Na Julius Konala,
Songea.
IMEELEZWA kuwa ujenzi wa Kiwanda cha kusaga nafaka katika
mtaa wa Namiholo kata ya Peramiho wilaya ya Songea mkoani Ruvuma, utagharimu zaidi
ya shilingi milioni 300 hadi kukamilika kwake na kusaidia kupunguza tatizo la
ukosefu wa soko la kuuzia mahindi, kwa wakulima wa vijiji vinavyozunguka eneo
la mradi huo.
Hayo yalisemwa na msimamizi wa mradi huo, Fredrick Lunje alipokuwa
akizungumza na mwandishi wetu mara baada ya kutembelea eneo la mradi kwa ajili
ya kujionea shughuli mbalimbali za ujenzi, ambazo zinaendelea katika mji huo
mdogo wa Peramiho.
Lunje alisema kuwa ujenzi wa kiwanda hicho upo katika hatua
za mwisho, kwa madai kwamba vifaa vyote vya ujenzi vimekamilika na kwamba
kinachosubiriwa ni mafundi wa kufunga mashine hiyo kutoka Afrika ya
kusini, ili ifikapo mwezi Mei mwaka huu kianze kufanya kazi.
Alisema kuwa kukamilika kwa ujenzi wa kiwanda hicho, pia
kutasaidia kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana linaloikabili
serikali pamoja na kuchangia pato la taifa kwa kulipa kodi, itakayoelekezwa kwa
ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Kiwanda hicho kitakuwa kinatoa huduma ya kusaga sembe aina
mbili, ikiwemo yenye kiini na isiyokuwa na kiini ambapo wanatarajia
kusambaza ndani na nje ya mkoa wa Ruvuma, huku akiongeza kuwa mashine hiyo
ikifungwa itakuwa na uwezo wa kusaga gunia kumi kwa saa moja.
Aidha ameiomba serikali kutoa ushirikiano kwa wawekezaji
wazawa, hasa katika suala la kusaidia kupata mikopo ya fedha, kwa ajili ya
kuendeshea shughuli zao badala ya kuwathamini wawekezaji wa nje peke yake.
Kwa upande wao baadhi ya wakulima wa vijiji vya Peramiho, wamempongeza
mwekezaji huyo kwa jitihada zake za kuanzisha mradi huo ambapo walieleza kuwa
utakuwa ni mkombozi mkubwa kwao, kwa kuwatatulia tatizo la ukosefu wa soko la
kuuzia mahindi yao lililokuwa likiwakabili kwa muda mrefu.
No comments:
Post a Comment