|
Kushoto
ni Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Jaji Joseph Warioba
akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo (Jumatatu,
Aprili 29, 2013). Kulia ni Katibu wa Tume, Assaa Rashid. (Picha na Tume
ya Katiba) |
Dar es Salaam,
Tanzania.
Tume ya Mabadiliko ya
Katiba LEO imesema imejipanga kuandaa rasimu ya katiba itakayoweka mbele
maslahi ya taifa na kuwaomba wananchi waijadili na kutoa maoni yao
katika mabaraza ya katiba yatakayokutana kuanzia mwezi Juni mwaka huu
(2013).
Mwenyekiti wa Tume hiyo Jaji Jospeh Warioba amesema
lLEO (Jumatatu, Aprili 29, 2013) jijini Dar es Salaam kuwa katika
kuandaa rasimu hiyo, Tume yake haitapokea shinikizo kutoka taasisi,
asasi, makundi au vyama vya siasa.
“Tume haitengenezi katiba
ya vikundi au vyama, tunaandaa katiba ya nchi,” amesema Jaji Warioba
katika mkutano wake na waandishi wa habari katika ofisi za Tume na
kufafanua kuwa Tume inazingatia uzito wa hoja zilizotolewa na wananchi
na sio idadi ya watu waliotoa maoni.
Jaji Warioba amewataka
wananchi kutokubali kutumiwa na makundi, asasi, taasisi na vyama wakati
wa kujadili na kutoa maoni katika mabaraza ya katiba ya wilaya.
Mabaraza ya Wananchi wenye ulemavu:Akizungumza
kuhusu ushiriki wa walemavu katika mabaraza ya katiba, Jaji Warioba
amesema Tume yake inatarajia kuunda mabaraza ya Katiba ya watu wenye
ulemavu ili kuwapa fursa walemavu kutoka Tanzania Bara na Zanzibar kutoa
maoni yao kuhusu rasimu ya Katiba itakayotolewa na Tume.
Hatua
hii inafuatia ombi la Shirikisho la Vyama vya Watu wenye ulemavu
Tanzania (SHIVYAWATA) na Umoja wa Watu wenye ulemavu Zanzibar (UWAZA)
waliloliwasilisha kwa Tume.
Jaji Warioba amesema Baraza moja
litaundwa Tanzania Bara na jingine Zanzibar na kwamba yatashirikisha
wananchi kutoka ngazi ya chini ya wilaya hadi Taifa.
“Tunaelewa
kuwa watu wenye ulemavu ni karibu asilimia 10 ya watanzania wote na
mchakato huu hauwezi kuwatenga katika ngazi yoyote,” amesema Jaji
Warioba na kuongeza kuwa taarifa ambazo Tume yake inazo zinaonyesha
baadhi ya watu wenye ulemavu wamependekezwa na mitaa, vijiji, vitongoji
na shehia kuwa Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya.
Chaguzi za Wajumbe Mabaraza ya Katiba ya Wilaya:
Aidha, Jaji Warioba amezungumzia mafanikio na changamoto
zilizojitokeza katika chaguzi zilizofanyika nchini kote hivi karibuni za
kuchagua Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba kuanzia ngazi ya mitaa, vijiji,
vitongoji na shehia.
Kwa mujibu wa Jaji Warioba, tathmini ya
Tume inaonyesha kuwa kwa kiwango kikubwa viongozi na watendaji katika
ngazi za vijiji, mitaa, shehia na kata walizingatia mwongozo uliotolewa
na Tume na kuwa maeneo mengi wananchi walichaguana kwa amani na utulivu.
“Kwa
mfano jumla ya shehia 323 sawa na asilimia 96.4 kati ya shehia 335 kwa
upande wa Zanzibar zimekamilisha vizuri mchakato huu, hali kadhalika
jumla ya Kata 3,331 sawa na asilimia 99.8 kati ya Kata 3,339 kwa
Tanzania Bara nazo zimekamilisha mchakato wa kuwapata wajumbe wa
Mabaraza ya Katiba ya Wilaya kwa kuzingatia utaratibu uliotolewa kwa
mujibu wa Mwongozo,” amesema Jaji Warioba.
Kuhusu hatua
inayofuata baada ya chaguzi hizo, Jaji Warioba alisema Tume inaendela
kupokea majina kutoka kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa na ya wananchi
wote waliopendekezwa kutoka katika Kata na Shehia na kazi hiyo
inatarajia kukamilika ifikapo tarehe 30 Aprili mwaka huu (2013).
Changamoto:
Akizungumzia
kuhusu changamoto zilizojitokeza katika chaguzi hizo, Jaji Warioba
amesema kuwa pamoja na mafanikio yaliyopatikana pia kulijitokeza
changamoto kadhaa ambazo zilisabishwa na misimamo ya kisiasa na kidini
“Katika
baadhi ya maeneo mikutano ya uchaguzi ngazi za vijiji, mitaa na shehia
ilishindwa kufanyika kutokana na mivutano ya kisiasa na kidini
zilizosababishwa na baadhi ya wananchi kufangamanisha chaguzi za Wajumbe
wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya na masuala ya kisiasa na kidini,”
amesema Jaji Warioba.
Jaji Warioba ametaja changamoto nyingine
kuwa ni pamoja na baadhi ya wananchi kujiingiza katika vitendo vya
rushwa katika chaguzi hizo ili wapendekezwe kuwa wajumbe wa mabaraza
hayo ya katiba.
“Tumepokea pia malalamiko ya vitendo vya
rushwa,” alisema Mwenyekiti huyo na kusema vitendo hivyo ni kinyume cha
sheria na kuongeza kuwa taasisi zenye mamlaka ya kupambana na vitendo
hivyo zinapaswa kushughulikia malalamiko hayo.
Aina na Majukumu ya Mabaraza ya Katiba:
Katika
mkutano huo uliofanyika katika katika Ofisi za Tume zilizopo mtaa wa
Ohio jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti huyo pia alizungumza kuhusu aina
na majukumu ya Mabaraza ya Katiba.
Kwa mujibu wa Jaji Warioba,
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83 imetoa fursa ya kuundwa kwa
mabaraza ya aina mbili ambayo ni Mabaraza yatakayoundwa, kusimamiwa na
kuendeshwa na Tume katika muda na tarehe itakayopangwa na Tume.
Aina
ya pili, kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo, ni Mabaraza ya Katiba ya Asasi,
Taasisi na Makundi mbalimbali yenye malengo yanayofanana. Mabaraza haya
yatajiunda, yatajisimamia na kujiendesha yenyewe na kisha kuwasilisha
maoni yao kuhusu rasimu ya Katiba ndani ya muda utakaopangwa na Tume.
“Kazi
kubwa ya Mabaraza ya Katiba ya aina zote mbili ni kuipitia, kuijadili
na kuitolea maoni rasimu ya Katiba itakayokuwa imeandaliwa na Tume
kutokana na maoni yaliyokusanywa kutoka kwa wananchi,” alisema Jaji
Warioba na kuziomba taasisi, makundi, asasi na vyama mbalimbali kutumia
fursa hiyo ya kisheria kuunda mabaraza na kutoa maoni yao kuhusu rasimu
ya Katiba itakayotolewa.