Na Steven Augustino,
Tunduru.
SERIKALI imewataka wataalamu na watumishi wa idara mbalimbali
katika Halmashauri zote nchini, kuondokana na utendaji wa kufanya kazi kwa mazoea
katika utekelezaji wa majukumu ya utumishi wa umma, ili kuweza kufikia
mabadiliko ya kweli yatakayolifanya taifa lisonge mbele.
Aidha watendaji hao wametakiwa kujipima kama wanao uwezo wa
kwenda sambamba na kauli mbiu ya serikali ya awamu ya tano ya ‘Hapa kazi tu’ na
kwamba, kama wapo watakaojiona kuwa hawawezi kuendana na kasi hiyo ya mabadiliko
hayo wajitoe mapema wenyewe.
Hayo yalisemwa na Naibu Waziri wa nchi Ofisi ya Rais Tawala
za Mikoa na Serikali za Mitaa na Utawara Bora, Suleiman Saidi Jafo wakati alipokuwa
akizungumza na watumishi wa idara za halmashauri ya wilaya ya Tunduru mkoani
Ruvuma, katika kikao kilichofanyika ukumbi wa Klasta ya walimu wa tarafa ya Mlingoti
mjini hapa.
Waziri Jafo alisema katika kuleta mabadiliko ya kweli, inatakiwa
kila mtumishi ajipange kufanya kazi kwa juhudi na maarifa kwa kujitoa kwa moyo
wa dhati kwa manufaa ya Watanzania wote.
"Katika kuhakikisha kwamba dhana ya hapa kazi tu
inafanikiwa, kila mfanyakazi katika idara yake afanye kazi kwa uadilifu
na weledi wa hali ya juu vinginevyo mtumishi ambaye hataki kufuata nyayo hizi, hafai
kuendana na kasi ya serikali ya awamu ya tano", alisema Naibu Waziri Jafo.
Vilevile katika hotuba yake pia alikumbushia agizo lake la
kuzitaka halmashauri zote kuhakikisha kwamba zinafunga mfumo wa kielektroniki
tayari kwa ajili ya kuanza ukusanyaji wa mapato, kupitia mfumo huo na kwamba
halmashauri itakayoshindwa kufanikisha zoezi hilo Mkurugenzi wake ajitoe
mwenyewe.
Naibu Waziri huyo aliendelea kusisitiza kuwa lengo la maagizo
hayo ni kukata mirija iliyokuwa imewekwa na wajanja wachache, ambao wamekuwa
wakijinufaisha kupitia utaratibu mbovu wa kukusanya mapato na kwamba utaratibu
wa kukusanya mapato kupitia mfumo huo, utasaidia kuinua mapato ya ndani ili
fedha zitakazokusanywa ziweze kufanya kazi ya kuboresha huduma mbalimbali za
wananchi.
Alisema utaratibu huo wa kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya
ndani, fedha zitakazopatikana zitasaidia kuondoa kero ambazo zimekuwa zikisumbua
halmashauri nyingi hapa nchini, ikiwemo ulipaji wa madeni ya watumishi.
Vilevile Waziri Jafo, aliwashukia wakuu wa idara na kuwataka
kuachana na tabia za ukiritimba usiokuwa wa lazima wa kukwamisha utekelezaji wa
mipango mbalimbali, ambayo imekuwa ikipangwa hadi wahakikishe kuwa wameweka
watu wao ndipo wakubali kupitisha malipo husika.
"Ole wenu wakuu wa idara wababaishaji, kwa sasa ofisi
yangu imeanzisha sera ya mlango wazi na tumegawa namba za simu katika ofisi
zote za Wenyeviti wa hamashauri, manispaa na majiji ili kudhibiti hali hii",
alisema.
Awali Mkuu wa wilaya ya Tunduru, Agnes Hokororo
alimweleza Naibu Waziri huyo kwamba, wilaya yake imejipanga kuhakikisha
inasimamia kikamilifu fedha ambazo wamezipata kwa ajili ya kutekeleza dhana ya
elimu bure kulingana na maelekezo ya serikali ya awamu ya tano.
No comments:
Post a Comment