Wanafunzi wa shule ya msingi Twiga Mbinga, wakipata kifungua kinywa. |
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
WATOTO hawa(Pichani) ni wanafunzi wa shule ya msingi Twiga iliyopo mtaa wa Mapera, kata ya Mbinga mjini mkoani Ruvuma, kama walivyokutwa na kamera yetu.
Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa habari hizi umebaini kuwa shule hiyo inafundisha watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu. Lakini shule haijasajiliwa rasmi na kupewa kibali na serikali kuendesha masomo ya shule ya msingi.
Pamoja na serikali kupitia wizara yake husika kukemea shule kama hizi ziache kutoa huduma mpaka zipewe usajili, hali hiyo imekuwa kinyume katika shule hiyo na hii inaonesha ni ukiukwaji wa taratibu na sheria zilizowekwa.
Hivyo tunashauri viongozi husika wa wilaya ya Mbinga, kuchukua hatua za haraka kunusuru hali hiyo kabla viongozi wengine kutoka ngazi ya taifa wizara ya elimu na mafunzo ya ufundi, kuchukua hatua juu ya tatizo hili.
Ofisi ya Mkurugenzi mtendaji na Mkuu wa wilaya ya Mbinga tunahitaji suala hili lifanyiwe kazi ili kusaidia watoto hawa waweze kupata elimu bora na sio kama ilivyo sasa, ukizingatia kwamba shule hiyo hata haina vifaa vya kutosha katika kukidhi mahitaji muhimu ya mwanafunzi anapokuwa darasani.
Cha kushangaza shule hii ina miaka mitano sasa, ikiendelea kutoa huduma hiyo bila kusajiliwa, Je viongozi tupo makini hapo katika kutekeleza majukumu yetu?
No comments:
Post a Comment