Na Kassian
Nyandindi,
Songea.
KITENDO cha kusitisha zoezi la Wazazi kuchangia chakula, kwa
shule za sekondari za kutwa za serikali zilizopo katika Manispaa ya Songea
mkoani humo baadhi ya Wakuu wa shule hizo wamesema kwamba, ni ukiukwaji wa
maagizo yaliyotolewa na serikali kupitia mwongozo wake uliosambazwa katika mikoa
yote hapa nchini.
Aidha kufuatia hali hiyo shule hizo ambazo sasa zimefunguliwa
na kuanza muhula wa masomo Januari 11 mwaka huu, nimeshuhudia watoto wakikosa
chakula shuleni huku wakilazimika kuhudhuria vipindi vya masomo darasani bila
kula chakula, kuanzia majira ya asubuhi hadi saa 10:00 jioni wanaporejea
majumbani kwao.
Ukiukwaji huo wa agizo la serikali, wanasema kuwa unathibitisha
kufuatia mwongozo uliotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Novemba 23 mwaka jana (nakala tunayo) wenye kumbu
kumbu namba DC. 297/507/01/146 katika kipengele cha 4 ukielekeza kwamba
majukumu ya mzazi ni pamoja na kuhakikisha kwamba huduma ya chakula kwa
wanafunzi wa kutwa anachangia, yakiwemo na mahitaji mengine ya kibinadamu kama
vile sare za shule na michezo, matibabu, vifaa vya kujifunzia ikiwemo daftari
na kalamu.
Vilevile mzazi akiwa sehemu ya mwananchi na jamii
inayozunguka shule husika, atashiriki kikamilifu katika kazi ya ujenzi wa
miundombinu ya shule kwa kuchangia nguvu zao kadri itakavyoamriwa na mkutano
husika wa kijiji, mtaa, kata au tarafa.
Uchunguzi wa mwandishi wetu umebaini kwamba, sera ya elimu na
mafunzo ya mwaka 2014 na ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya
mwaka 2015 hadi 2020 ibara ya 52 (a) imebainisha kwamba serikali itatoa elimu
bure kwa ngazi ya elimu awali, msingi hadi kidato cha nne bila malipo ya ada na
michango mingine ya uendeshaji wa shule kuanzia mwaka wa masomo wa 2016, lakini
haitamki kwamba mzazi asichangie chakula cha mtoto wake shuleni kwa shule hizo
za kutwa.
Serikali kuu na mamlaka za serikali za mitaa zitaendelea
kugharimia uendeshaji wa shule, kwa kutoa ruzuku na fedha ya chakula kwa shule
maalumu za msingi na sekondari za bweni na sio zile za kutwa, kugharimia pia
taaluma, madawati na ukamilishaji ujenzi wa majengo ya shule.
Pia walimu hao wa shule za sekondari za kutwa katika Manispaa
ya Songea nimezungumza nao kwa nyakati tofauti, wameeleza kuwa usitishaji wa
mchango wa chakula kutoka kwa wazazi ni agizo lilitolewa na Ofisa elimu wa sekondari
mkoani humo, Mayasa Hashim kwani wao walikwisha andaa na kufuata utaratibu wa
mzazi kuchangia chakula kadri ya mwongozo huo uliotolewa na Ofisi ya Waziri
Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, kuhusiana na shule hizo hapa nchini
zinavyopaswa kuchangia.
Walisema kuwa kufikia Disemba 21 mwaka jana, wakuu wa shule
za sekondari katika Manispaa hiyo wote waliitwa na kupewa mwongozo huo uliotolewa
na TAMISEMI huku wakisisitizwa kufuata yaliyomo ndani yake.
“Baada ya kupewa tuliambiwa na kusisitizwa tufuate yaliyomo
katika mwongozo huu, wakuu wa shule wote tulifanya hivyo tunachotambua michango
na ada imefutwa lakini chakula kwa shule za kutwa mzazi lazima achangie”, walisema.
Hata hivyo alipohojiwa na waandishi wa habari ofisini kwake,
Ofisa elimu wa shule za sekondari mkoa wa Ruvuma Mayasa Hashim alikiri
kusitisha kwa mchango wa chakula na michango mingine kutoka kwa wazazi, huku
akiongeza kuwa utaratibu mwingine unaandaliwa na tayari wakuu wote wa shule za
sekondari za kutwa katika Manispaa hiyo, wamepewa maelekezo ya kufanya juu ya
suala hilo.
No comments:
Post a Comment