Monday, February 24, 2014

MAFUNZO YA UTENGENEZAJI VITO VYA THAMANI MBINGA YAKAMILIKA, WASHIRIKI WAIOMBA SERIKALI KUUNGA MKONO

Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
 
WASHIRIKI wa mafunzo ya kutengeneza vito vya thamani wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, wameiomba serikali wilayani humo kuendelea kuunga mkono mafunzo waliyoyapata ili yaweze kuleta faida kwa kizazi cha sasa na kijacho.
 
Kauli hiyo ilitolewa kupitia risala yao iliyosomwa na mmoja kati ya washiriki hao, Editha Komba mbele ya mgeni rasmi Mkuu wa wilaya hiyo Senyi Ngaga wakati wa kufunga mafunzo hayo ya wiki mbili yaliyofanyika katika chuo cha maendeleo ya wananchi (FDC) kilichopo mjini hapa.
 
Aidha katika risala hiyo washiriki hao walisema wameweza kujifunza kutengeneza ukataji wa vipande vya aluminiamu na shaba, kutengeneza mapambo mbalimbali kama vile heleni, cheni na bangili.
 
Walieleza kuwa wameweza kujifunza kutumia vitu vya asili kama vile mbegu za maembe, kahawa, maboga na manyoya ya kuku kutengeneza mapambo ya asili.

Friday, February 21, 2014

POLISI WAFANIKIWA KUKAMATA JAMBAZI LILILOKUWA LIKITESA WANANCHI WA MBINGA KWA MUDA MREFU

Jambazi linalodaiwa kuwa sugu Roster Ndunguru (katikati) akiwa chini ya ulinzi wa polisi katika hospitali ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, ambako amelazwa baada ya kuambulia kipigo kutoka kwa Polisi wakati akijaribu kutoroka.

Jambazi linalodaiwa kuwa sugu Roster Ndunguru (27) mkazi wa kijiji cha Mbangamao akiwa amefungwa pingu katika hospitali ya wilaya ya Mbinga ambako amelazwa baada ya kuambulia kipigo kikali kutoka kwa Polisi wakati akijaribu kutoroka mikononi mwao. (Picha zote na Kassian Nyandindi)



Na Kassian Nyandindi,

Mbinga.

JESHI la Polisi wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, limefanikikwa kumkamata Roster Ndunguru mkazi wa kijiji cha Mbangamao wilayani humo ambaye anadaiwa kuwa ni jambazi sugu na amekuwa akifanya matukio mengi ya kiuhalifu ikiwemo kuwajeruhi watu na kunyang’anya mali zao.

Aidha Jambazi hilo lilikuwa likitafutwa kwa muda mrefu baada ya kumjeruhi Mratibu elimu kata ya Mbangamao, Florence Kowelo kwa kumjeruhi sehemu mbalimbali za mwili wake na kumpiga na kitu kizito kichwani.

Tukio hilo imeelezwa kuwa lilitokea majira ya usiku wakati Mratibu huyo akiwa nyumbani kwake amelala na familia yake, ambapo baada ya kupiga kelele majirani walijitokeza na jambazi hilo lilitokomea kusikojulikana.

Kwa mujibu wa chanzo cha uhakika kutoka Jeshi la Polisi wilayani Mbinga ambacho hakikutaka jina lake litajwe katika mtandao huu, kilisema kuwa Roster amekuwa na matukio mengi ya kiujambazi ambayo amekuwa akiyafanya katika maeneo mbalimbali wilayani humo.

Tuesday, February 18, 2014

HALMASHAURI YA MBINGA YAINGIA MKATABA WA MAFUNZO YA KUTENGENEZA VITO VYA THAMANI, WAKOREA KUJENGA KIWANDA

Mbunge wa jimbo la Mbinga Gaudence Kayombo(aliyesimama) akisisitiza jambo wakati wa kumkaribisha mtaalamu wa madini kutoka Korea, Dokta Kim (katikati) ambaye ana lengo la kupanua soko la madini kwa wachimbaji wadogo wadogo wa madini na kutangaza fursa za kimaendeleo kwa mataifa mengine wilayani Mbinga. Kushoto ni mtaalamu mwenzake aitwaye Changlee.



Mtaalamu wa madini ambaye ni wa kwanza kutengeneza vito vya thamani Korea kusini Dokta Kim, (kushoto) akiweka sahihi katika mkataba aliotiliana nao na Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma katika hafla fupi iliyofanyika ukumbi wa chuo cha maendeleo uliopo mjini hapa, Upande wa kushoto kwa Dokta Kim ni mkuu wa chuo cha maendeleo ya jamii (FDC) wilayani Mbinga Aidan Mchawa naye akiweka sahihi katika mkataba huo wa kutoa mafunzo ya kutengeneza vito hivyo na kujenga kiwanda cha kutengeneza vito vya thamani wilayani humo, kiwanda hicho kinatarajiwa kujengwa na wakorea hao miaka mitano ijayo. Wanaoshuhudia kutoka kushoto ni Askofu wa jimbo la Mbinga John Ndimbo na anayefuatia ni Mbunge wa jimbo la Mbinga Gaudence kayombo. (Picha na Kassian Nyandindi)

Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
 
HALMASHAURI ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma kupitia chuo chake cha maendeleo ya jamii (FDC) kilichopo mjini hapa, kimeingia mkataba na mtaalamu wa madini ambaye anafahamika kwa jina la Dokta Kim kutoka nchi ya Korea kusini, kwa ajili ya kutoa mafunzo ya wiki mbili ya utengenezaji wa vito vya thamani.
 
Pia mkataba huo unalenga miaka mitano ijayo mtaalamu huyo ataweza kujenga kiwanda cha kutengeneza vito vya thamani wilayani humo, jambo ambalo litaweza kupanua soko la ajira kwa wananchi wa wilaya hiyo.
 
Akizungumza katika hafla fupi ya kutiliana sahihi katika ukumbi wa chuo cha maendeleo uliopo Mbinga mjini, Dokta Kim alisema yeye ni mtu wa kwanza katika nchi hiyo ya Korea kusini ambaye anaongoza kwa utengenezaji wa vito vya thamani, hivyo anawaomba washiriki walioteuliwa kujiunga na mafunzo hayo kuwa makini wakati watakapo kuwa darasani.
 
Dokta Kim alisema kuwa wazo hili la kuja Mbinga na kutaka kufanya hayo ni jitihada zilizofanywa na Mbunge wa jimbo la Mbinga Gaudence Kayombo, ambapo mafunzo hayo yataweza kuwafungua vijana wa wilaya hiyo waweze kufanya shughuli za utengenezaji wa vito hivyo na kuweza kuondokana na umasikini.

Monday, February 17, 2014

WAZAZI WILAYANI MBINGA WASHAURIWA KUPELEKA WATOTO WAO KATIKA CHUO CHA UFUNDI PILIKANO

Kibao kikionyesha mwelekeo wa chuo cha ufundi Pilikano, ambacho kipo umbali wa kilometa 18 kutoka Mbinga mjini mkoani Ruvuma.

Wanafunzi wakijifunza ufundi wa umeme wa majumbani.

Baadhi ya wanafunzi wakiwa darasani wakijifunza fani ya ushonaji.

Mkurugenzi wa chuo cha ufundi Pilikano, Bruno Kapinga, akizungumza na mwandishi wa habari hizi (Hayupo pichani) wakati wa mahojiano yaliyofanywa juu ya maendeleo ya chuo hicho. (Picha zote na Gwiji la matukio Ruvuma)



Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

WADAU wa elimu wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, wametakiwa kuwa na mwamko wa kupeleka watoto wao katika vyuo vya ufundi hususani kwa vile ambavyo vipo karibu na maeneo yao, ili waweze kupata ujuzi wa aina mbalimbali.

Aidha imeleezwa kuwa watoto wanaomaliza darasa la saba wilayani humo, wamekuwa wengi wakizurula mitaani hivyo ni vyema sasa wakapelekwa katika vyuo hivyo ili waweze kuwa na maendeleo katika fani za ufundi kwa faida ya kizazi cha sasa na baadaye.

Wito huo ulitolewa na Mkurugenzi wa chuo cha ufundi Pilikano Bruno Kapinga, kilichopo katika kata ya Mkumbi wilayani Mbinga wakati alipokuwa akihojiwa na mwandishi wa habari hizi juu  ya maendeleo ya chuo hicho.

Kapinga alisema kuwa chuo hicho kimesajiliwa na VETA na kilianza rasmi kutoa mafunzo ya ufundi mwaka 2012 katika fani ya ushonaji, magari na umeme.

Mkurugenzi huyo alisema kwamba wazo la kujenga chuo alilipata baada ya kupata ufadhili kutoka Uholanzi, ambapo wafadhili kutoka katika nchi hiyo waliweza kumsaidia vifaa vya ufundi katika fani hizo.

Tuesday, February 11, 2014

MBINGA NAKO KWA CHAFUKA WAFANYABIASHARA WAGOMA

Jakaya Kikwete, Rais wa Tanzania.

 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
 
HALI  si shwari  katika  mji  wa Mbinga mkoani Ruvuma, kufuatia  kuanza kwa mgomo  usio na kikomo wa wafanyabiashara kama njia ya  kufikisha ujumbe  kwa Waziri wa viwanda na biashara   na  serikali ya  Rais Jakaya  Kikwete,  juu ya gharama za mashine za kutolea risiti (EFD) wakidai kwamba gharama hizo ni kubwa na ni sawa na kumtishwa mzigo mfanyabiashara ambao hauna tija kwake.  


Mgomo huo umeanza leo  asubuhi  hii  huku  makundi ya wafanyabiashara wakiwa wamekusanyika katika maeneo mbalimbali ya mji huo, huku wakipanga kufanya maandamano  kuwaadhibu wenzao wanaokiuka mgomo huo ambao wataonekana wamefungua maduka.


Hali kwa upande wa wakazi wa Mbinga mjini  na wale wa maeneo ya vijijini ambao  wanakuja kwa ajili ya kupata huduma mbalimbali imewafanya wawe katika wakati mgumu kutokana na mgomo huo, hivyo kujikuta wakiambulia makufuri katika maduka hayo.


Wafanyabiashara  hao  wametoa onyo kwa  wenzao iwapo  watafungua  maduka yao  watakiona cha moto  na  kuanzia  wakati  wowote sasa,  wataanza msako wa duka moja hadi jingine kwani wamesema mgomo  huo ni wa nchi nzima na wao  wametii uamuzi wa  wafanyabiashara wenzao katika mikoa yote iliyopo hapa nchini.

Saturday, February 8, 2014

OFISA ELIMU SHULE ZA SEKONDARI MBINGA AVULIWA MADARAKA, WAZIRI ASEMA NIMEMSHUSHA MADARAKA AKAFUNDISHE AKIWA MWALIMU WA KAWAIDA

Naibu Waziri Elimu na Mafunzo ya Ufundi Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Kassim Majaliwa, akiwasili wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma baada ya kupokelewa na Mkuu wa wilaya hiyo (Kulia kwake) Senyi Ngaga katika eneo la Kanisa Katoliki (Jimboni) lililopo mjini hapa.

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Kassim Majaliwa akiweka sahihi katika vitabu vya wageni baada ya kuwasili kwenye ofisi ya Mkuu wa wilaya ya Mbinga, Senyi Ngaga ambaye yupo mbele yake akishuhudia.

Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Kassim Majaliwa akizungumza na Walimu hawapo pichani wa wilaya hiyo katika ukumbi wa UVIKAMBI uliopo Mbinga mjini, upande wa kulia mwanzo kwake Waziri ni Mkuu wa wilaya hiyo Senyi Ngaga na wa mwisho kutoka kwa Mkuu wa wilaya hiyo ni Katibu tawala wa wilaya hiyo Stephano Ndaki. (Picha zote na Gwiji la Matukio Ruvuma)


Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

NAIBU Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Ofisi ya Waziri mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Kassim Majaliwa amemvua madaraka kwa kumshusha cheo Ofisa elimu shule za sekondari wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Hanji Yusuph Godigodi kwenda kuwa mwalimu wa kawaida wa sekondari kutokana na Ofisa huyo kushindwa kutekeleza majukumu yake ya kazi na kufanya ubadhirifu wa shilingi milioni 268 za maendeleo ya elimu ya sekondari wilayani humo.

Aidha amewashusha vyeo Wakuu wa shule za sekondari sita za wilaya hiyo kwenda kuwa walimu wa kawaida, kutokana na walimu hao wakidaiwa
kushirikiana na Ofisa huyo wa sekondari kufanya ubadhirifu wa fedha hizo.

Hatua ya Naibu Waziri huyo kuwashusha vyeo viongozi hao ilifikiwa katika kikao ambacho alikuwa akizungumza na Walimu wa shule za msingi na sekondari wilayani humo, ambacho kiliketi kwenye ukumbi wa Uvikambi uliopo mjini hapa na kwamba Waziri huyo yupo katika ziara yake ya kikazi wilayani Mbinga kwa muda wa siku mbili.

Waziri Majaliwa aliwataja wakuu wa shule za sekondari wilayani Mbinga ambao wameshushwa madaraka kuwa ni William Hyera ambaye ni wa shule ya
sekondari Maguu, Clemence Sangana anatoka shule ya sekondari Mkuwani, Method Komba Langilo sekondari, John Tillia Ukilo sekondari, Leonard Juma Luli Sekondari huku akimtaja kwa jina moja mwalimu Konga ambaye yupo sekondari ya Kihangimahuka.

Wednesday, January 29, 2014

DOKTA KAMANI AFUNGUKA AWATAKA WAFANYAKAZI WASIOENDANA NA KASI YAKE WAJIONDOE MAPEMA




Na Mwandishi wetu,


WAZIRI  wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi Dokta Titus Kamani, amesema ili kwenda na kasi ya maboresho ya wizara hiyo, inahitajika dhana ya uwajibikaji na uwazi sambamba na kujitolea kwa nguvu zote katika kufanya kazi.

Kamani, aliyasema hayo juzi katika mkutano wa kwanza uliowakutanisha wafanyakazi wote wa wizara hiyo, wakiwemo wastaafu wa mwaka jana katika ofisi ya wizara hiyo ilizopo Temeke jijini Dar es Salaam.

Alisema kama kuna mtu ambaye ni kikwazo katika kukwamisha shughuli za wizara, ni bora akawapisha mapema na kwamba kila mtumishi kwa nafasi yake, anatakiwa kuifanya kazi kwa uwazi na akaitaka wizara kufanya kazi na vyombo vya habari kwani ndio njia pekee ya kuwafanya watanzania wajue wizara inafanya nini.

“Wewe upo ofisini, halafu unaogopa ogopa vyombo vya habari, kwani unatatizo gani kuweni wazi mambo yenu yawe hadharani watanzania wa Mbeya wayajue, Rufiji mpaka Pemba, hakuna kuficha ficha jambo katika wizara yangu.” alisistiza Dokta Kamani.

Alisema wizara ya maendeleo ya mifugo na uvuvi ndio moyo wa taifa kwani huwajumuisha watanzania wengi wenye maisha ya kawaida, lakini amesikitishwa kwa jinsi ambavyo wizara hiyo imekuwa ikichukuliwa na baadhi ya watu kama ni wizara yenye migogoro na kuleta hasara maeneo mengine.

GUNINITA AMRUSHIA KOMBORA NAPE


Na Mwandishi wetu,
Dar es Salaam.

KITENDO cha Katibu mwenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Nape Nnauye cha kupinga uteuzi wa Mawaziri uliofanywa na Mwenyekiti wa chama hicho ambaye ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni mwendelezo wa tabia zake za ukosefu wa nidhamu kwa viongozi wake.

Hayo yamo katika taarifa yake kwa vyombo vya habari aliyoitoa hivi karibuni, ambapo aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Dar es salaam, John Guninita  amesema Nape ni mkiukwaji wa maadili, asiyeheshimu wakubwa ambao wamemteua kushika nafasi hiyo.

Alisema ni kiongozi ambaye anatakiwa kufanya kazi kwa  kuzingatia mipaka yake hivyo ni vema akafahamu kuwa madaraka ya kuteua Baraza la mawaziri ni kazi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano na sio vinginevyo.

Guninita alisema hata kama ingetokea Rais akashauriwa na washauri zaidi ya mia moja, bado uamuzi wake unapaswa kuheshimiwa na hakuna mtu anayeweza kuingilia au kubeza.

Wednesday, January 15, 2014

CHAMA CHA WALIMU MBINGA KWA CHAFUKA, NAIBU KATIBU MKUU TAIFA APOKELEWA KWA MABANGO

Baadhi ya Wanachama wa CWT wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, wakiwa wameshika mabango yenye ujumbe wa aina mbalimbali ambayo yanawashutumu Katibu wao wa mkoa huo Zebedayo Mwasandungila na wa wilaya hiyo Samwel Mhaiki, ambapo Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho kwa hasira alikataa kuyasoma na kuwaambia Wajumbe wa mkutano huo twendeni kwanza ndani kwenye ukumbi tukafanye mkutano.



Bado Wajumbe wa mkutano huo wakiwa ndani ya ukumbi wa Jumba la maendeleo uliopo mjini hapa ambako mkutano huo ulikuwa ukifanyika, wakiwa na hasira na kuendelea kushika mabango yenye ujumbe wa aina mbalimbali ambao ulikuwa ukiwashutumu baadhi ya viongozi wao wa mkoa na wilaya ya Mbinga .

Katibu Mkuu wa Chama Cha Walimu Tanzania, Ezekiah Oluoch, akihutubia katika ukumbi wa Jumba la maendeleo uliopo mjini hapa, mara baada ya Wanachama wa chama hicho kutuliza jazba zao. Upande wa kulia ni Mbunge wa jimbo la Mbinga Gaudence Kayombo na kushoto ni Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya hiyo Hussein Ngaga. (Picha zote na Kassian Nyandindi) 



Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Walimu Tanzania (CWT) Ezekiah Oluoch amejikuta akiwa katika wakati mgumu, baada ya kupokelewa na wanachama wa chama hicho wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, kwa malalamiko ya hapa na pale na mabango yaliyobeba ujumbe wa aina mbalimbali ambayo yalikuwa yakiwashutumu Katibu wa CWT wa mkoa huo na Wilaya hiyo.

Waliokuwa wakishutumiwa ni Zebedayo Mwasandungila ambaye ni Katibu wa CWT mkoa wa Ruvuma na Samwel Mhaiki, Katibu wa chama hicho wilayani Mbinga ambao wanalalamikiwa kutengeneza makundi ndani ya chama.

Vilevile Mhaiki alikuwa akinyoshewa kidole kwamba yeye na kamati yake ya chama wilayani humo, wameshindwa kukiongoza chama na badala yake makato wanayokatawa wanachama ya asilimia 15 katika mishahara yao hawarejeshewi katika matawi yao, hivyo hawaoni sababu ya kuendelea kubaki na viongozi hao na kuwataka wajiuzuru mara moja.

Walisema wamekwisha mpatia Bw. Mhaiki notisi ya siku 30 kwa lengo la kusudio la kumfikisha Mahakamani ili haki zao ziweze kupatikana.

“Tumekwisha mwona mwanasheria kwa lengo la kusudio la kumfikisha Mahakamani ndugu Samwel Mhaiki, na sasa tumempatia notisi ya siku 30 atuambie fedha zetu za makato ya kila mwezi zipo wapi”, walisikika wakisema kwa sauti.

Wednesday, January 8, 2014

WATUHUMIWA MAUAJI YA MLINZI WA GAPCO WAPANDISHWA KIZIMBANI

Watuhumiwa wanaodaiwa kumuua mlinzi wa kampuni ya GAPCO inayouza mafuta wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, wakipandishwa katika Karandika la Polisi baada ya kusomewa mashtaka yao katika Mahakama ya wilaya hiyo leo. (Picha na Kassian Nyandindi)










Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

WATU watano wakazi wa Mbinga mjini mkoani Ruvuma, wameburutwa katika Mahakama ya wilaya ya Mbinga mkoani humo kwa tuhuma ya mauaji ya mlinzi wa kituo cha kuuza mafuta GAPCO, kilichopo mjini hapa.

Mwendesha mashtaka wa Polisi Inspekta Nassib Kassim alidai mbele ya Hakimu wa Mahakama ya wilaya hiyo, Joackimu Mwakyolo kuwa tukio hilo lilitokea Desemba 31 mwaka huu majira ya usiku.

Kassim aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Thito Turuka (30), Boniface Nombo (40), Ally Aman Chinga (29), Egno Nchimbi (24) na Felix Turuka (38).

Monday, January 6, 2014

TUNDURU WATAKIWA KUJENGA MSHIKAMANO NA UPENDO



Aliyesimama Diwani wa kata ya Majengo Athuman Nkinde akisisitiza jambo kabla ya kugawa vifaa vya kutengeneza batiki na sabuni za maji na vipande, kwa vikundi vya Majengo A na B wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma. Ambao wameketi ni viongozi wengine wa kata hiyo.  


Na Steven Augustino,
Tunduru.

WANACHAMA na wakereketwa wa chama cha Mapinduzi (CCM) katika kata ya Majengo wilayani Tunduru Ruvuma, wamehimizwa kudumisha muungano na upendo miongoni mwao na kuhakikisha wanapata ushindi wa  chama chao katika chaguzi zijazo za serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika mwaka huu.

Mariwani Athumani Nkinde wa Kata hiyo na  Diwani waviti maalumu wa tarafa ya Mlingoti Bi. Atingala Mohamed walisema hayo kwa nyakati tofauti  wakati wa  uzinduzi wa mradi wa maji safi ya bomba ugawaji wa vifaa vya kutengenezea Batiki, mafuta ya kupaka, sabuni za maji, na vipande katika kata hiyo.

Madiwani hao walisema kuwa endapo wanaCCM hawatashikamana katika ujenzi na uimarishaji wa chama chao ipo hatari ya mamluki kuingia miongoni mwao, na kuwavuruga kwa lengo la kuvipatia ushindi vyama pinzani.
 
Akifafanua taarifa ya ujenzi wa mtandao wa bomba la maji hayo na vifaa hivyo Diwani Athuman Nkinde, alisema kuwa hadi kukamilika kwake miradi hiyo imegharimu shilingi 400,000 na akatumia nafasi hiyo kuwaomba waitumie na kuitunza.

WAKAZI WA MBINGA MJINI WASHAURIWA KUTOA MSAADA KWA WAGONJWA

Mganga wa zamu wodi ya watoto (kulia) katika hospitali ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma,  Revina Kayombo akipokea msaada wa sabuni za kufulia wagonjwa, kutoka kwa Philiberth Hyera (aliyevaa suti nyeusi ambaye amekaa) mkazi wa Mbinga mjini. Hyera alitoa wito kwa wakazi wengine waliopo mjini hapa kupenda kuwasaidia wagonjwa.

Aliyevaa suti nyeusi ni Philiberth Hyera mkazi wa Mbinga mjini akitoa msaada wa sabuni za kufulia, kwa wagonjwa ambao wamelazwa katika wodi ya akina mama hospitali ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, hivi karibuni. (Picha zote na Kassian Nyandindi)

Thursday, January 2, 2014

UWT MBINGA YAWATAKA AKINA MAMA KUEPUKANA NA MAKUNDI YA ANASA

Wanachama wa UWT wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kukabidhi zawadi zao walipokwenda kuwataka hali akina mama wenzao ambao wamelazwa katika hospitali ya wilaya hiyo iliyopo mjini hapa.


Upande wa kushoto aliyevaa shati la kijani ni Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, Pendo Ndumbaro akifurahia jambo baada ya kushika mtoto mchanga ambaye alizaliwa usiku wa kuamkia mwaka mpya (2014) alipokuwa ametembelea jana wodi ya akina mama katika hospitali ya wilaya hiyo iliyopo mjini hapa kwa lengo la kuwataka hali, na wanaoshuhudia ni baadhi ya akina mama ambao wamelazwa katika hospitali hiyo. (Picha zote na Kassian Nyandindi).



Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
 
WANAWAKE wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma wametakiwa kuwa makini katika kuendesha maisha yao kwa kujishughulisha na kilimo, biashara na kujiunga na vyama vya akiba na mikopo ili waweze kuepukana na kujiingiza kwenye anasa ambazo zinachangia maambukizi ya virusi vya ukimwi.
 
Sambamba na hilo wameshauriwa kushirikiana na kuchukua hatua katika kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazowakabili katika maisha yao ya kila siku kwa kufanya kazi kwa bidii.

Rai hiyo ilitolewa  jana na Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) wilayani Mbinga Pendo Ndumbaro, alipokuwa akizungumza na akina mama waliolazwa katika hospitali ya wilaya hiyo iliyopo mjini hapa ambao aliwatembelea kwa lengo la kuwataka hali na kuwapa zawadi mbalimbali.

Pia Mwenyekiti huyo alikuwa ameambatana na wanachama wenzake wa umoja huo ambao walishiriki kwa pamoja kwenda kuwaona wagonjwa hao waliokuwa wamelazwa katika hospitali hiyo.

GAUDENCE KAYOMBO ASIKITISHWA NA UJENZI WA BARABARA KIWANGO CHA LAMI KUTOKA SONGEA KWENDA MBINGA

Gaudence Kayombo.



















Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

MBUNGE wa jimbo la Mbinga Gaudence Kayombo amesema, ujenzi wa  barabara kiwango cha lami kuanzia eneo la Likuyufusi pacha ya Peramiho wilaya ya Songea hadi Mbinga, katika baadhi ya maeneo umejengwa kwa kiwango kisichoridhisha kutokana na barabara hiyo kuanza kuwekwa viraka kabla ya kukabidhiwa rasmi mikononi mwa serikali.

Kayombo alisema hayo alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habari hizi mjini hapa, huku akisisitiza kuwa hali hiyo huenda ikatokana na wataalamu husika kutozingatia ipasavyo vipimo vya kimaabara na ndio maana barabara hiyo hubomoka na kulazimika kuweka viraka.

Alisema uzembe huo uliofanywa wa kutozingatia viwango husika ni hasara kubwa kwa serikali kutokana na fedha nyingi iliyotumika kujengea barabara hiyo kutofanya kazi yake kama ilivyokusudiwa.

MLINZI AUAWA NA MAJAMBAZI KWA KUKATWA KOROMEO


Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

MLINZI wa kituo cha kuuza mafuta GAPCO kilichopo Mbinga mjini mkoani Ruvuma, amekutwa akiwa ameuawa kikatili na watu wasiojulikana kwa kukatwa koromeo na kujeruhiwa vibaya sehemu mbalimbali za mwili wake.

Kwa mujibu wa taarifa zilizolifikia gazeti hili imeelezwa kuwa aliyeuawa ni Kelvin Mapunda(52) mkazi wa mjini hapa, ambapo mwili wake ulikutwa ukiwa umetelekezwa karibu na eneo la kituo hicho cha mafuta.

Mwandishi wa habari hizi alipofika katika eneo la tukio hilo, alikuta umati mkubwa wa watu ukiwa umezunguka mwili wa marehemu huyo huku wakionekana kuchukizwa na kitendo hicho cha kinyama.

WAKIMBIA FAMILIA ZAO WAKIHOFIA KUKAMATWA NA POLISI


Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

BAADHI ya Wanaume wa kijiji cha Mbangamao kati, kata ya Mbangamao wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma wamezikimbia familia zao wakihofia kukamatwa na polisi baada ya kuvamia nyumba ya Mratibu elimu wa kata hiyo Florence Kowelo, na kumjeruhi kwa kumpiga nondo kichwani.

Watu hao wanadaiwa kufanya kitendo hicho na kutishia usalama wa Watumishi wengine wa serikali, katika kata hiyo baada ya kuwatuhumu wamekuwa na tabia ya kufanya mapenzi na wake zao.

Tukio hilo lilitokea usiku wa Desemba 27 mwaka huu na kwamba vibaka hao ambao wanatamba kijijini hapo kwa jina la M 23, kuwa wameapa kupambana na Watumishi wote waliopo katika kata ya Mbangamao.

Monday, December 23, 2013

UJENZI WA BARABARA KIWANGO CHA LAMI SONGEA HADI MBINGA UTATA MTUPU

Na Kassian Nyandindi,
Songea.
 
UJENZI wa barabara kiwango cha lami kuanzia eneo la Likuyufusi pacha ya Peramiho wilaya ya Songea hadi Mbinga, umeanza kuzua malalamiko kutokana na barabara hiyo kuanza kuwekwa viraka kabla ya kukabidhiwa rasmi mikononi mwa serikali.
 
Barabara hiyo ambayo ni ya kilometa 78 inagharimu kiasi cha shilingi bilioni 79.8 na kutekelezwa chini ya mradi mkuu wa changamoto za milenia Tanzania (MCAT).
 
Fedha za ujenzi wa barabara hiyo ni miongoni mwa dola 698 za Kimarekani zilizotolewa nyakati za mwisho katika utawala wa Rais mstaafu George Bush, ikiwa ni sehemu ya msaada kwa ajili ya kujenga miradi mbalimbali ya kimaendeleo hapa nchini.
 
Malalamiko hayo yalitolewa kwa nyakati tofauti wakati mwandishi wa habari hizi alipokuwa akizungumza na wananchi wa Songea na Mbinga, ambapo walisema kuwa ni jambo la kushangaza kuona ujenzi wa barabara hiyo kabla haijakabidhiwa rasmi imeanza kuwekwa viraka baadhi ya maeneo.

Sunday, December 22, 2013

TAMCU TUNDURU WALIA NA TAKWIMU ZA KOROSHO



Na Steven Augustino,

Tunduru.

CHAMA kikuu cha ushirika Wakulima wa korosho wilaya ya Tunduru (TAMCU) mkoani Ruvuma, kimefanikiwa kukusanya tani  554 ambazo ni kidogo, kati ya tani 9115 zilizokadiriwa kuzalishwa katika msimu wa mwaka huu.

Hayo yalisemwa na Katibu mkuu wa chama hicho wilayani humo, Imani Kalembo akiwemo na Mwenyekiti wake Mahamudu Katomondo mbele ya waandishi wa habari, waliokuwa wakifanya mahojiano nao mjini hapa juu ya maendeleo ya uzalishaji wa zao hilo.

Viongozi hao walifafanua kwamba wamepata wakati mgumu kukusanya takwimu hizo za uzalishaji, kwa kile walichoeleza kuwa kutokana na wilaya hiyo kuwa na utaratibu mbovu uliotumika kununulia zao hilo katika msimu wa mwaka huu.

"Takwimu tulizowapeni ni zile ambazo tu zimetokana na manunuzi yaliyofanywa na TAMCU kupitia vyama 18 vya ushirika vya wakulima ambavyo vipo katika tarafa za Lukumbule, Namasakata, Nalasi, Matemanga, Mlingoti Nakapanya na Namtumbo ambako chama kilipeleka fedha kwa ajili ya ununuzi wa Korosho", alisema Kalembo.

MAHAKAMA KUTOA MAAMUZI JUU YA MAUZO MBAO ZILIZOKAMATWA KATIKA OPARESHENI TOKOMEZA UJANGILI



Na Steven Augustino,
Tunduru.

MAHAKAMA ya wilaya Tunduru mkoani Ruvuma, imepanga kutoa maamuzi ya kuuza au kutouzwa kwa mbao 8,328 zenye thamani ya shilingi milioni 291.4 ambazo zilikamatwa kupitia “Oparesheni tokomeza ujangili”, iliyofanyika hivi karibuni kuanzia Oktoba hadi Desemba mwaka huu.

Hakimu mfawidhi wa Mahakama hiyo Ernest Mgongolo alisema hayo wakati alipokuwa akijibu, maombi yaliyotolewa na Mawakili waliokuwa wakiwakilisha upande wa serikali katika kesi tano zinazowakabili watuhumiwa saba ambao walinaswa wakati wa oparesheni hiyo wakiwa na na mbao hizo kinyume cha sheria.

Watuhumiwa hao ni wakazi wa Jijini Dar es Salaam na Mtwara  ambapo awali wakitoa maombi, Wanasheri  wa serikali  Mwahija Sembeni na Francis Aloyce waliiomba Mahakama kwa mamlaka iliyonayo kutumia kifungu cha sheria namba 352 kifungu kidogo (2) kinacho ambacho huruhusu kutoa kibali cha kuuzwa kwa kidhibiti chochote au mali ambayo ipo mbele ya mahakama na yenye kuweza kuharibika.

Wednesday, December 18, 2013

MKUU WA MKOA WA RUVUMA ALIA NA WAKUGURUGENZI WA HALMASHAURI KUWAPA KAZI WAKANDARASI WAZEMBE

Na Muhidin Amri,

Ruvuma.

SERIKALI mkoani Ruvuma imewaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri  za wilaya katika mkoa huo, kutowapa tena zabuni Wakandarasi ambao ni wababaishaji, wazembe na wenye rekodi mbaya katika utendaji wa kazi zao, ili wasiweze kuisababishia serikali hasara ya kuingia gharama nyingine upya ya ujenzi wa miradi ya Wananchi.

Mkuu wa mkoa huo Said Mwambungu aliyasema hayo mwishoni mwa wiki wakati akifungua kikao cha siku moja cha Wajumbe wa jumuiya ya serikali za mitaa(ALAT) kilichofanyika mjini Namtumbo mkoani humo, ambapo alitumia nafasi hiyo kupiga marufuku wakandarasi wasiokuwa na sifa kuomba na kufanya kazi katika mkoa wa Ruvuma kwani wamekuwa wakiurudisha nyuma maendeleo ya taifa letu kwa ujumla.

Mwambungu amesikitishwa na usimamizi mbovu wa fedha zinazotolewa na serikali wakati wa utekelezaji wa miradi mbalimbali, ambapo imebainika kuwa wakandarasi wengi wamekuwa na tabia ya wizi kwa kuingia mikataba hewa na halmashauri husika na wakishapata fedha hukimbia bila kukamilisha kazi walizoomba kufanya, tatizo ambalo alidai kuwa linachangiwa kwa kiasi fulani na baadhi ya watumishi hasa wakuu wa idara wasiokuwa waaminifu.

Alisema ni kosa kumpa kazi Mkandarasi mwenye rekodi mbaya huku akiwaonya Wakurugenzi na Wenyeviti wa Halmashauri  juu ya tabia ya kuwa na urafiki wa jirani na wakandarasi hao kwa kile alichoeleza kuwa kinatokana na tamaa ya fedha huku akisisitiza ni vema  kutoa kipaumbele kwa wakandarasi waaminifu  na wenye sifa ambao wanatimiza majukumu yao ya kazi kwa viwango vinavyotakiwa.