Thursday, December 20, 2012

KATIBU WA JUMUIYA YA WAZAZI RUVUMA NUSURA AZICHAPE NA KATIBU WAKE WA WILAYA


Na Steven Augustino,
Songea.

KATIBU wa Jumuiya ya wazazi mkoa wa Ruvuma na wa wilaya ya Tunduru mkoani humo, wamenusurika kuchapana makonde, kwa kile kinachodaiwa kutokana na katibu wa jumuiya hiyo kutoka Tunduru, kumpelekea barua ya uhamisho katibu wa jumuiya hiyo mkoani humo.

Katibu wa jumuiya hiyo mkoani humo Lotali Mbawala na katibu huyo wa Tunduru Deogratias Lweyemamu ndio waliotaka kuzua kizaa zaa hicho, baada ya Lweyemamu kudaiwa kumpelekea barua ya uhamisho  Mbawala, kwenda makao makuu ya jumuia ya wazazi taifa.

Kizaa zaa hicho pia kilichoonesha kuwashitua wajumbe wa kamati ya utendaji  ya mkoa, ilifikia hatua kumtaka Mbawala atii taratibu zilizoamriwa na ngazi husika na kumtaka akabidhi ofisi hiyo kwa Lweyemamu ambaye alionesha barua ya uteuzi wake kuwa Kaimu katibu wa jumuiya ya wazazi wa mkoa wa Ruvuma.



Malumbano hayo yalitokea hivi karibuni ndani ya ofisi za jumuiya ya wazazi mjini Songea ambapo katibu wa jumuiya ya wazazi wa wilaya ya Tunduru alifika katika ofisi ya wazazi mkoa, kwa lengo la kukabidhi barua hizo na kumjulisha kwamba ameteuliwa kuwa kaimu katibu wa jumuiya hiyo ngazi ya mkoa na kumtaka amkabidhi ofisi kwa kuzingatia na kuheshimu maamuzi yaliyotolewa na uongozi wa ngazi ya juu taifa.

Wakiwa katika ofisi hizo pia Mbawala  alishitushwa kuona anapewa barua hiyo ya uhamisho kutoka Ruvuma kwenda makao makuu ya jumuiya hiyo ya Dares salaam, jambo ambalo lilileta mzozo katika ofisi hiyo na kumtaka Lweyemamu aeleze ni nani aliyemkabidhi barua hiyo wakati anafahamu kuwa katibu wa jumuiya hiyo ngazi ya wilaya hana haki ya kukabidhiwa barua ya kumhamisha bosi wake.

Kufuatia hali hiyo Malumbano hayo yaliamuliwa na Mwenyekiti wa jumuiya ya wazazi wa mkoa wa Ruvuma Merius Ponela ambaye alilazimika kuitisha kikao cha dharula  cha kamati ya utekelezaji mkoa, ambacho kiliangalia na kujadili kwa kina juu ya tatizo hilo ambalo limeonekana kuwa na harufu mbaya na kuleta mtafaruku usio wa lazima.

Akizungumzia hali hiyo katibu wa jumuiya hiyo mkoa wa Ruvuma Lotali Mbawala alisema kuwa Agosti 20 mwaka huu, alihamishiwa katika mkoa huo kutoka mkoa wa Lindi hivyo anashangaa kuona tena anakabidhiwa barua ya uhamisho inayomtaka atoke katika mkoa huo na kwenda Dar es Salaam huku akisema huu ni utata.

Mbawala aliendelea kubainisha kuwa katika hali isiyo ya kwaida mwaka 2010 akiwa mkoani Lindi alihamishiwa Ruvuma kushika nafsi hiyo, lakini baada ya siku tatu alirudishwa tena Lindi akiwa katibu wa jumuiya ya wazazi na baada ya wiki moja tena alikabidhiwa barua ya kuhamishiwa kutoka mkoa wa Lindi kwenda Rukwa ambako baada ya kwenda kuripoti alipokea barua nyingine  ya kusitishwa kwa uhamisho wake na kumtaka arudi tena Lindi jambo ambalo amedai kuwa linamletea hofu juu ya hatma ya ajira yake.

Alifafanua kwamba ni zimepita siku chache, alikuwa amemwomba Mwenyekiti huyo wa jumuiya ya wazazi mkoa wa Ruvuma Merius Ponela kwenda mkoani Lindi kuhamisha familia yake pamoja na kuchukua mizigo kuileta Songea, lakini sasa anatakiwa  kwenda kuripoti makao makuu ya jumuiya Dar es salaam hali ambayo alidai kuwa inamchanganya na kushindwa kutoa maamuzi ya nini afanye.

Mwandishi wa habari hizi alipozungumza na Katibu wa jumuiya ya wazazi wilaya ya Tunduru Deogratias Lweyemamu alisema, uteuzi wake ni wa halali na kwamba barua ya uteuzi huo pamoja na barua ya uhamisho wa katibu wake, amekabidhiwa toka makao makuu ya jumuiya hiyo na kwamba mambo anayomtuhumu hayana msingi wowote.

No comments: