Baadhi ya Wanahisa wa Benki ya wananchi Mbinga (MCB) wakiwa katika picha ya pamoja leo, mara baada ya kufanya mkutano wao maalum wa kujadili namna ya kukuza mtaji wao wa benki, uliofanyika kwenye ukumbi wa Mbiku hoteli Mbinga mjini. (Picha na Kassian Nyandindi)
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
MWENYEKITI wa bodi ya Benki ya Wananchi Mbinga mkoani
Ruvuma(MCB) Altemius Millinga, amewataka wateja wa benki hiyo, kuendelea kununua
hisa kwa wingi ili kukuza mtaji wa ndani wa benki.
Hivi sasa benki hiyo tokea ianzishwe mwaka 2003 imeweza kujiendesha na kufikia kuwa na mtaji wa shilingi milioni 347,238.
Rai hiyo ilitolewa leo na Mwenyekiti huyo katika mkutano maalum wa wanahisa wa
MCB, ulioketi kwenye ukumbi wa Mbiku hoteli uliopo mjini hapa.
“Ndugu zangu hisa zilizonunuliwa hadi sasa ni 32,555 tu, hizi
ni kidogo tunaomba tuongeze juhudi ya kuendelea kuzinunua kwa wingi, ili tufikie malengo
yetu tuliyojiwekea na benki iweze kusonga mbele”, alisisitiza.
Millinga alisema mafanikio ya kimaendeleo ya benki ya wananchi
Mbinga hayawezi kusonga mbele, kama Wanahisa hawatakuwa tayari kununua hisa kwa
wingi ambazo zitaifanya benki iweze kukuza mtaji wake wa ndani.
Alisema dira ya benki hiyo, ni kuwa asasi kiongozi ya fedha,
itakayotoa huduma bora za kifedha kwa wananchi wa mkoa wa Ruvuma.
Kutokana na huduma kuendelea kuboreshwa, alisema MCB hivi
sasa imekwisha jenga mfumo wa mashine ya kutolea fedha ATM kwa wateja wake, na
hivi sasa wateja wamekuwa wakipata huduma za kifedha kupitia mashine hiyo.
Aliongeza kuwa hadi sasa benki imeweza kufikia vijiji
206 mkoani Ruvuma, ambapo vikundi vimeanzishwa katika vijiji hivyo na wananchi
waliojiunga navyo hupata huduma za kifedha kwa urahisi.
Aidha benki ya wananchi Mbinga imeweza kutoa mikopo katika
nyanja mbalimbali kama vile mikopo kwa wenye ajira, vikundi, uzalishaji mali,
wafanyabiashara, elimu na pembejeo za kilimo.
No comments:
Post a Comment