Friday, August 30, 2013

BAADHI YA WATUMISHI WA IDARA YA KILIMO MBINGA WADAIWA KUHUSIKA NA UTOROSHAJI WA KAHAWA

Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Said Thabit Mwambungu.

 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
 
MTANDAO wa kuhujumu mapato ya Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, kupitia utoroshaji wa zao la kahawa umezidi kubainika kufuatia kuwepo kwa baadhi ya watumishi wa wilaya hiyo kuhusika na biashara ya zao hilo.

Utoroshaji huo wa kahawa kavu umekuwa ukifanyika kwa kasi kubwa tangu kuanza kwa msimu wa mavuno Julai mwaka huu, ambapo baadhi ya wafanyabiashara kwa kushirikiana na watumishi kutoka idara ya kilimo wamekuwa wakisafirisha kahawa hiyo kwenda wilayani Mbozi mkoa wa Mbeya kwa lengo la kukwepa ushuru.

Kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa na mtandao huu umebaini kuwa watumishi hao (majina tunayo) ambao wapo watatu mpaka sasa ndio wamekuwa vinara wa kuhujumu uchumi wa Mbinga kupitia biashara ya zao hilo na kwamba tayari uongozi wa ngazi ya juu wa wilaya hiyo umeunda timu ya kufanya uchunguzi juu ya suala hilo.

Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga Allanus Ngahi amekiri kuwepo kwa baadhi ya watumishi wa iadara hiyo kuhusika na utoroshaji wa kahawa, ambapo alisema watumishi hao wanafahamika hivyo hapo baadaye taarifa rasmi itatolewa na hatua zitachukuliwa dhidi yao.

Tuesday, August 27, 2013

MSHAURI WA ZAO LA KAHAWA MBINGA ADAIWA KUHUSIKA NA UTOROSHAJI WA ZAO LA KAHAWA KWA LENGO LA KUKWEPA KULIPA USHURU

Mkuu wa Wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma,  Senyi Ngaga.














Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

KIGOGO mmoja wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, anadaiwa kuhusika katika vitendo vinavyofanywa na baadhi ya wafanyabiashara wa zao la kahawa wilayani humo, la utoroshaji wa  zao hilo kwa lengo la kukwepa kulipa ushuru jambo ambalo linasababisha halmashauri hiyo kukosa mapato.

Wakizungumza na waandishi wa habari kwa nyakati tofauti mjini hapa, wafanyabiashara hao walitoboa siri hiyo kwa kumtaja jina kuwa ni, Mshauri wa zao la kahawa wilayani humo Gotham Haulle ambaye ni mmoja kati ya maofisa kilimo amekuwa akijihusisha na biashara ya ununuzi wa kahawa vijijini kwa kuwatumia wafanyabiashara wajanja ambao huwarubuni wakulima kwa kununua zao hilo kwa bei ya chini.

Aidha walisema tukio la kukamatwa kwa mfanyabiashara Madawa Mwaijande la utoroshaji wa kahawa kavu tani 10 yenye thamani ya shilingi milioni 28 Agosti 21 mwaka huu majira ya usiku katika kijiji cha Kitai, Haulle anahusishwa katika tukio hilo kwa kile kinachodaiwa kuwa ofisa kilimo huyo amekuwa akishirikiana kufanya biashara hiyo na mfanyabiashara huyo.

Mfanyabiashara huyo alikamatwa akitorosha kahawa hiyo kuelekea Jijini Mbeya kwa lengo la kukwepa kulipa ushuru akiwa na gari lenye namba za usajili T 856 CFL mali ya Medson Ulendo mkazi wa mjini hapa.

Vilevile baadhi vigogo wa halmashauri hiyo ambao majina yao hawakutaka yatajwe katika mtandao huu, wamemnyoshea kidole mtumishi mwenzao wakisema, muda mwingi amekuwa hakai ofisini kutokana na kukabiliwa na shughuli ya biashara hiyo ya kahawa badala ya kutekeleza majukumu yake ya msingi aliyopewa na serikali.

“Hii kahawa tuliyoikamata juzi tumefanya utafiti na kubaini kwamba huyu mfanyakazi mwenzetu anahusika kwa kiasi kikubwa na biashara hii, lakini tupo katika hatua ya kuchukua maamuzi sahihi ambayo yatasaidia kudhibiti vitendo hivi viovu vinavyolenga kuikosesha halmashauri mapato yake”, alisema mmoja kati ya vigogo wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga.

Pamoja na mambo mengine Waandishi wa habari walipofanya mahojiano na Mshauri huyo wa zao la kahawa wilaya ya Mbinga Gotham Haulle juu ya kuhusishwa na tuhuma za kushirikiana na wafanyabiashara kutorosha kahawa kwa lengo la kukwepa kulipa ushuru huo, alikana huku akisema yeye anazobiashara zake zingine ambazo huzifanya na kumuingizia kipato.

“Mimi kwa kifupi nina hela nyingi sana, haya maneno yanayozungumzwa ni kutaka kumchafua mtu tu, na hii ni kawaida kwa vijana wahuni  wakitaka kumharibia mtu lazima wamhusishe na matukio maovu”, alisema Haulle.

Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo Hussein Issa Ngaga alipoulizwa na waandishi wa habari alithibisha kuwepo kwa tukio hilo na kusema, anazotaarifa kuwa baadhi ya watumishi wake wamekuwa wakijihusha na biashara ya ununuzi wa kahawa huku wakishirikiana na wafanyabiashara wengine wilayani humo kuhujumu mapato ya halmashauri hiyo.

Ngaga alisema katika kukabiliana na hali hiyo tayari kuna kamati husika imeundwa ambayo hufanya kazi ya kufuatilia vitendo hivyo viovu na wale watakaobainika, watachukuliwa hatua stahiki za kisheria na kwamba alikemea kitendo cha watendaji kuacha shughuli za kiutumishi na kupoteza muda mwingi kufanya shughuli zao binafsi, huku kazi za utumishi wa umma walizoajiriwa nazo zikiendelea kuzorota.


Saturday, August 24, 2013

MFANYABIASHARA MAARUFU WA JIJINI MBEYA AKAMATWA MBINGA AKITOROSHA KAHAWA KINYEMELA KWA LENGO LA KUKWEPA KULIPA USHURU

Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga Allanus Ngahi (Kushoto), aliyevaa kofia akiangalia gari ambalo lilikamatwa na shehena ya magunia ya kahawa ambalo mfanyabiashara maarufu Madawa Mwaijande wa Mwanjelwa mkoani Mbeya, alikuwa akilitorosha kuelekea Mbeya kwa lengo la kukwepa kulipa ushuru.


Gari lenye namba za usajili T. 856 CFL mali ya Medson Ulendo mkazi wa Mbinga mjini, lipo chini ya ulinzi katika kituo kikuu cha polisi wilaya Mbinga, ambalo lilikuwa likitumika kutorosha kahawa tani 10,000 kutoka kijiji cha Langiro wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma. Gari hilo lilikamatwa katika kijiji cha Kitai kwenye geti la kukagua mazao ya maliasili wilayani humo.(Picha zote na Kassian Nyandindi) 


Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

HALMASHAURI ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, imemkamata mfanyabiashara mmoja maarufu, ambaye alikuwa akitorosha kahawa tani 10 yenye thamani ya shilingi milioni 28 kutoka wilayani humo kuelekea mkoani Mbeya, kwa lengo la kukwepa kulipa ushuru wa halmashauri hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya hiyo Allanus Ngahi alisema kahawa hiyo ilikamatwa Agosti 21 mwaka huu kijiji cha Kitai wilayani humo, majira ya saa tano usiku katika geti la kukagua mazao ya maliasili ikiwa inasafirishwa kwenye gari aina ya Scania lenye namba za usajili T. 856 CFL mali ya Medson Ulendo mkazi wa mjini hapa.

Ngahi alisema kahawa hiyo iliyokamatwa ni mali ya mfanyabiashara  Madawa Mwaijande ambaye ni wa Mwanjelwa mkoani Mbeya, ambapo wakati anakamatwa alikuwa na dereva aliyekuwa akiendesha gari hilo aliyemtaja kwa jina la Julius Kinunda.

Tuesday, August 20, 2013

WALIOFARIKI DUNIA KATIKA AJALI YA GARI WATAMBULIWA MAJINA YAO

Na Kassian Nyandindi,
Nyasa.



WATU wawili wamefariki dunia na wengine 40 wamejeruhiwa vibaya, kufuatia ajali ya gari iliyotokea majira ya usiku katika milima ya Burma wilayani Nyasa mkoa wa Ruvuma.

Tukio hilo limetokea Agosti 19 mwaka huu majira ya saa 3 usiku na kwamba, waliofariki dunia wametambuliwa kwa majina ya Lumanyama Sanga na Issa Adamu wakazi wa Songea mjini, huku baadhi ya majeruhi wakiwa wamelazwa katika hospitali ya wilaya ya Mbinga.

Aidha majeruhi wengine ambao hali zao ni mbaya, wamesafirishwa kwenda hospitali ya mkoa Songea na Peramiho zilizopo mkoani humo.

BREAKING NEWS: WATU WAWILI WAFARIKI DUNIA NA WENGINE 40 WAJERUHIWA VIBAYA KUTOKANA NA AJALI YA GARI


Baadhi ya majeruhi wa ajali hiyo Rahabu Nziku kushoto, na mwenzake Joseph Kapinga wakiwa wamelazwa katika hospitali ya wilaya ya Mbinga wakiendelea kupatiwa matibabu. (Picha na Kassian Nyandindi)

Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.


WATU wawili wamefariki dunia na wengine 40 wamejeruhiwa vibaya, kufuatia ajali iliyotokea usiku wa kuamikia leo katika milima ya Burma wilayani Nyasa mkoa wa Ruvuma.

Tukio hilo limetokea Agosti 19 mwaka huu majira ya saa 3 usiku na kwamba, baadhi ya majeruhi wamelazwa katika hospitali ya wilaya ya Mbinga.

Aidha majeruhi wengine ambao hali zao ni mbaya, taratibu za kuwasafirisha kuwapeleka hospitali ya Peramiho iliyopo Songea mkoani humo zinafanywa.

Pamoja na mambo mengine taratibu za kutambua miili ya marehemu hao zinafanywa, hivyo ndugu wasomaji wa mtandao huu tutaendelea kuwajuza hapo baadaye.

Gari lililopata ajali ni aina ya fuso lenye namba za usajili T. 807 AVH ambalo lilikuwa likiendeshwa na Lehani Mohamed Makunganya.

Kwa mujibu wa vyanzo vya uhakika vya habari, vimedai kuwa ajali hiyo ilitokana na gari hilo, kuwa katika mwendo kasi na kupakia mizigo mingi ya nguo ambazo zilikuwa zikipelekwa Mbamba bay wilayani Nyasa, kwa ajili ya kwenda kufanya biashara ya kupiga mnada.


Friday, August 16, 2013

WAANDISHI WA HABARI MKOANI RUVUMA WAPIGWA MSASA JUU YA MATUMIZI BORA YA INTANETI


Baadhi ya Waandishi wa habari wa mkoa wa Ruvuma, wakiwa katika picha ya pamoja na wawezeshaji waliokaa wawili kutoka kushoto, ni Sengiyuva Gasirigwa na Simon Berege wakati walipokuwa kwenye mafunzo ya Intaneti yaliyofanyika kwenye ukumbi wa VETA mjini Songea. Upande wa kulia aliyekaa ni Ngaiwona Nkondora mwandishi wa habari wa Radio Free Africa.  (Picha zote na Kassian Nyandindi)

Na Steven Augustino,
Songea.

WAANDISHI wa habari mkoani Ruvuma, wameonywa kuamini habari kutoka mitandaoni na kuzitumia kuhabarisha umma bila  kuzifanyia utafiti wa kutosha katika intaneti, na kutumia vyanzo vya kuaminika ikiwemo kuwahoji wahusika kupata habari za ukweli ambazo zitakuwa na manufaa kwa wasomaji.

Onyo hilo limetolewa na Simon Berege wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo wa namna ya kuandika habari kwa kutumia mitandao ya Intaneti na kutuma picha za kihabari  mtandaoni yanayoendeshwa katika Ukumbi wa Veta, Manispaa ya Songea mjini hapa, na Taasisi ya Vyombo vya habari kusini mwa Africa (Media Institute Of Southern Africa) MISA TANZANIA.

Wanahabari hao wamehitimu leo mafunzo hayo ambapo wamefundishwa namna ya kufanya utafiti wa vyanzo vya habari mbalimbali katika Intaneti, na kufungua njia nyingine za mawasiliano kama  ‘youtube’, Blogu na namna ya kuzitumia katika tasnia ya habari na kuzitengeneza zikiwa na takwimu sahihi.

Thursday, August 15, 2013

KASHFA DAWA ZA KULEVYA JNIA, MWAKYEMBE ASEMA ANAJITOA MUHANGA KUWATAJA WANAOHUSIKA HAPA NCHINI

Dokta Harrison Mwakyembe.

 
















WAZIRI wa Uchukuzi, Dkt. Harrison Mwakyembe amesema anajitoa mhanga kuhakikisha Wizara yake inawatia mbaroni watu wanaojihusisha na usafirishaji wa dawa za kulevya kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIA). 

“Nitajitoa mhanga juu ya biashara hiyo na siogopi vitisho vya watu, maana mimi nilishakufa siku nyingi, hatuwezi kuidhalilisha nchi yetu kiasi hicho,” alisema. 

Alisema hayo juzi, wakati akieleza mkakati wa Wizara yake kudhibiti wanaosafirisha dawa hizo kupitia uwanja huo uliopewa heshima ya kuitwa jina la Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere wakati wa maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani yaliyofanyika jijini hapa juzi. 

“Dawa za kulevya sasa zinasafirishwa kupitia kiwanja cha ndege, ambacho kimepewa jina la mtu muhimu katika nchi yetu, Mwalimu Nyerere, ni aibu kwa nchi yetu na Taifa letu, kuona uwanja huo unatumika kwa biashara hiyo, nipeni muda, mimi ndiye Waziri wa Uchukuzi, hatutakubali hali hii,” alisema na kuongeza: “Pale uwanjani kuna ofisi nne, Polisi, Uhamiaji, Usalama wa Taifa na watu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege, wote nimewaagiza wanipe taarifa, walikuwa wanafanya nini hadi dawa hizo zinapita uwanjani hapo?” 

Alisema anawapa notisi watu wote wanaosafirisha dawa za kulevya kupitia uwanjani hapo, watambue kuwa alishajitoa mhanga kupambana na dawa za kulevya, maana ni biashara inayodhalilisha Taifa. 

Mwakyembe alipata kuugua kiasi cha kukatisha tamaa ambapo ilikuja kubainika kuwa aliwekewa sumu iliyosababisha mwili wake kuharibika na nywele kunyonyoka huku kucha zikibadilika rangi, lakini alipona alipopelekwa kwa matibabu zaidi India. 

Alivitaka viwanja vyote vya ndege nchini, kuhakikisha vinaweka mikakati ya kisayansi kubaini watu wanaosafirisha dawa hizo kupitia kwenye mipaka yao. 

“Na kwa hili, niviagize viwanja vyote vya ndege nchini vihakikishe kuwa vinadhibiti wasafirishaji wa dawa za kulevya kwa kushirikiana na vyombo vingine vya Dola vilivyo katika viwanja hivyo,” aliongeza. 

Alitaka viongozi wa dini washiriki kujenga amani nchini huku akionya vijana dhidi ya kushabikia vitendo vinavyoweza kuipeleka nchi katika migogoro ya kivita na wajifunze mifano kwa baadhi ya nchi zilizoingia kwenye vita. 

Alisema uzoefu unaonesha, kuwa nchi zilizoingia katika migogoro ya kivita imekuwa vigumu kurudia hali ya kawaida na zimeendeleza vita vya wenyewe kwa wenyewe. 

“Afrika Kusini, Congo DRC ni nchi ambazo zimejaaliwa kuwa na rasilimali nyingi za madini, lakini kutokana na kukosa amani kwa muda mrefu, imekuwa vigumu rasilimali kufikia wananchi wote,” alisema. 

Alitaka vijana kubadili tabia na mtazamo kwa kuwa ndiyo njia pekee ya kujikomboa kiuchumi na kifikra na kuacha kutumiwa na wanasiasa. 

Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba, Deus Kibamba ambaye alikuwa Mwezeshaji Mkuu katika tamasha hilo, alitaka viongozi wa madhehebu ya dini nchini waendelee kujenga amani iliyopo kwa ajili ya vizazi vya sasa na vijavyo. 

“Mimi huwa naamini kuwa amani hujengwa, haiombewi, hivyo naomba viongozi wa dini mshiriki kuijenga amani nchini, kwa manufaa yetu sote,” alisema na kutaka vijana waache kulalamika bila kufanya kazi. 

Mkurugenzi wa Shirika lisilo la Serikali la Jitambue Foundation, Isaac Mwanahapa, alisema kuwa Jitambue iliandaa tamasha hilo la vijana kwa lengo la kuwaleta pamoja ili kujadili mambo ya msingi ya Taifa. 

Alisema kwa maadhimisho hayo, shirika lake liliadhimisha siku hiyo kwa kuchagua kaulimbiu ya “Tetea Amani, Okoa Kizazi Kijacho”, kutokana na nchi kugubikwa na matukio ya uvunjifu wa amani, yakiwamo ya watu kupigwa mabomu na kumwagiwa tindikali, kwenye maeneo ya ibada na hata kwenye mikutano ya kisiasa. (Kwa hisani ya Jukwaa huru)

AMUANGUSHIA KIPIGO MKE WAKE HADI KUFA KUTOKANA NA WIVU WA KIMAPENZI



Na Steven Augustino,
Namtumbo.

MFUGAJI mmoja wa Kisukuma anayeishi katika kijiji cha Mtelamwahi wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma, Maiko Sajini (24) anashikiliwa na Polisi kwa tuhuma ya kumshushia kipigo mke wake hadi kufa.

Chanzo cha tukio hilo inadaiwa kuwa ilitokana na wivu wa kimapenzi.

Kwa mujibu wa shuhuda wa tukio hilo Anna Yohana ambaye ni mjomba wa marehemu alisema kuwa marehemu Dagwanedi Jogi (22) alikumbwa na mkasa huo, baada ya mumewe huyo kumtuhumu kuwa amekuwa na uhusiano wa kimapenzi na mtu mmoja anayeishi kijijini hapo ambaye hakumtaja jina lake, hali ambayo ilizusha mtafaruku huo katika ya wanandoa hao.

Alisema siku ya tukio mumewe huyo alisafiri kwenda kijiji jirani na kawaida yake huwa anarudi usiku wa manane lakini anaporudi   humkuta mkewe  akiwa amelala, lakini cha kushangaza wakati akikaribia nyumbani hapo alikutana na kijana huyo njiani ambaye kila mara alidai kuwa amekuwa akimhisi kumuingilia katika ndoa yake, na hata alipofika nyumbani kwake alimkuta mkewe akiwahaja lala hali ambayo ilimfanya  amhoji juu ya hali hiyo.

Alisema wakiwa katika mahojiano hayo ilitokea kutoelewana kwa wanandoa hao, ambapo mwanaume huyo aliomba amkague mkewe katika sehemu zake za siri ili aweze kujiridhisha juu ya mashaka yake, lakini mkewe alikataa hali ambayo ilisababisha vurugu na mtuhumiwa huyo kutumia nguvu katika ukaguzi huo ambapo baada ya kuangalia aligundua kuwa mkewe huyo alikuwa ametoka kufanya mapenzi.

Wednesday, August 14, 2013

WAANDISHI WA HABARI MKOANI RUVUMA WAPATIWA MAFUNZO JUU YA MATUMIZI BORA YA INTANETI


Mwezeshaji wa mafunzo ya Intaneti Simon Berege kutoka mkoani Iringa (aliyesimama) akitoa maelezo kwa waandishi wa habari wa mkoa wa Ruvuma juu ya matumizi ya kisasa ya tekinolojia ya habari kwa kutumia Intaneti. Waandishi wa habari wapo katika mafunzo ya siku tatu wakishiriki mafunzo hayo ambayo yanafanyika kwenye ukumbi wa VETA mjini Songea.

Waandishi wa habari mkoani Ruvuma wakiendelea na mfunzo hayo katika ukumbi wa VETA mjini Songea.

Mwezeshaji Simon Berege akisisitiza jambo juu ya matumizi ya Intaneti kwa Waandishi wa habari(hawapo pichani) wa mkoa wa Ruvuma.


Aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa habari mkoani Ruvuma, Juma Nyumayo naye akishiriki katika kazi ya kutoa maelekezo juu ya matumizi ya Intaneti.

Mwandishi wa habari Kassian Nyandindi anayeandikia magazeti ya Businesstimes LTD na Joyce Joliga wa gazeti la Mwananchi, nao wakiwa makini katika kushiriki mafunzo hayo.

Mwezeshaji Simon Berege upande wa kulia, akizungumza na Juma Nyumayo aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa habari mkoani Ruvuma.

Waandishi wa habari wa mkoa wa Ruvuma, wakiendelea na mafunzo ya Intaneti mjini Songea, lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo waandishi wa mikoani katika utendaji wa kazi zao kwa kutumia Intaneti.(Picha zote na Kassian Nyandindi)

TUJIKUMBUSHE YALIYOJIRI SIKU YA KILELE CHA SHEREHE ZA NANENANE WILAYANI MBINGA

Vallence Ndendya, mkazi wa Mbinga mjini akiangalia mbogamboga na matunda siku ya maadhimisho ya kilele cha sherehe za Nanenane wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma. Anayeshuhudia upande wa kulia ni mkulima Kandidus Komba mkazi wa kitongoji cha Masasi.

Kandida Lyambila, mtaalamu wa kutengeneza vyungu vya udongo kutoka kikundi cha Mbalawala Women Organisation kilichopo kata ya Ruanda wilayani Mbinga, akionyesha utalaamu wake siku ya maadhimisho ya sherehe hizo Mbinga mjini.

Meneja mkuu wa kikundi cha Mbalawala Women Organisation, Leah Kayombo akitoa maelezo mafupi kwa mgeni rasmi Katibu tawala wa wilaya ya Mbinga, Idd Mponda aliyevaa suti nyeusi juu ya utengenezaji wa vitu mbalimbali vya asili siku ya kilele cha sherehe za nane nane zilizoazimishwa wilayani Mbinga, mtaa wa Lusaka Mbinga mjini.

Mama Kayombo akiendelea kutoa maelezo ya utengenezaji wa vyungu, kwa wageni waliotembelea banda la kikundi cha Mbalawala Women Organisation.

Meneja mkuu wa Mbalawa Women Organisation, Leah Kayombo akitoa maelezo juu ya utengenezaji wa mkaa wa mawe kwa mgeni rasmi Katibu tawala wa wilaya ya Mbinga Idd Mponda aliyevaa suti nyeusi. Mkaa huo ukisha tengenezwa hutumika pia katika shughuli za kupikia nyumbani.

Katibu tawala wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Idd Mponda aliyeinama amevaa suti nyeusi, akiangalia majiko yaliyotengenezwa na kikundi cha Mbalawala Women Organisation.

Pia maua ya asili nayo hutengenezwa na Mbalawala Women Organisation, kushoto Mama Kayombo akitoa maelezo namna yanavyotengenezwa.

Banda la Maliasili na Mazingira nalo halikuwa mbali katika maonesho hayo.


Katibu tawala wa wilaya ya Mbinga Idd Mponda, akitia sahihi katika kitabu cha wageni, kwenye banda la maonyesho la kikundi cha Mbalawala Women Organisation, kilichopo katika kata ya Ruanda wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma.


Banda la maliasili na mazingira Mbinga, nalo likiendelea na maonyesho.

Katibu tawala wilayani Mbinga Idd Mponda (aliyevaa suti nyeusi) akipewa maelezo juu ya uzalishaji wa miche ya miti unavyofanywa. (Picha zote na Kassian Nyandindi)

Tuesday, August 13, 2013

CCM KAGERA YATIMUA MADIWANI NANE

 





KATIBU wa CCM mkoa wa Kagera Avelin Mushi amemaliza Press Conference, hivi punde na kufafanua kuwa kikao cha Halmasahuri Kuu ya mkoa huo imemaliza kikao chake hivi punde na kuamua madiwani nane wa Manispaa ya Bukoba, kufukuzwa katika chama na kufutiwa nyadhifa za udiwani kutokana na mgogoro uliokuwa ukiendelea.

Waliofukuzwa ni:
1. Richard Gaspar (Miembeni )
2. Murungi Kichwabuta (viti maalum)
3. Alexander Ngalinda ambaye pia ni Naibu Meya (Buhembe)
4. Yusuf Ngaiza ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM wa wilaya (Kashai)
5. Deusdedit Mutakyahwa (Nyanga)
6. Robert Katunzi (Hamugembe)
7. Samwel Ruhangisa (Kitendaguro) na
8. Dauda Kalumuna (Ijuganyondo)

Katibu huyo ameongeza kuwa madiwani hao wanaweza kukata rufaa kwa ngazi za juu za chama wakiona hawakutendea haki na kuwa ngazi ya mkoa ina mamlaka ya kufanya hivyo kwa madiwani wa ngazi hizo. 

Aidha amesema kwa Bw Yusuph ngaiza amabye ni mwenyekiti wa CCM bukoba, nafasi yake hiyo inasubiriwa ngazi za juu amabazo ndizo zenye mamlaka juu yake(kwa cheo hicho) (Source Jamii Forum)

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU MAJERAHA YA SHEIK PONDA ISSA PONDA

Sheikh Ponda Issa Ponda (54) alipokelewa hapa Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Upasuaji wa mishipa ya fahamu (MOI) jana tarehe 11/8/2013 saa 7.30 adhuhuri akitokea Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Baada ya kupokelewa alionekana akiwa na majeraha chini ya bega la mkono wa kulia lililokuwa limeshonwa mbele na nyuma madaktari wetu walifanya uchunguzi na kushauri afanyiwe kipimo cha x-ray ili ubaini kama kuna mvunjiko kwenye sehemu ya jeraha. 

Tathimini ya madaktari baada ya kupata majibu ya x/ray ilionyesha alikuwa na mvunjiko bila mifupa kupishana. Vivyo hivyo kidonda hakikuwa katika hali nzuri licha ya tiba ya mwanzo na iliamuliwa afanyiwe upasuaji mpya ili kuzuia maambukizi kama kingeachwa hivyo  
KWA HIYO ….
Kufuatana na tiba ya awali aliyopata ikiwa ni pamoja na kushonwa jeraha kabla ya kufikishwa MOI imekuwa vigumu kujua kama jeraha lilisababishwa na kitu gani.

Kipimo cha x-ray kilionyesha kwamba alikuwa amepata mvunjiko wa mfupa mkubwa wa bega bila mifupa kupishana.  

Hivyo basi sheikh Ponda Issa Ponda anaendelea na matibabu baada ya upasuaji.
                                            
Mkurugenzi Mtendaji,
Taasisi ya Mifupa na Upasuaji wa Mishipa ya Fahamu (MOI)

WATANZANIA WAASWA KUWAJALI WENYE MAHITAJI MAALUM

Na Anna Nkinda – Maelezo
 
Watanzania wametakiwa kujenga tabia ya kuwajali watu wenye mahitaji maalum ikiwa ni pamoja na watoto yatima na wanaoishi katika mazingira hatarishi ili nao wajione kana kwamba wana wazazi ingawa baadhi yao wamefiwa na wazazi wao.
 
Wito huo umetolewa jana na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Montage Tanzania Teddy Mapunda  wakati wa sherehe za sikuku ya Eid Mubarak zilizofanyika katika Shule ya Sekondari ya watoto wa kike  ambao ni yatima na wanaoishi  katika mazingira hatarishi ya WAMA-Nakayama iliyopo kijiji cha Nyamisati wilaya ya Rufiji mkoani Pwani.
 
Mapunda alisema ingawa watoto hao hawana wazazi lakini kama jamii itawajali na kuwaonyesha upendo hawatahisi tofauti ya kutokuwepo kwa wazazi wao kwani kutakuwa na watu wanaowajali kama vile wazazi wao wako hai.
 
Mkurugenzi huyo pia aliipongeza shule hiyo kwa kuzisaidia shule za  jirani za Sekondari za  Mahege na Nyamisati ingawa nao wanapata msaada kutoka kwa wafadhili kwa kuimarisha miundombinu ikiwa ni pamoja na kujenga majengo, kutoa vitabu, kuweka umeme wa jua na kuwapatia walimu wa mazoezi ambao wakimaliza vipindi vya kufundisha katika shule ya WAMA-Nakayama wanaenda kufundisha katika shule hizo.
 
Naye  Kaimu Mkuu wa Shule hiyo Mwalimu Suma Mensah  alisema kuwa  shule yake inawanafunzi  322 wa kidato cha kwanza hadi cha nne kutoka mikoa yote ya Tanzania ambao ni watoto yatima na wanaoishi katika mazingira hatarishi.
 
Kwa upande  wa michezo alisema kuwa wanashiriki michezo mbalimbali ikiwa ni pamoja na mpira wa miguu kwa wanawake na mpira wa mikono kwa wanawake, drama na riadha.
 
Aliongeza  kuwa eneo la viwanja wanalo kubwa na la kutosha lakini  hawana viwanja rasmi pia wanakabiliwa na upungufu wa vifaa vya michezo kama vile jezi, viatu na mipira. 
 
“Kwa mara ya kwanza shule yetu ilishiriki mashindano ya UMISETA mwaka 2012 na kufikia ngazi ya mkoa hali ambayo imetutia  moyo na tunaamini kuwa ipo siku wanafunzi wetu watafika ngazi ya Taifa”, alisema Mwalimu Mensah .
 
Wafanyakazi wa kampuni ya Montage Tanzania waliamua kusherehekea sikukuu ya Eid Mubarak na wanafunzi hao ili kuonyesha kuwa wanawajali na kuwathamini. Pia waliwapatia zawadi za  jezi nne za michezo mbili za mpira wa miguu na mbili za mpira wa mikono na mipira 10, mitano ya mpira wa miguu na mitano ya mpira wa mikono. (Kwa hisani ya Jukwaa Huru)

ANYOFOLEWA SEHEMU ZA SIRI NA MKEWE KUTOKANA NA KUTOHUDUMIA FAMILIA YAKE



Na Steven Augustino,
Tunduru.

MKAZI mmoja wa kijiji cha Mchuluka wilayani Tunduru mkoa wa Ruvma, Abdalah Njuga (23) amelazimika kutoa talaka kwa mkewe baada ya kumtuhumu kumjeruhi kwa kumvuta sehemu zake za siri, na kumsababishia maumivu makali.

Kufuatia hali hiyo Njuga alichukua hatua hiyo ya kuachana nae kwa madai kwamba, maamuzi hayo yametokana na hofu ya kuendelea kupata madhara zaidi.  

Akizungumza kwa taabu, Njuga ambaye amelazwa katika hospitali ya wilaya yaTunduru, alisema chanzo cha tukio hilo, kimetokana na mkewe kumtuhumu kushindwa kumhudumia yeye pamoja na watoto wake, kwa kuwapatia mahitaji muhimu ya maisha yao ya kila siku.
  
Akifafanua taarifa hiyo Njuga alisema kuwa katika tukio hilo mkewe huyo ambaye alimtaja kwa jina la Sauda Njuga, alisema kuwa pamoja na kumvuta nyeti hizo, pia alimpiga kwa kutumia mti na kumuuma meno sehemu mbalimbali za mwili wake.

Alisema ugomvi huo ulianza usiku wa manane wakati mkewe ghafla alipoanza kucharuka na kuanza kumshambulia mwilini, na baadaye kumvuta sehemu zake za siri ambapo baada ya tukio hilo ndipo alikimbizwa katika zahanati ya kijiji cha Mchuluka, kwa ajili ya kupatiwa matibabu ya huduma ya kwanza.

Mganga mfawidhi wa hospitali hiyo Dokta Joseph Ng’ombo alisema kuwa hali ya majeruhi huyo inaendelea vizuri, baada ya kupatiwa matibabu.

Alisema katika tukio hilo majeruhi huyo aliumizwa vibaya sehemu zake
za siri, pamoja na kupata majeraha makubwa mwilini mwake.