|
Rais Jakaya Kikwete akimtaka hali Absalom Kibanda, hospitali ya Muhimbili Jijini Dar es Salaam ambako alilazwa baada ya kuumizwa vibaya hivi karibuni. |
UTANGULIZI:
Usiku wa Jumanne ya Machi 5 kuamkia Machi 6, 2013,
Mhariri Mtendaji wa New Habari (2006) Ltd, ambaye pia Mwenyekiti wa Jukwaa la
Wahariri Tanzania (TEF), Absalom Kibanda alivamiwa na kujeruhiwa vibaya akiwa
nje ya lango la kuingilia nyumbani kwake Mbezi Juu, Dar es Salaam.
Tukio hilo liliishtua na kutikisa taifa kwa kiwango
kikubwa si tu katika tasnia ya habari nchini, bali pia jamii kwa ujumla hasa
baada ya aina ya utekaji, utesaji na usiri uliotumika katika kufanikisha
uhalifu huu kufanana kwa karibu na tukio lilomkuta Mwenyekiti wa Jumuiya ya
Madkatari Tanzania, Dk. Stephen Ulimboka lililotokea karibu miezi tisa kabla ya
tukio la Kibanda yaani, usiku wa Juni 26, 2012.
Ukiacha matukio hayo, miezi sita kabla ya Kibanda
kutekwa na kuteswa Mwandishi Daudi Mwangosi, aliuawa akiwa mikononi mwa vyombo
vya dola Septemba 2, 2012 huko Nyololo, Iringa akiwa kazini.
Tukio la Kibanda limekuwa na sura ya mwendelezo wa
mauaji au utesaji wa wanahabari, hasa ikitiliwa maanani kuwa Mwandishi Issa
Ngumba (45) wa Radio Kwizera aliyekuwa anafanyia kazi zake katika Wilaya ya
Kakonko, Kigoma, Januari mwaka huu, alipigwa risasi na kuuawa katika mazingira
ya kutatanisha.Kama hiyo haitoshi, tukio la kutekwa na kudhuriwa kwa Kibanda
limetokea mwezi mmoja tu baada ya Mwandishi wa Gazeti la Tanzania Daima,
Shaaban Matutu kupigwa risasi na polisi akiwa nyumbani kwake Dar es Salaam kwa
maelezo kuwa kimakosa polisi walidhani Matutu ni jambazi.
Mazingira ya kutekwa na kuumizwa kwa Kibanda yalitia
wasiwasi kuwa upo uwezekano, na dalili zilionyesha kwamba waliofanya kitendo
hicho cha kinyama hawakuwa wezi wala majambazi kutokana na ukweli kwamba licha
ya kuwa na fedha zipatazo shilingi milioni tatu taslimu ndani ya gari, laptop,
simu tatu za gharama (ipad, iphone na Blackberry), watekaji hawa hawakuchukua
chochote baada ya kukamilisha uhalifu wao.Kibanda aliumizwa kwa kiwango
kikubwa.
Alitobolewa jicho la kushoto, akaumizwa vibaya
kichwani kiasi cha kusababisha kuvunjika kwa baadhi ya mifupa ya kichwa.
Aling’olewa meno mawili na kucha mbili, tena bila gazi.
Watekaji hawa, katika unyama wa ajabu kabisa,
walimkata pingiri ya kidole cha pete chini ya kucha na kuondokana nayo.Hali
hiyo iliibua maswali mengi, watu wengi wakajiuliza na kutafuta sababu za
kutekwa na kuumizwa kwa Kibanda kiasi hiki.
Kutokana na kuwapo kwa maelezo mengi yanayotofautiana
kuhusu tukio hilo, ikabidi Jukwaa la Wahariri Tanzania lifanye uamuzi.Katika
kikao cha Machi 8, 2013 Jukwaa la Wahariri Tanzania liliunda TIMU ya watu
watano na kuipa hadidu rejea za kufanya uchunguzi wa kihabari juu ya shambulio
hilo kubaini limetokana na nini.
Timu hiyo iliundwa kufuatia uamuzi wa Jukwaa la
Wahariri kufanya uchunguzi huo na baada ya kukubalika kwa ombi la ruzuku ya
kufanya uchunguzi huo wa kihabari kutoka Mfuko wa Vyombo Vya Habari Tanzania
(TMF).
Ruzuku ya TMF ililenga kiujumla kutumia tukio la
Kibanda kuwa chanzo cha kutengeneza mazingira salama zaidi kwa waandishi na
wahariri na kwamba kiwango cha matukio ya kuteswa, kupigwa na kuuawa kwa
waandishi yanapungua kila mwaka.
Timu hii imefanya kazi usiku na mchana kwa kwa zaidi
ya mwezi. Timu imezungumza na wadau 26. Kati ya hawa yumo Kibanda mwenyewe, mke
wake, ndugu zake, wasaidizi wake, waajiri wake wa zamani na wa sasa, viongozi
wa kisiasa na vyombo vya dola kutafuta ukweli wa jambo hili.
Pia tumesoma matamko na habari zilizochapishwa kwenye
mitandao ya kijamii na magazeti ya kati ya Machi 5, 2012 na Aprili 5, 2012 kwa
nia ya kufanya ulinganishi wa taarifa tulizozipata kutokana na uchunguzi na habari
zilizochapishwa baada ya kutekwa kwake.
Vyombo vya dola akiwamo Waziri mwenye dhamana
walikataa kuhojiwa wakisema kuna tume ya serikali inayofanya kazi hiyo na
kwamba kuhojiwa kungeonyesha kutokuwa na imani na tume hiyo.Leo tunawasilisha
muhtasari wa ripoti hii.