Sunday, December 9, 2012

MTUHUMIWA WA MAUAJI AACHIWA HURU



Na Steven Augustino,
Tunduru.

MAHAKAMA Kuu kanda ya Songea mkoani Ruvuma kupitia vikao vyake vinavyoendelea wilayani Tunduru, imemuachilia huru Suzana Kapinga(28) aliyekuwa anakabiliwa na shauri  namba Rm11/2012 la mauaji ya kukusudia, kinyume cha sheria kifungu namba 196 sura ya 16 cha kanuni ya adhabu.

Pamoja na kumuachilia huru pia mahakama hiyo imetoa masharti ya kuomba mtuhumiwa huyo kuwa chini ya uangalizi wa maafisa tabibu wa magonjwa ya akili katika hospitali iliyopo Gereza la ISANGA mjini Dodoma.

Akifafanua hukumu hiyo msajili wa mahakama Kuu mwenye mamlaka ya kijaji Wilifred Peter Ndyansobera alisema kuwa, maamuzi hayo yaliyofanyika na mahakama hiyo imebaini na kuzingatia taarifa iliyotolewa na Daktari wa hospitali ya Milembe, alikopelekwa kwa ajili ya uchunguzi kubaini kuwa pamoja na  mtuhumiwa huyo kutenda kosa hilo la mauaji hayo lakini mtuhumiwa huyo hakuwa amedhamiria kufanya kosa hilo.



Alisema kutokana na hali hiyo pia pamoja na kuzingatia usalama wa mtuhumiwa na jamii kijijini kwake, mahakama hiyo imechukua maamuzi hayo
kwa usalama wake, ambapo baada ya kupata nafuu na kupona madakatari hao watatoa taarifa kwa waziri wa sheria kwa maamuzi zaidi.

Alisema katika hukumu hiyo mahakama hiyo  imezingatia Kifungu cha sheria namba 219(3)A kanuni ya adhabu sura namba 20 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

Akitoa hoja kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo, Mwanasheria wa serikali Hamimu Nkoleye pamoja na kukubaliana na taarifa ya Mei 28 /2012  iliyotolewa na madaktari wa hospitali hiyo inayoshughulikia magonmjwa ya akili huko Isanga, alisema kuwa upande wa Jamhuri hauna pingamizi juu ya taarifa hiyo.

Upande wa majibu uliowasilishwa na wakili wa kujitegemea Sebastian Waryuba uliimbia mahakama hiyo kuwa kutokana na upande wa Jamhuri kutokuwa na pingamizi juu ya taarifa hiyo, ambayo ni majibu ya ombi la mahakama hiyo kutaka mtuhumiwa huyo achunguzwe kupitia oda iliyotolewa Aprili 6/2012 aliiomba mahakama hiyo imuone hana hatia na kumfanya anufaike kupitia kifungu cha sheria ya ushahidi namba 220 vifungu vidogo namba (2 na 3).

Awali akimsomea shitaka hilo ambalo mtuhumiwa huyo alikiri kulifanya kwa maelekezo kuwa hakuwa anajitambua, mwanasheria wa serikali  Hamimu Nkoleye, alidai mbele ya Jaji huyo kuwa, Kapinga akiwa amekusudia alimuua kwa kumpiga kwa kutumia Gongo, alimpiga kichwani marehemu Jafeth Njovu aliyekuwa mwanafunzi wa darasa la tatu shule ya msingi Mtwarapachani wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma.

Nkoleye aliendela kufafanua kuwa mtuhumiwa huyo ambaye alikuwa mkazi wa kijiji cha Kumbala wilayani humo alifanya kosa hilo wakati marehemu akiwa kijijini hapo, ambapo alienda kumtembelea mama yake mkubwa aliyefahamika kwa jina la Christina Nekata na kwamba tukio hilo lililotokea Aprili 27/2010 majira ya saa kumi jioni.  

No comments: