Na Muhidin Amri,
Songea.
WAZIRI wa nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, sera, uratibu, bunge na
walemavu Jenister Mhagama amesema serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na
Dokta John Magufuli imefanikiwa kurudisha heshima ya nchi, ambayo awali
ilipoteza matumaini kwa wananchi wake.
Jenister ambaye pia ni mbunge wa Jimbo la Peramiho mkoani
Ruvuma, alitoa kauli hiyo hivi karibuni katika kijiji cha Lundusi wilaya ya Songea
mkoani humo wakati alipokuwa akizungumza na wananchi wa kijiji hicho katika
eneo la ujenzi wa ofisi ya makao makuu ya halmashauri ya wilaya hiyo.
Alisema kuwa wananchi wa jimbo hilo wanahitaji mabadiliko makubwa
ya kimaendeleo hivyo viongozi waliopewa dhamana wanapaswa kuongeza jitihada na uwajibikaji
katika maeneo yao ya kazi ili kuweza kuleta ufanisi kwa faida ya sasa na
baadaye.
Pamoja na mambo mengine Waziri huyo alifafanua kuwa baada ya
serikali kufuta ada na michango mbalimbali kwa wanafunzi wa shule za msingi na
sekondari, atahakikisha watoto wote wenye sifa ya kuanza masomo wanakwenda
shule ili kupunguza tatizo la watu wasiojua kusoma, kuandika na kuhesabu katika jimbo
hilo.
Mbali na hilo, Jenister ameishukuru serikali kutenga fedha za
kutosha kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi ya makao makuu ya halmashauri hiyo, nyumba
ya mkurugenzi na nyumba mbili za wakuu wa idara hatua ambayo itasaidia wananchi
kupata huduma kwa karibu na hivyo kuchochea kuharakisha maendeleo yao na mkoa huo
kwa ujumla.
Aidha ameiomba serikali kupitia shirika la ugavi wa umeme
nchini (TANESCO) kuhakikisha kwamba linapeleka nishati hiyo katika kata ya
Maposeni na baadhi ya maeneo ili kuweza kusaidia kuharakisha maendeleo na
kukaribisha baadhi ya watu kuwekeza miradi ya maendeleo.
Akizungumzia kuhusu kilimo Waziri huyo alisema, wananchi wa
jimbo la Peramiho ndiyo wanaoongoza kwa uzalishaji mkubwa wa chakula
hasa zao maarufu la mahindi ambapo asilimia 50 ya mahindi
yanayolimwa katika mkoa wa Ruvuma yanatoka Peramiho hivyo ni vyema serikali ikaongeza
upatikanaji wa pembejeo za kutosha kwa wakulima wa jimbo hilo.
Pia alieleza kuwa suala la upatikanaji wa pembejeo limeleta
malalamiko mengi kwa serikali, kwani wanaonufaika na mpango huo ni mawakala na
wajanja wachache badala ya wakulima wenyewe, jambo ambalo linarudisha
nyuma mpango wa serikali wa kuleta maendeleo kupitia sekta ya kilimo.
Katika msimu wa mwaka huu imeshauriwa kwamba Wizara ya
kilimo inapaswa kuangalia upya suala la kuwatumia mawakala kununua
mahindi ya wakulima kwa bei ndogo ya shilingi 120 mpaka 200 kwa kilo, huku wao huiuzia
serikali kwa bei kubwa ya shilingi 500 kwani haileti usawa kwa wakulima ambao
ndiyo walengwa wakubwa na mawakala hao wanaotumia mgongo wa
watu wengine kujinufaisha.
Tayari serikali kupitia Ofisi ya Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa imeshapiga marufuku kwa Wakala wa hifadhi ya chakula hapa
nchini (NFRA) kuwatumia mawakala kwenda vijijini kununua mahindi kwa wakulima, badala
yake serikali ndiyo itakayonunua mahindi hayo na kuiagiza
NFRA kufungua vituo vya ununuzi katika maeneo yanayozalisha kwa
wingi zao hilo na kununua kwa bei ambayo itapangwa na serikali.
No comments:
Post a Comment