Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
MKUU wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Senyi Ngaga amelitaka
Baraza la Usimamizi wa Mazingira ya Taifa (NEMC) kuchukua hatua za haraka dhidi
ya tatizo la uchafuzi wa mazingira, ambalo linaendelea kufanyika katika mgodi
wa makaa ya mawe Ngaka uliopo kijiji cha Ntunduaro kata ya Ruanda mkoani humo.
Aidha alifafanua kuwa kampuni ya Tancoal Energy, ambayo ndiyo
imepewa dhamana ya uchimbaji wa makaa hayo, licha ya kupewa maelekezo na NEMC mara
kwa mara namna ya utunzaji wa mazingira ikiwemo kudhibiti maji taka yasiweze
kuingia kwenye mto ambao hutumika kwa shughuli za kibinadamu na wananchi wa
kata hiyo, bado wamekuwa wakipuuza na hawazingatii maelekezo husika waliyopewa.
“Jambo hili limekuwa likijirudia mara kwa mara, nitawasiliana
na watu wa baraza la mazingira kuona ni namna gani hatua zichukuliwe juu ya
tatizo hili, ambalo uharibifu wa mazingira bado unaendelea”, alisema Ngaga.
Ngaga alisema hayo alipokuwa kwenye kikao maalumu, katika kata
ya Ruanda na uongozi wa kampuni ya Tancoal Energy wakiwemo na baadhi ya
wananchi wa kata hiyo wakijadili juu ya athari mbalimbali, zitokanazo na shughuli
za mgodi ambazo zinaendelea kufanyika na kuathiri jamii.
Kadhalika Mkuu huyo wa wilaya ya Mbinga alibainisha kuwa
kampuni hiyo inayozalisha makaa ya mawe, imeshindwa kubuni mbinu mbadala ya
kuweza kuzuia maji taka ambayo yamechanganyika na chembe chembe za mkaa huo
yasiingie kwenye mto Nyamabeva ambao upo katika kata hiyo, jambo ambalo pia ni
hatari kwa afya ya jamii inayozunguka katika eneo hilo ambao hutegemea maji
hayo.
Vilevile kufuatia hali hiyo, Ngaga ametoa agizo kwa uongozi
wa Tancoal Energy kuhakikisha kwamba wanazingatia juu ya suala la upimaji ubora
wa maji mara mbili kwa mwaka na sio mara moja kama wanavyofanya sasa, ambayo
wananchi huyatumia katika shughuli zao za kibinadamu ili kuweza kujua yana
madhara gani na hatua husika ziweze kuchukuliwa katika kunusuru hali hiyo.
Alisema kuwa amekuwa akipokea malalamiko mengi kutoka kwa wananchi
wa kata ya Ruanda kwamba, hata magari yanayosafirisha mkaa huo hayafunikwi
maturubai ipasavyo ili kuweza kuzuia vumbi la mkaa lisiweze kuleta madhara kwa wananchi.
Pamoja na mambo mengine, awali alipokuwa akichangia hoja katika
kikao hicho juu ya malalamiko hayo, Diwani wa kata ya Ruanda kupitia tiketi ya
Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Edimund Nditi alisisitiza kuwa
umefika wakati sasa jambo hilo halipaswi kufumbiwa macho hivyo kuna kila sababu
kwa mamlaka husika kuchukua hatua, ili kuweza kudhibiti hali hiyo na kuzuia madhara
makubwa yanayoweza kutokea hapo baadaye.
Nditi alifafanua kuwa nyakati za masika kumekuwa na tatizo
kubwa katika mgodi huo, hasa pale mvua zinaponyesha maji yanayotiririka kutoka
kwenye mashimo ya mgodi husafirisha kiasi kikubwa cha sumu ya mkaa wa mawe na
kuingia kwenye visima vya asili ambavyo wananchi hutegemea maji yake kuendeshea
maisha yao.
Naye Asteria Mahundi ambaye ni mkazi wa kijiji cha Ntunduaro
aliongeza kuwa maji yote wanayotumia katika kijiji hicho sio salama kwa afya ya
binadamu, ambapo alieleza kuwa wakisha ya chota kutoka kwenye visima hivyo na
kuyafikisha nyumbani baada ya muda mfupi yanapo tuama, huwa na rangi nyeusi
huku juu yake yakiwa yametanda chembe chembe za mkaa wa mawe.
Pia Mwenyekiti wa kijiji cha Ruanda, Deograthias Haulle
alimweleza Mkuu wa wilaya ya Mbinga, Ngaga kwamba ufanyike utaratibu kwa
kampuni hiyo ya makaa ya mawe itoe mchango wake kwa wananchi kwa kuwajengea
miundo mbinu ya bomba la maji safi na salama ili wasiweze kuathirika afya zao.
Kikao hicho kimefanyika kufuatia agizo lililotolewa na Waziri
wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo alipokuwa katika ziara yake ya
kikazi Januari 12 mwaka huu hapa mkoani Ruvuma, alipotembelea mgodi huo na
kujionea changamoto mbalimbali.
Hata hivyo Profesa Muhongo aliagiza kwa kumtaka Mkuu wa
wilaya ya Mbinga, Ngaga akae na menejimenti ya kampuni hiyo inayozalisha mkaa
wa mawe katika mgodi wa Ngaka, wakiwemo baadhi ya wananchi na uongozi wa kata
hiyo ili waweze kujadili changamoto zilizopo mbele yao na kuzifikisha ngazi ya
juu serikalini ili ziweze kufanyiwa kazi.
No comments:
Post a Comment