Na Muhidin Amri,
Songea.
WAZIRI wa afya, maendeleo ya jamii, wazee na watoto Ummy
Mwalimu amewataka wanawake kujiepusha na matumizi ya dawa za asili pindi
wanapokuwa wajawazito, ili waweze kujiepusha na uwezekano wa kupata matatizo mbalimbali
wakati wa kujifungua.
Mwalimu ametoa rai hiyo jana mjini Songea, alipokuwa akizungumza
na madakatari na wauguzi wakati alipotembelea hospitali ya
mkoa Songea, ambapo alijionea uhaba wa vitanda katika wodi namba ya tatu
inayotumiwa na akinamama waliojifungua pamoja na mlundikano wa wagonjwa.
Alisema kuwa sera ya afya serikali awamu ya tano, inalenga
kuboresha huduma za matibabu kwa wananchi wake kwa kuongeza vifaa tiba, wauguzi
na madakatari na kwamba alieleza kuwa ni jambo la kushangaza kuona baadhi ya
watu hadi tunaingia karne hii ya 22 bado wanaendelea kutumia madawa ya
asili kutibu maradhi waliyonayo.
Alibainisha kuwa serikali itaendelea kuboresha huduma zake za
matibabu katika vituo vya afya, zahanati na hospitali zote bhapa nchini, hivyo
ni vyema wananchi wajitokeze kupata huduma za matibabu pale wanapohisi
dalili za homa badala ya kutumia dawa za asili ambazo wakati mwingine zina
madhara makubwa kwa mtumiaji.
Mbali na hilo, amewaasa wananchi kuendelea kujiunga na Mfuko
wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) na wa afya ya jamii (CHF) ili kuwa na uhakika
wa matibabu na kupunguza, matumzi makubwa ya fedha kuliko kuweka fedha nyumbani
au kutembea nazo mifukoni.
Aidha ameuagiza uongozi wa mkoa wa Ruvuma, kuangalia namna
wanavyoweza kupunguza msongamano wa wagonjwa katika hospitali hiyo kwa
kuboresha huduma za matibabu kwenye zahanati, vituo vya afya na kuimarisha
hospitali za wilaya.
“Nawasihi viongozi wa
mkoa wa Ruvuma, mmejionea wenyewe msongamano uliopo katika hospitali zetu angalieni
namna ya kukabiliana na tatizo hili kwa kuboresha huduma katika hospitali zenu
za wilaya, tuweze kuondoka na kero ya mlundikano wa wagonjwa”, alisema Waziri
Mwalimu.
Kwa mujibu wa Waziri huyo ni kwamba, licha ya serikali
kukabiliwa na tatizo la fedha hata hivyo itaendelea kuimarisha huduma za afya
hasa kwa akina mama wajawazito na watoto ili kuwa na vizazi salama na kusaidia
kuokoa maisha ya wanawake wakati wa kujifungua.
Mwalimu amesikitishwa na vitendo vilivyokithiri katika
mkoa huo, vya wanawake kutupa watoto mara baada ya kujifungua ambapo
amewashauri kutumia njia za kisheria kupata haki ya matunzo ya mtoto, kwa
wanaume wanaowapa mimba.
Kutokana na hilo amewaagiza watendaji wa vijiji, mtaa na kata
kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama vilivyopo katika maeneo yao
kuwachukulia hatua wanawake wanaotupa watoto, kwa kuwa kufanya hivyo ni kosa la
jinai.
Alisema kuwa, mkoa wa Ruvuma ni miongoni mwa mikoa
iliyokithiri kwa vitendo vingi vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto, hivyo
ameitaka jamii kuunganisha nguvu ili kupunguza vitendo hivyo ambavyo pia ni
kinyume na maagizo ya mwenyezi Mungu.
No comments:
Post a Comment