema kuwa kabla ya tukio hilo marehemu alikuwa ametoka kunywa pombe aina ya Gongo.

Walisema kutokana na hali hiyo kuna mashaka kuwa huenda pombe aliyokunywa ilikuwa ya moto ambayo walidai kuwa ikiwa katika hali hiyo huwa ni hatari kwa maisha ya wanywaji.

Kamanda wa polisi wa mkoa wa Ruvuma Bw. Deusdedith Nsemeki amwethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuongeza kuwa polisi
wanaendelea na uchunguzi.

No comments: