Wednesday, July 31, 2013

MAHAKAMA KUINGILIA KATI MGAWANYO WA MALI MBINGA, MADIWANI WASEMA HAWAKUBALIANI NA MCHAKATO WA UGAWAJI

Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Hussein Ngaga akijibu hoja za madiwani katika kikao kilichoketi leo mjini hapa katika ukumbi wa Jumba la maendeleo, ambapo madiwani hao walisitisha mara moja mgawanyo wa mali kati ya wilaya hiyo na wilaya mpya ya Nyasa, kutokana na kubaini kuna mbinu chafu zimetumika katika mgawanyo huo.

Baadhi ya madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga, wakimsikiliza kwa umakini Mkurugenzi wao wakati alipokuwa akijibu hoja zao za msingi, ambazo ziliwasilishwa katika kikao hicho cha baraza la madiwani kilichoketi leo mjini hapa.                                          (Picha zote na Kassian Nyandindi)


Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida Baraza la Madiwani, Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, limesitisha zoezi la mgawanyo wa mali kati ya wilaya hiyo na wilaya mpya ya Nyasa, kutokana na zoezi hilo kuonekana kuingiliwa na vitendo vinavyoashiria kuwepo kwa upendeleo wa upande mmoja, na wenye kulenga njia za siri na ujanja ujanja.

Aidha usitishaji huo umefuatia Madiwani hao kubaini kuwa aliyekuwa Mkurugenzi wa wilaya ya Mbinga Shaibu Nnunduma, ametumia mbinu za ujanja katika kutengeneza makabidhiano(Handing Over) kwa Mkurugenzi mpya wa wilaya hiyo Hussein Ngaga, ambayo yanalenga asilimia kubwa ya mali zilizopo Mbinga zipelekwe Nyasa.

Hali hiyo imejitokeza leo katika kikao cha baraza hilo kilichoketi kwenye ukumbi wa Jumba la maendeleo uliopo mjini hapa, kikao ambacho ni cha kawaida chenye kulenga kujadili maendeleo mbalimbali ya wilaya hiyo.

Mbunge wa Jimbo la Mbinga, Gaudence Kayombo akichangia hoja katika kikao hicho alisema, endapo uongozi wa wilaya hiyo na mkoa huo kwa ujumla utaendelea kulifumbia macho suala la mgawanyo halali wa mali za halmashauri za wilaya ya Mbinga na Nyasa, baraza la madiwani la wilaya ya Mbinga lipo tayari suala hili kulifikisha mahakamani ili haki iweze kupatikana.

Alisema jambo hili hata yeye binafsi linamsikitisha kwa jinsi lilivyofanyika, hivyo hakubaliani nalo na sasa tayari amekwisha ongea hata na uongozi wa makao makuu ya Tawala za mikoa na serikali za mitaa(TAMISEMI) ili waweze kuja na kulifanyia kazi.

“Kuhusu mgawanyo huu wa mali hata mimi unanisikitisha, nimeongea na mkoa na TAMISEMI wamesema wanakuja kushughulikia suala hili, na kwa kweli nasema jambo hili linaonesha kuna ujanja ujanja umefanyika na sisi kama madiwani wa Mbinga, hatutakubali kuona linaendelea”, alisema Kayombo.

Mbunge huyo alisisitiza akisema, mali hizo ni vyema zigawanywe kwa uwiano ulio sawa, huku akiongeza kuwa pasipo kufanya hivyo itakuwa ni ulafi ambao unadhihirisha wazi kwamba, mtu mmoja anataka kujilimbikizia mali nyingi wakati Mbinga nayo inabidi isonge mbele kimaendeleo.

Monday, July 29, 2013

WAFANYABIASHARA SOKO KUU SONGEA WACHARUKA, WAPINGA MPANGO ULIOWEKWA NA MANISPAA HIYO

Kulia ni Mwenyekiti wa Umoja wa Wafanyabiashara wa Masoko Manispaa ya Songea(UWABIMASO) Karim Matumla, akiwa na Makamu Mwenyekiti wa Uwabimaso Leonard Chiunga wakifuatilia hoja mbalimbali kutoka kwa wanachama wa Uwabimaso.

Wanachama wa Uwabimaso wakifuatilia kwa makini kikao hicho chenye lengo la kupinga ongezeko la kodi la Vibanda vya Soko Kuu, na Kupinga tangazo la Zabuni lililotangazwa hivi karibuni.


   
Na Stephano Mango, 
Songea.
          
WAFANYABIASHARA katika Soko Kuu la Halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, wamepinga ongezeko la pango kwa asilimia 100 na tangazo la Zabuni  la ukodishaji wa vibanda hivyo lililotolewa na halmashauri hiyo hivi karibuni.
Akitoa maazimio ya kikao cha Umoja wa Wafanyabiashara Masoko ya Manispaa ya Songea(UWABIMASO) kilichofanyika mjini hapa kwenye ukumbi wa Saccos ya Walimu Songea vijijini, Mwenyekiti wa Uwabimaso Karim Matumla alisema kuwa wafanyabiashara wamepinga kwa nguvu zote mpango huo ambao waliuita kuwa ni wa kifisadi, ulioletwa na viongozi wa  halmashauri hiyo wa kuongeza kiwango cha kodi kwa asilimia 100 na tangazo hilo la Zabuni.
Matumla alisema kuwa mipango ya halmashauri kuhusu masoko yake haina ushirikishwaji wa pamoja kutoka pande zote mbili, jambo ambalo limekuwa likisababisha wanyabiashara hao na uongozi wa halmashauri hiyo kujenga migogoro mara kwa mara.
Alisema kuwa kwa muda mfupi wamepokea barua mbili zenye malengo tofauti ndani ya kipindi cha mwezi mmoja, hivyo inaleta mashaka kwao na kuwataka viongozi wa halmashauri hiyo kufanya kazi zao kwa weledi ikiwemo ushirikishwaji katika jamii.
Imeelezwa kuwa kitendo cha mkurugenzi kutoheshimu wala kutimiza makubaliano yao yaliyomtaka kuondoa kero wanazopata wafanyabiashara waliopo katika Masoko ya halmashauri hiyo ni kitendo cha dharau kwao.
“ Tulimtaka mkurugenzi katika vikao vyetu kuondoa mashimo na kuboresha mifereji na miundombinu mingine ndani ya masoko, wauza matunda watafutiwe eneo maalumu la biashara zao kwani kwa sasa wanazuia mizigo kuingia ndani na wateja wanapata kero ya kuhudumiwa, unyanyasaji unaofanywa na ofisa masoko uachwe na pia tulimuomba atukutanishe na viongozi wa halmashauri ili tutoe kero zetu, lakini yeye amekaidi”, alisema Matumla.
Alisema kuwa mnamo Mei 22 mwaka huu halmashauri ya Songea ilileta barua Uwabimaso ikitoa taarifa ya ongezeko la kodi ya pango kwa asilimia 80 kulingana na ukubwa wa chumba cha biashara kuanzia Julai 1 mwaka huu, kabla hawajaanza kuitekeleza, Julai 9 mwaka huu waliletewa barua nyingine yenye kutangaza zabuni ya ukodishaji wa vibanda hivyo, baada ya Uwabimaso kupinga ongezeko la pango la asilimia 80.
Vilevile kumekuwepo na mgongano wa kimaagizo kutoka katika Ofisi ya mkurugenzi wa halmashauri hiyo, kitendo ambacho kinaibua maswali mengi, hivyo Uwabimaso imeamua kwenda kwa Mwanasheria ili aweke zuio la mpango wa upandishaji wa kodi na utangazaji wa zabuni yenye lengo la kuwaondoa wafanyabiashara wote wa maduka katika soko hilo.
Akizungumza na Mwandishi wetu kwa njia ya simu mkurugenzi wa Manispaa hiyo Zakaria Nachoa alisema, halmashauri imekusudia kuongeza mapato yake kupitia miradi yake, hivyo mfanyabiashara ambaye hataki kuendana na utaratibu huo aache kibanda ili mfanyabiashara mwingine achukue, na baadaye alikata simu.

Wednesday, July 24, 2013

CHAMA CHA WALIMU MBINGA MKOANI RUVUMA, CHATUPIWA MFUPA ULIOMSHINDA FISI

Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu.





















Na Mwandishi wetu,

Mbinga.

VURUGU na migogoro ya hapa na pale inayoondelea kudaiwa kufanywa na baadhi ya vigogo wa Chama Cha walimu Tanzania(CWT) Tawi la Mbinga mkoani Ruvuma, mapya yameibuka juu ya sakata hilo, mtandao huu umeelezwa.

Wadau wa elimu wilayani humo wametoboa siri hiyo nzito kwamba, chanzo cha vurugu na migogoro hiyo, kinatokana na Katibu wao wa CWT wilayani Mbinga Samwel Mhaiki kukosa busara na utulivu katika utendaji wake wa kazi.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Mwandishi wetu, walifafanua kuwa Mhaiki ni mtu wa kupenda kuendekeza migogoro kazini na  tabia hiyo hajaanzia hapa Mbinga, bali tokea alipokuwa akifanya kazi ambako alianzia Ukatibu wake mkoani Mtwara.

Kana kwamba haitoshi, wameeleza kuwa huko alikuwa akiendesha migogoro na migongano kwa watumishi wenzake, wakiwemo hata viongozi wa serikali.

Waliendelea kueleza kuwa baada ya kuonekana Mhaiki ni tatizo na mwiba katika jamii, akahamishiwa wilaya ya Tunduru nako anadaiwa kuendeleza malumbano hayo, na hata kufikia hatua ya kukosa maelewano na viongozi wa wilaya hiyo.

“Kufuatia hali hiyo na mambo mengine yasiyoelezeka, chama cha walimu kilichukua jukumu la kumhamishia hapa Mbinga, hivyo yanayoendelea leo hapa wilayani ni mwendelezo wa historia yake na sasa inadaiwa kaungana na Katibu wake wa mkoa kuendeleza malumbano haya”, alisema Mwalimu mmoja ambaye hakutaka jina lake litajwe.

Kadhalika Wadau hao wa elimu wilayani humo wameeonesha masikitiko yao juu ya migogoro hiyo wakisema, tabia hii haifai kuigwa katika jamii kwa kile walichoeleza kuwa maendeleo katika sekta ya elimu hususani kwa shule za msingi wilayani hapa, yanaweza kurudi nyuma endapo vitendo hivyo vitaendelea kufumbiwa macho.

RODNEY NDUNGURU, SHUJAA ALIYEFIA DARFUR AZIKWA KWAO SONGEA MKOANI RUVUMA


 Asikari wa JWTZ, wakiwa wamebeba mwili wa Rodney Ndunguru.
 
Aliyekaa katikati ni mama wa marehemu Rodney Ndunguru.
 
 Askari wakiwa wamebeba mwili wa marehemu Rodney Ndunguru, wakati wakielekea  katika makaburi ya Mjimwema mjini Songea.
 
 Umati wa watu uliojitokeza katika mazishi ya Rodney Ndunguru katika makaburi ya  mjimwema jana.
 
 
 Mwili wa Rodney Ndunguru ukiingizwa katika kaburi.
 
 Mama wa marehemu Rodney Ndunguru akiweka taji katika kaburi la mwanaye.
 
 
Na Mwandishi wetu,
Songea.


SIMANZI, vilio na majonzi  vimetawala wakati wa mazishi ya askari wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) Rodney Ndunguru wa kikosi cha makomando cha 92 KJ Ngerengere mkoani Morogoro, ambapo mamia ya wakazi wa mkoa wa Ruvuma, wakiwemo askari wa Jeshi la wananchi ambao walihudhuria mazishi hayo yaliyofanyika jana kwenye makaburi ya Mjimwema Manispaa ya Songea.

Katika mazishi hayo ambayo yaliongozwa na Paroko wa kanisa katoliki jimbo kuu la Songea parokia ya Mjimwema padre Noel Duwe, ambaye wakati  akiendesha ibada ya mazishi aliwaonya Watanzania kutochezea amani  na kwamba utulivu walionao watanzania unahitajika kulindwa kwa namna ya aina yeyote na sio vinginevyo.

Padre Due alisema kuwa kwa wale wote wanaotaka kuchezea amani na utulivu tulionao sasa, wanapaswa kukemewa kwa nguvu zote kwa kuwa watanzania hatujazoea vurugu wala umwagaji wa damu jambo ambalo lilionekana kuvuta hisia kwa watu waliofika kuomboleza msiba huo.

Aidha Padri Due alimfagilia Waziri mkuu wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mizengo Pinda kwa kauli yake aliyoitoa Bungeni kuwa jeshi la Polisi lihakikishe linawadhibiti watu wanaoleta fujo kwa kupiga na kwamba kauli yenye agizo hilo inapaswa kuungwa mkono kwa nguvu zote, badala ya kuibeza kwa kuwa hivi sasa watu wengi wamekuwa wakidharau vyombo vya Dola  wakidhani kwamba serikali haipo.
 
Kwa upande wake  Kaimu wa Brigedi ya kanda ya Kusini Kanarli George Msongole alieleza kuwa taarifa ya kifo cha Rodney, ilipokelewa muda mfupi baada ya kifo chake na kuwa Jeshi la wananachi linaungana  na familia ya marehemu katika majonzi na msiba huo mzito.

Kwa upande wake msemaji wa familia ya Marehemu Rodney Ndunguru alisema kuwa  familia imepata pengo kubwa kwa kuondokewa na kijana wao ,na ameiomba serikali kuangalia uwezekano wa kuisaidia  ili waweze kujengewa nyumba ambayo itwasaidia kwa kuishi mama yake mzazi na mjane.
 
Alisema kuwa Rodney Ndunguru amefariki akiwa na miaka takribani miaka saba kazini na akiwa na umri wa miaka 28 ambapo kimsingi kifo chake kimeacha pengo kubwa katika famila kwani katika uhai wake ilikuwa farja kwa ndugu na jamaa.
 
Rodney Ndungu amezikwa saa 10:45 jioni kwenye makaburi ya Mjimwema ambako mamia ya wakazi ya mkoa wa Ruvuma, walihudhulia akiwemo mwakilishi wa mkuu wa mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu ambaye ni Katibu tawala wilaya ya songea Joseph Kapinga na kwamba mazishi yaliendeshwa kijeshi ambapo askari wote walikuwa wamevaa sare huku wakifunga vitambaa vyeusi kwenye mikono yao. 
(habari kwa hisani ya demashonews.blogspot.com)
 

Tuesday, July 23, 2013

UWANJA WA MAONI: CWT MBINGA TUMEPOTEZA MWELEKEO NA MALENGO YA CHAMA TUSIHANGAIKE KUZIBA JUA KWA UNGO

Mwenyekiti wa CWT Taifa, Grattian Mukoba.

 

















Na Kassian Nyandindi,

VIONGOZI wa Chama Cha Walimu Tanzania (CWT) tawi la Mbinga mkoani Ruvuma, wanalalamikiwa na walimu ambao ni wanachama wa chama hicho wilayani humo, kwa kutowalipa fedha za marejesho ya asilimia 15 kutoka kwenye makato ya mishahara yao.

Nionavyo kwa hakika hii ni dharau na dhuluma ni vyema sasa wahusika wachukuliwe hatua kwa kutotimiza wajibu wao ipasavyo kwa wanachama hao.

Nahoji, Katibu wa CWT na Mwenyekiti wako mnafanya nini, hizi fedha mmezipeleka wapi? tunaomba sasa tupate majibu ili tuweze kujiridhisha juu ya malalamiko haya.

Ni malalamiko ambayo sasa yamedumu kwa muda mrefu, wanachama nimezungumza nao baadhi yao kwa nyakati tofauti wanasikitika wakisema wengine ni zaidi ya miezi 24 hadi 30 fedha zao wengi wao bado hawajalipwa.

Hii ni dhambi jasho la mtu huwa halipotei bure ni vyema sasa tukawa wastaarabu kwa kuchukua hatua mapema, katika kunusuru hali hii ambayo mbele tunaweza tukatengeneza shimo la kutumaliza wenyewe.

Uongozi wa namna hii haufai katika jamii, kila kukicha wanachama wamekuwa wakikinyoshea kidole CWT Mbinga, ni dhahiri sasa tunaonesha udhaifu katika utendaji wetu wa kazi, yatupasa sasa tubadilike !

Zama za watu kudanganywa na kupigwa danadana zimepitwa na wakati, kwa hili la marejesho ya makato ya mishahara ya walimu ni vyema tukae mezani na kulifanyia kazi haraka.

Nimeambiwa na wanachama wengi kwamba endapo suala hili litaendelea kuwa sugu, wametishia kujitoa uanachama, nasema endapo itakuwa hivyo hili litakuwa ni pigo kubwa kwa uongozi wa chama cha walimu Mbinga, na jamii sasa itatucheka na kutuzomea hata tutakapokuwa tukipita barabarani.

Kumekuwa na hata tabia ya kupakana matope na kumchafua ofisa elimu wa wilaya hiyo Mathias Mkali, kuwa anahamasisha walimu wajitoe, nimefanya mahojiano na baadhi ya walimu wanasema wao ni waelewa na wana akili timamu hawawezi kuhamasishwa na mtu mmoja juu ya kujitoa katika chama hicho, bali wanachohitaji ni kulipwa madai yao ya makato ya mishahara yao kila mwezi.

Wengine walisema huyo ofisa elimu tangu amekuja hapa wilayani ameweza kuhakikisha stahili zao za msingi ikiwemo uhamisho, likizo, matibabu na masomoni wamelipwa kwa wakati; tofauti na siku za nyuma walikuwa wakipata shida.

Wengine wamefafanua kwamba Mkali amekuwa ni mtu msikivu pale    wanapokuwa na shida zao za msingi, na amekuwa akihimiza utendaji bora wa kazi mashuleni.

Wanasema leo wanashangaa kuona maneno hayo yanatoka wapi, kwa ujumla viongozi wa CWT Mbinga wamepoteza mwelekeo na malengo ya chama hicho, sasa wanahangaika kuziba jua kwa ungo, ukweli upo bayana tunachohitaji hapa walimu walipwe madai yao ya msingi.

Wahenga walisema, Cheo ni dhamana hivyo hatuna budi kuihudumia jamii iliyotuweka madarakani, kwa misingi ya utawala bora ili tuweze kuondoa malalamiko na mitafaruku isiyokuwa na tija.

Katibu wa CWT uliopo Mbinga, sote tunafahamu ndiyo mtendaji mkuu wa kuliongoza jahazi hili la chama hapa Mbinga, sasa kama matatizo haya yanaendelea kweli tutafika?.....tubadilike.

Yawezekana viongozi wa ngazi ya mkoa na taifa, mmefumbwa macho na uongozi wa CWT wilaya ya Mbinga ! ndio maana hakuna hatua zinazoonesha kuzaa matunda licha ya malalamiko haya kudumu kwa kipindi kirefu sasa. Ama kweli tunaweza kusema ufisadi upo kila kona !
  
Nashauri kilio hiki cha wanachama wa chama hicho hapa wilayani ni vyema kikafanyiwa kazi haraka, ikiwezekana hata viongozi wa ngazi ya juu serikalini ingilieni kati suala hili ili wanachama husika waweze kupata haki zao za msingi, vinginevyo tukiendelea kufumbia macho hatutawatendea haki wanakondoo hawa wa Mbinga, ambao kilio chao kimedumu kwa muda mrefu sasa…….. tuchukue hatua.

Mungu ibariki Mbinga na Tanzania kwa ujumla,   

Mwandishi wa makala haya anapatikana kwa simu namba 0762578960.

Monday, July 22, 2013

WANACHAMA WA CWT MBINGA WAUJIA JUU UONGOZI WA WILAYA, WATISHIA KUJITOA UANACHAMA

Katibu wa CWT wilayani Mbinga, Samwel Mhaiki.




















Na Mwandishi wetu,

Mbinga.

KATIKA hali inayoonesha kuwa ni matumizi mabaya ya madaraka na ukiukaji wa taratibu na sheria za utumishi wa umma, Katibu wa Chama Cha Walimu Tanzania(CWT) tawi la Mbinga mkoani Ruvuma, Samwel Mhaiki ananyoshewa kidole na wanachama wa chama hicho wilayani humo, akidaiwa kutowalipa baadhi ya wanachama fedha zao  zinazotokana na asilimia 15 ya makato yatokanayo na mishahara yao ya kila mwezi.

Wamezungumza na mwandishi wetu kwa nyakati tofauti wilayani hapa, wakisema Katibu huyo amekuwa akifanya kitendo hicho, kwa kushirikiana na Mwenyekiti wake wa wilaya hiyo Batson Mpogolo.

Pia wanachama hao wengi wao wametishia kujiondoa uanachama katika umoja huo na kusema wakisha kamilisha mchakato huo wa kujitoa, wapo tayari kwenda kufungua kesi Mahakamani dhidi ya Katibu wao wa wilaya hiyo na Mwenyekiti, ili waweze kulipwa fedha zao wanazodai.

Vilevile viongozi hao wa CWT wamekuwa wakilalamikiwa kwamba, ni zaidi ya miezi 20 sasa walimu wengi waliopo wilayani Mbinga hawajalipwa fedha hizo.

Kadhalika muda mwingi wamekuwa wakionekana wakiwa safarini kuelekea Manispaa ya Songea hususani kwa siku za mapumziko yaani Jumamosi na Jumapili kwa kutumia wakati mwingine gari la chama la wilaya hiyo.

Kitendo hicho cha kusafiri mara kwa mara katika siku za kazi na kwenda huko, walieleza wakidai kuwa wanamashaka na safari zao wanazozifanya na huenda wakawa wanafuja fedha hizo kwa kufanya starehe au kwa manufaa mengine binafsi.

“Hizi safari za mara kwa mara zinatutia mashaka, huenda huko wanakula bata kwa kutumia fedha zetu hizi za makato ya kila mwaka lakini viongozi wetu wa CWT mkoa na taifa wapo kimya wameziba masikio hakuna hatua iliyochukuliwa licha ya sisi wanachama kulalamika kwa muda mrefu”, walisema.

BREAKING NEWS: PADRE WA KANISA KATOLIKI PERAMIHO SEMINARI JIMBO LA SONGEA, ABURUTWA MAHAKAMANI KWA KUMPATIA HONGO MKUU WA WILAYA YA MBINGA

Padre Xavery Kazimoto Komba  wa Peramiho Seminari jimbo la Songea, akiwa amegeuza mgongo kwa lengo la kuficha sura yake, wakati Waandishi wa habari wakimpiga picha alipokuwa eneo la Mahakama ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, akisubiri kusomewa mashtaka yake.(Picha na Kassian Nyandindi)


Na Kassian Nyandindi,

Mbinga.

MAPYA yameibuka juu ya sakata la Padre mmoja wa Kanisa Katoliki hapa nchini, Peramiho Seminari jimbo la Songea mkoani Ruvuma, Xavery Kazimoto Komba ambaye alikamatwa na kuwekwa mahabusu, leo amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya wilaya ya Mbinga mkoani humo, kwa tuhuma ya kutoa hongo ya shilingi milioni 1 kwa Mkuu wa wilaya hiyo Senyi Ngaga, kwa lengo la kumshawishi asichukuliwe hatua kwa makosa aliyofanya ya kuwatapeli baadhi ya wakulima wa kahawa wilayani humo.

Padre huyo anatuhumiwa kufanya utapeli huo kwa kutumia kampuni yake ambayo hujishughulisha na kununua kahawa, inayofahamika kwa jina la Songea network Company Limited ambayo yeye ndiye Mkurugenzi wa kampuni hiyo.

Inadaiwa kuwa Kasisi huyo wa kanisa Katoliki alikamatwa na kuswekwa mahabusu katika Kituo kikuu cha Polisi wilayani humo, mapema Julai 19 mwaka huu majira ya mchana, kufuatia kutoa hongo ya fedha hizo kwa kutumia utaratibu wa M – pesa kwenda namba ya simu ya Mkuu wa wilaya hiyo ambazo mahakamani hapo hazikutajwa.

Ilidaiwa Mahakamani hapo na Mwendesha mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(TAKUKURU) mkoani Ruvuma, Bi. Maria Mwakatobe mbele ya Hakimu mkazi mfawidhi wa wilaya ya Mbinga, Geofrey Mhini kuwa Xavery Kazimoto Komba anadaiwa kufanya kosa hilo Mei 20 mwaka huu na Mei 26 mwaka huu katika majira tofauti.

Mwakatobe aliendelea kudai kwamba Padre huyo anatuhumiwa mnamo Mei 20 mwaka huu alituma kiasi cha shilingi 400,000 na Mei 26 mwaka huu alituma tena shilingi 600,000 kwenda namba ya simu ya Mkuu wa wilaya ya Mbinga Senyi Ngaga, akiwa na lengo la kumshawishi mkuu wa wilaya hiyo asimchukulie hatua kufuatia shauri ambalo lilikuwa kisheria katika ofisi yake.

PADRE WA KANISA KATOLIKI SEMINARI PERAMIHO JIMBO LA SONGEA ASWEKWA MAHABUSU KWA TUHUMA ZA UTAPELI

IGP Said Mwema.


















Na Kassian Nyandindi,

Mbinga.

PADRE wa Kanisa Katoliki Xavery Kazimoto Komba, amekamatwa na kuwekwa mahabusu katika kituo kikuu cha polisi wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, kwa tuhuma ya kuwatapeli wakulima kahawa yenye thamani ya shilingi milioni 95.

Habari zinaeleza kuwa mchungaji huyo ambaye ni wa Seminari kuu Peramiho jimbo la Songea, amesota mahabusu kwa siku tatu ambapo anadaiwa kuchukua kahawa ya wakulima hao na kutokomea nayo kusikojulikana.

Komba anatuhumiwa kukusanya kahawa kilo 25,000 yenye thamani ya fedha hizo, katika vikundi vitano vya wakulima, msimu wa mavuno wa mwaka 2012 na 2013 kwa lengo la kwenda kuuza na baadaye aweze kurejesha malipo halali ya wakulima hao.

Vikundi ambavyo alikusanya kahawa na kutokomea nayo bila kurejesha malipo yao ni Lutondo, Muungano Lituru, Jaribio Lunoro, kipando na Otmary vilivyopo wilayani Mbinga.