Monday, July 20, 2015

MWANDISHI WA HABARI KASSIAN NYANDINDI ATANGAZA RASMI NIA YA KUGOMBEA UDIWANI KATA YA MBINGA MJINI A

Mwandishi wa habari Kassian Nyandindi, ambaye ametangaza nia ya kugombea udiwani katika kata ya Mbinga mjini A, iliyopo wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi. (CCM)
Na Dustan Ndunguru,
Mbinga.

KASSIAN Nyandindi ambaye amebobea katika fani ya uandishi wa habari, na sasa anaandikia gazeti la Majira mkoani Ruvuma, ametangaza nia yake ya kugombea udiwani katika kata ya Mbinga mjini A, iliyopo wilayani Mbinga mkoani humo kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Akizungumza leo na vyombo mbalimbali vya habari mjini hapa, Nyandindi alisema amekwisha chukua fomu ya kuwania nafasi hiyo na kuirejesha, huku akitamka vipaumbele vyake endapo wananchi wa kata hiyo watampatia ridhaa ya kuwaongoza, atahakikisha huduma muhimu za kijamii zinaboreshwa.

Alisema atazingatia kwamba miundombinu mbalimbali kama vile barabara za mitaa, afya, maji na elimu vinaboreshwa huku akisisitiza kuboresha elimu kutoka ngazi ya elimu ya msingi hadi sekondari kwa kuwataka pia wazazi kupeleka watoto wao shule na kuwapatia mahitaji muhimu ili mtoto aweze kusoma vizuri.  

“Uwezo wa kuongoza na kushughulikia matatizo ya wananchi wa kata hii ninao, kinachotakiwa hapa ni kutumia rasilimali tulizonazo ili tuweze kujipatia maendeleo na kuweza kuondokana na umasikini”, alisema Nyandindi.

Sunday, July 19, 2015

KALUMANGA MBIONI NA UBUNGE VITI MAALUM RUVUMA

Mwanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Songea mkoani Ruvuma, Sondy Kalumanga kulia, akipokea fomu ya kuomba kugombea ubunge viti maalum kupitia tiketi ya CCM mkoani humo.

TINGA TINGA NA MIKAKATI YA MAENDELEO KATA YA MTIPWILI NYASA

Stanford Nyambo (Tinga tinga)
Na Dustan Ndunguru,

MWAKA huu unatarajiwa kufanyika uchaguzi mkuu ambapo Madiwani, Wabunge na Rais watachaguliwa na kuongoza kwa kipindi cha miaka mitano ijayo, ambapo uchaguzi huo utafanyika kwa kuvihusisha vyama ambavyo vimesajiliwa kisheria.

Chama Cha Mapinduzi (CCM) ndicho chama kinachoongoza nchi ya Tanzania kwa kipindi kirefu sasas, kwa kuhakikisha amani na utulivu kwa wananchi wake vinaendelea kuwepo.

CCM ni chama ambacho Watanzania wengi wanakiamini na kukichagua kushika dola tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992.

Watanzania hawa wameamua kwa dhati kuwachagua wagombea waliotokana na chama hiki tawala, kutokana na kuridhishwa na sera zake nzuri ambazo kimsingi zimekuwa zikilenga kuwaletea maendeleo wananchi, ikilinganishwa na sera za vyama pinzani.

KALOLO NA HARAKATI ZA KUPATA UBUNGE TUNDURU KASKAZINI

Ajili Kalolo, mgombea nafasi ya ubunge jimbo la Tunduru Kaskazini mkoani Ruvuma, akionesha fomu ya kugombea mara baada ya kuichukua kutoka ofisi za CCM wilayani Tunduru.
Na Steven Augustino,
Tunduru.
WANACHAMA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika jimbo la Tunduru kaskazini wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, wametakiwa kuwa makini na kutokubali kutumiwa na wajanja wachache wanaopita kuwanadi wagombea wanaowania nafasi ya ubunge katika majimbo ya uchaguzi wilayani humo, ambao wakishapata nafasi hiyo huondoka na kwenda kuishi mbali na majimbo yao.
Aidha wanachama hao ambao ni wakereketwa wa CCM, pia wametahadharishwa dhidi ya wagombea wa nafasi hiyo ambao wamekuwa na tamaa ya madaraka, hivyo wameshauriwa kuwachuja kwa hoja zao majukwaani, ili kuona kama kweli watakuwa na uwezo na moyo wa kuwasaidia wananchi pale watakapokuwa wamepewa nafasi ya kuwaongoza.
Hayo yalisemwa na kada wa Chama Cha Mapinduzi na afisa wa idara ya utawala na uwezeshaji  jumuiya ya wazazi  makao makuu ya chama hicho, Omary Kalolo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari, mara baada ya chukua fomu ya kuwania nafasi ya ubunge katika jimbo hilo ambalo awali lilikuwa linaongozwa na mhandisi Ramo Makani.
Alisema kwamba licha ya kila mwanachama wa chama hicho, anayohaki ya kuchukua fomu na kuomba ridhaa ya kuingia katika kinyang’anyiro hicho, lakini wanapaswa kumchagua mtu makini na mwenye uwezo wa kuwaletea maendeleo wananchi wake na sio vinginevyo.

NDILIMALITEMBO SONGEA KUONGOZWA NA DIWANI MWANDISHI WA HABARI

Mgombea nafasi ya udiwani, kata ya Ndilimalitembo katika Manispaa Songea mkoani Ruvuma kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Cresencia Kapinga kushoto, ambaye pia ni mwandishi wa habari gazeti la Majira akijibu maswali kutoka kwa waandishi wa habari mara baada ya kuchukua fomu ya kuomba ridhaa ya kugombea nafasi hiyo katika kata hiyo.
Cresensia Kapinga akisindikizwa, ndugu na jamaa mara baada ya kutoka kuchukua fomu hiyo ya kuwania nafasi ya udiwani katika kata hiyo.


Saturday, July 11, 2015

AJINYONGA KUTOKANA NA KUDAIWA DENI

Na Mwandishi wetu,
Songea.

WATU wawili wamefariki dunia katika matukio tofauti, yaliyotokea wilayani Nyasa na Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, likiwemo la fundiseremala mmoja kujinyonga kutokana na kukimbia deni alilokuwa akidaiwa.

Akifafanua juu ya matukio hayo, Kamanda wa Polisi mkoani humo Mihayo Msikhela alisema tukio la kujinyonga lilitokea mtaa wa Ostarbey, katika kata ya Msamala Songea mjini.

Katika tukio hilo marehemu aliyefahamika kwa jina la PeterLufunda (38) alichukua hatua ya kujinyonga, baada ya Mahakama ya wilaya ya Songea kutoa hukumu ya kuiruhusu SACCOS ya mtaa huo kuuza nyumba yake aliyokuwa akiishi, ili kulipa deni la mkopo wa shilingi milioni 1 ambalo alikopa na kushindwa kulipa.

WAANDISHI NYANDA ZA JUU KUSINI WANOLEWA

Na Steven Augustino,
Lindi.

WAANDISHI wa habari Nyanda za juu kusini, wameshauriwa kufanya utafiti na kuandika habari zitakazofichua vitendo viovu vinavyofanywa na baadhi ya vigogo hapa nchini, ambao wamekuwa wakifanya biashara ya uvunaji misitu na kusafirisha kwa njia za panya jambo ambalo limekuwa likiikosesha serikali mapato yake.

Meneja kampeni ya mama misitu, Gwamaka Mwakyanjala alisema hayo alipokuwa akitoa mafunzo ya siku tano kwa waandishi wa habari wa mikoa ya Ruvuma, Mtwara na Lindi yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Halmashauri ya Lindi mkoani hapa.

Mwakyanjala alifafanua kuwa lengo la mafunzo hayo, ni kuwajengea uwezo waandishi wa mikoa hiyo waweze kuandika habari za misitu ili kusaidia kuibua mijadala ambayo itaiwezesha serikali, kutatua kero ambazo zimekuwa zikijitokeza juu ya uvunaji haramu wa misitu.

Tuesday, July 7, 2015

NYASA WAMPATA MRITHI WA KAPTENI KOMBA MJUMBE WA NEC


Wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani Nyasa mkoa wa Ruvuma, wakishangilia kwa pamoja kumpata mjumbe wa NEC wa wilaya hiyo Alex Shauri, mara baada ya uchaguzi kufanyika jana wilayani humo. (Picha na Kassian Nyandindi)
Na Kassian Nyandindi,
Nyasa.

WANACHAMA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Nyasa mkoa wa Ruvuma, wametakiwa kuwa makini kwa kutokubali kutumiwa na wagombea wanaowania nafasi ya ubunge wilayani humo hasa kwa wale ambao wamekuwa na tamaa ya madaraka, badala yake jukumu lao kubwa ni kuwachuja ili kuona kama kweli watakuwa na uwezo na moyo wa kuwasaidia wananchi, pale watakapokuwa wamepewa nafasi ya kuwaongoza.

Aidha wametakiwa kuhakikisha kwamba, CCM kinapata ushindi wa kishindo katika uchaguzi mkuu ujao unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25 mwaka huu, ambapo hilo litatokana na kujenga mshikamano wa dhati ikiwemo kutangaza kwa wananchi yale yote yaliyotekelezwa kwa vitendo na chama hicho, kama ilivyoainishwa ndani ya ilani yake ya uchaguzi.

Hayo yalisemwa na Mjumbe wa NEC wa wilaya ya Nyasa, Alex Shauri alipokuwa akiwashukuru wajumbe wenzake wa Chama Cha Mapinduzi wilayani humo, mara baada ya kumchagua kupeperusha bendera ya nafasi hiyo katika wilaya hiyo.

POLISI WAMSAKA BINTI ALIYETUPA KICHANGA CHOONI

Na Steven Augustino,
Songea.   

JESHI la Polisi wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, wanamtafuta binti mwenye umri wa miaka 19 kwa lengo la kutaka kumfikisha kwenye vyombo vya sheria, ili aweze kujibu tuhuma za mauaji ya kichanga na mwili wake kuutumbukiza chooni.

Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Mihayo Msikhela alisema kuwa mtuhumiwa huyo alifanya unyama huo juzi na kutokomea kusikojulikana.

Msikhela alimtaja mtuhumiwa aliyefanya kitendo hicho kuwa ni, Germana Ndimbo mkazi wa kijiji cha Mkumbi kata ya Mkumbi wilayani humo ambapo alikuwa mjamzito na mara alipofanikiwa kujifungua, alichukua jukumu la kufanya unyama huo.

Sunday, July 5, 2015

WAJAWAZITO WAJIFUNGULIA MWANGA WA TOCHI YA SIMU

Kamanda wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) wilayani Nyasa mkoa wa Ruvuma, akihutubia wananchi wa kata ya Linga wilayani humo hivi karibuni.
Na Kassian Nyandindi,
Nyasa.

AKINA mama wajawazito wanaopatiwa matibabu katika kituo cha afya Litumba kuhamba kata ya Linga, wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma wanapata shida wakati wa kujifungua nyakati za usiku, kutokana na kukosa nishati ya mwanga.

Kufuatia hali hiyo wauguzi wa kituo hicho cha afya, wanalazimika kutumia tochi za mwanga wa simu pale mama mjamzito, anapofikia hatua ya kutaka kujifungua.

Hayo yalisemwa na Muuguzi wa kituo hicho, Witness Mtende mbele ya Kamanda wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) wilayani humo, Cassian Njowoka alipokuwa ametembelea kituo hicho kwa ajili ya kukabidhi msaada wa vifaa vya mfumo wa nishati ya umeme wa jua (Solar).

Mtende alisema pia wanakabiliwa na tatizo la ukosefu wa maji, nyumba za kuishi wahudumu wa afya hivyo wanaiomba serikali, ifanye jitihada ya kumaliza kero hiyo.

BIBIYE AGONGWA NA LORI AFARIKI DUNIA

Na Steven Augustino,
Tunduru.

MFANYABIASHARA mmoja ambaye ni maarufu kwa kuuza viazi vitamu, katika kitongoji cha Ng’apa kijiji cha Namiungo wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, Bibiye Yasin Mkao (43) amefariki dunia baada ya kugongwa na lori.

Chanzo cha ajali hiyo kimeelezwa kuwa kimetokana na dereva aliyekuwa akiendesha gari lenye namba za usajili, T 442 CBM ambalo ni mali ya kampuni ya kichina Synohdro, inayojenga barabara kwa kiwango cha lami kutoka wilaya ya Tunduru kwenda Mangaka mkoani Mtwara.

Diwani wa kata hiyo, Nurdin Mnolela alisema marehemu huyo aligongwa na lori hilo la kichina aina ya Howo Syno truck ambalo lilikuwa likiendeshwa na dereva, Noel Beda ambaye mpaka sasa ametokomea kusikojulikana.

Monday, June 29, 2015

UVCCM NYASA YAWATAKA WANACHAMA WAKE KUJENGA USHIRIKIANO


Wanachama wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) wilayani Nyasa mkoa wa Ruvuma, wakiwa wamekusanyika pamoja kumsikiliza Kamanda wao wa Umoja huo, Cassian Njowoka.

Kamanda wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma, Cassian Njowoka akiwa na wanachama wake wa umoja huo ambapo mbele yao kuna moja kati ya kikombe ambacho hukitoa zawadi kwa mshindi wa kwanza wa mpira wa miguu katika timu mbalimbali, ambazo huendelea kushindana wilayani humo. Hapo tukio hilo lilifanyika jana katika kata ya Liuli wilayani Nyasa.
Na Kassian Nyandindi,
Nyasa.

ZIARA ya Kamanda wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) wilayani Nyasa mkoa wa Ruvuma, imeendelea kung’ara na kushika kasi katika maeneo mbalimbali wilayani humo, kufuatia wanachama wa umoja huo kujitokeza kwa wingi katika kila eneo la mapokezi yanapofanyika.

Njowoka ambaye anaendelea na ziara yake ya kikazi wilayani humo, ikilenga kutembelea timu za mpira wa miguu na ambazo zinashiriki ligi kuu ya UVCCM wilayani humo, maarufu kwa jina la Njowoka Cup pamoja na kuongea na wanachama wa umoja huo.

Washiriki wa ligi hiyo amekuwa akiwapatia zawadi ya vifaa vya michezo kama vile kikombe kimoja cha ushindi, jezi seti tatu na mpira mmoja kwa mshindi wa kwanza, jezi seti mbili na mpira mmoja kwa mshindi wa pili na seti moja ya jezi kwa mshindi wa tatu.
Haya yote yanajiri kufuatia ahadi yake aliyoitoa hivi karibuni katika zoezi lake la kuwasimika makamanda wa UVCCM kwa kila kata za wilaya hiyo.

NJOWOKA AENDELEA KUFUNIKA NYASA

Kamanda wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) wilayani Nyasa mkoa wa Ruvuma, Cassian Njowoka akipokelewa kwa shangwe na wanachama wa umoja huo kijiji cha Songambele kata ya Kihagara wilayani humo, wakati alipokuwa jana kwenye ziara yake ya kikazi kwa lengo la kuzungumza na wanachama hao.   

Kamanda wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Cassian Njowoka akizungumza jana na wanaumoja huo katika viwanja vya kijiji cha Songambele kata ya Kihagara wilaya ya Nyasa mkoa wa Ruvuma, ambapo aliwataka wanachama wake kupenda kushiriki kikamilifu katika shughuli mbalimbali za kimaendeleo ili waweze kuondokana na umaskini.

Saturday, June 27, 2015

ASHIKILIWA NA POLISI KWA KUMBAKA MLEMAVU

Kamanda wa Polisi mkoani Ruvuma, Mihayo Msikhela.
Na Sreven Augustino,
Songea.

NIRU Nyimbi (42) ambaye ni mkazi wa kitongoji cha Mwombezi kilichopo kijiji cha Chandarua mkoani Ruvuma, anashikiliwa na jeshi la Polisi mkoani humo kwa tuhuma ya kumbaka mlemavu mwenye mtindio wa ubongo.

Kwa mujibu wa taarifa za tukio hilo, mtuhumiwa alinaswa akiwa anafanya unyama huo kijijini humo ambako imeelezwa kwamba, alikwenda kufanya kazi ya kibarua cha kufyatua tofari.

Mihayo Msikhela, Kamanda wa polisi wa mkoa huo aliwaambia waandishi wa habari kuwa mtuhumiwa huyo alifumaniwa na mama mzazi wa binti huyo aliyemtaja kwa jina la, Oresta Ndonde.

Mama huyo alifanikiwa kumkamata mtuhumiwa, baada ya kusikia sauti ya binti yake akiwa analia kutokana na maumivu aliyokuwa akiyapata wakati anafanyiwa unyama huo.

VETA YAJIVUNIA MAFANIKIO YAKE

Na Mwandishi wetu,
Songea.

ZAIDI ya vijana 60 mkoani Ruvuma, ambao hujishughulisha na kazi mbalimbali ya kuwahudumia wateja katika maeneo yao ya kazi, wamepata mafunzo ya kuwaongezea uelewa ambayo yametolewa na Mamlaka ya elimu na mafunzo ya ufundi stadi (VETA) kanda ya nyanda za juu kusini, jambo ambalo litawasaidia kuleta ufanisi mzuri katika majukumu ya kazi zao za kila siku.

Kaimu Mkurugenzi wa VETA nyanda za juu kusini, Suzan Magani alisema mafunzo hayo yatawasaidia vijana hao kukabiliana na changamoto mbalimbali mahali pa kazi, ambapo pia yanawaongezea uwezo wa namna ya kuwakaribisha na kuwahudumia wateja wao.

Magani alisema kuwa Mamlaka hiyo imepewa jukumu la kutoa mafunzo ili kuweza kukidhi mahitaji ya sekta rasmi na isiyo rasmi, kwa lengo la kuwaongezea uwezo wadau waweze kufanya shughuli zao kwa ufanisi na sio kwa kubahatisha, jambo ambalo linaweza kuwarudisha nyuma kiuchumi.

MFUGAJI ASHAMBULIWA NA SIMBA TUNDURU

Na Steven Augustino,
Tunduru.

MFUGAJI mwenye asili ya Mmang’ati, ambaye ametambuliwa kwa jina la Alex Poketi (22) amelazwa katika Hospitali ya wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, baada ya kujeruhiwa vibaya na simba wakati akiwa machungani.

Walioshuhudia tukio hilo, walisema kuwa majeruhi huyo alipatwa na mkasa huo wakati akijitosa kuokoa maisha ya ng’ombe wake ambao walivamiwa na mnyama huyo mkali, kwa lengo la kutaka kuwafanya kitoweo.

Walisema tukio hilo lilitokea katika kijiji cha Mbuyuni kilichopo kando kando ya mto Ruvuma, eneo ambalo wafugaji hao wamekuwa wakichungia mifugo yao tangu mwaka 2007.

Katika eneo hilo imeelezwa kuwa, simba huyo alijitokeza ghafla na kuanza kushambulia ng’ombe hao aliokuwa akiwachunga ambapo Alex alijawa na jazba na kwenda kumrukia simba huyo kwa kumchoma mkuki, jambo ambalo lilimfanya mnyama huyo akimbie.

NYALANDU: VIONGOZI WASIOKUWA NA SIFA NI MIZIGO KWA CHAMA

Na Muhidin Amri,
Songea.

WAZIRI wa maliasili na utalii, Lazaro Nyalandu ambaye pia ni mmoja kati ya makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) hapa nchini ambao wanawania kuteuliwa na chama hicho kugombea nafasi ya urais, amewatahadharisha viongozi na wanachama wa CCM kuwa makini katika uteuzi wa wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi, ili kuepuka kuteua watu wasiokuwa na sifa ambao watakuwa mzigo kwa chama wakati utakapofika wa kuwanadi kwa wananchi.

Nyalandu alisema kuwa CCM imara itajengwa na viongozi imara waliopo madarakani, kwa kuzingatia hekima na kusimamia vizuri misingi ya haki na ukweli na kwamba pasipo kufanya hivyo wanaweza kukipeleka chama kubaya na kusababisha baadhi ya wanachama, kushindwa kukiamini tena.

Waziri huyo aliyasema hayo wakati alipokuwa akizungumza na baadhi ya wanachama wa Chama Cha Mapinduzi mkoani Ruvuma, mara baada ya kukamilisha zoezi la kuwapata wadhamini kwa nafasi hiyo anayogombea.

Friday, June 26, 2015

NJOWOKA KUMALIZA KERO YA UJENZI ZAHANATI NKALACHI NYASA

Wananchi wa kijiji cha Nkalachi kata ya Liuli wilayani Nyasa mkoa wa Ruvuma, wakiwa wamemzunguka na kumsikiliza kwa makini Kamanda wa Umoja wa Vijana wa Chama cha mapinduzi (UVCCM) wa wilaya hiyo, Cassian Njowoka wakati alipokuwa akiwahutubia.
Na Kassian Nyandindi,
Nyasa.

WANANCHI wanaoishi katika kijiji cha Nkalachi kata ya Liuli wilayani Nyasa mkoa wa Ruvuma, wameiomba serikali na wadau mbalimbali wasaidie vifaa vya kiwandani ili waweze kukamilisha ujenzi wa jengo la Zahanati ya kijiji hicho na hatimaye waondokane na kero ya kukosa huduma za matibabu.

Aidha walisema kuwa hivi sasa akina mama wajawazito na watoto wadogo wamekuwa wakifariki dunia, hasa pale wanapokuwa njiani kuelekea Hospitali ya Anglikana iliyopo wilayani humo, ambayo ipo mbali nao kwa ajili ya kutafuta matibabu.

Hayo yalisemwa kwa nyakati tofauti na wakazi wa kijiji hicho, mbele ya Kamanda wa Umoja wa vijana wa chama cha mapinduzi (UVCCM), Cassian Njowoka walipokuwa kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kijijini humo.

TASAF TUNDURU YAWATAKA WANANCHI KUTOA USHIRIKIANO


Baadhi ya Wataalamu kutoka katika kata mbalimbali wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, wakiwa katika semina ya mpango wa TASAF kwa ajili ya kwenda kutoa elimu kwa wananchi vijijini.

Na Steven Augustino,

Tunduru.

WANANCHI wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, wameombwa kutoa ushirikiano wa kutosha juu ya hatua zote zinazotakiwa kutekelezwa pale unapofanyika upembuzi yakinifu katika matatizo yao, hasa yale yanayolenga uhifadhi wa udongo, uvunaji maji, udhibiti makorongo na kuotesha vitalu vya miti.

Aidha wametakiwa kuondokana na dhana potofu ambazo zinaenezwa na watu wasio na nia njema, kwa yale yanayofanywa katika awamu ya tatu ya utekelezaji wa mpango wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) wakiwa na lengo la kutaka kukwamisha maendeleo ya mpango huo, ili usiweze kuleta mafanikio katika jamii wilayani humo.

Hayo yalisemwa na Peter Lwanda ambaye ni mmoja kati ya watendaji wa mfuko huo, alipokuwa akimwakilisha Mkurugenzi mtendaji wa TASAF hapa nchini, Ladislaus Mwamanga akitoa maelezo ya kuutambulisha juu ya kutoa ajira za muda, kupitia mpango wa kunusuru kaya maskini kwenye kikao cha kazi kilichofanyika ukumbi wa Klasta ya walimu tarafa ya mlingoti mjini hapa.

Tuesday, June 23, 2015

NCHIMBI ATANGAZA RASMI KUTOGOMBEA JIMBO LA SONGEA MJINI

Dokta Emmanuel Nchimbi, Mbunge wa CCM jimbo la Songea mjini mkoani Ruvuma.
Na Julius Konala,
Songea.

BAADHI ya wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Wananchi wa jimbo la Songea mjini mkoani Ruvuma, wamejikuta wakiangua kilio baada ya Mbunge wa jimbo hilo, Dokta Emmanuel Nchimbi kuwatamkia rasmi kuwa hatagombea tena nafasi ya kiti cha ubunge katika jimbo hilo. 

Tukio hilo lilitokea wakati Mbunge huyo, alipokuwa akizungumza na viongozi na wanachama mbalimbali wa CCM kuanzia ngazi ya mashina hadi kata, kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika uwanja wa Majimaji mjini hapa.

Dokta Nchimbi aliwaambia wanachama hao kuwa ameamua kuachia jimbo hilo, baada ya kulitumikia kwa kipindi cha miaka kumi jambo ambalo wanachama hao wa chama tawala, walilipokea kwa mshituko mkubwa.