Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
WANAFUNZI wanaosoma shule ya msingi Ntunduaro iliyopo katika
kata Ruanda wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, majengo wanayotumia kusomea yapo
katika hali mbaya na huenda yakabomoka wakati wowote kutokana na kujenga nyufa
zinazosababishwa na mtetemeko mkubwa wa ulipuaji wa miamba, kwenye mgodi wa
makaa ya mawe Ngaka uliopo katika kijiji hicho.
Hali ya mazingira ya shule hiyo hivi sasa ni mbaya na kwamba husababishwa
na kuendelea kwa shughuli hizo za ulipuaji wa baruti katika miamba, jambo
ambalo huenda likaleta madhara makubwa katika jamii.
Mkuu wa wilaya ya Mbinga, Senyi Ngaga alisema hayo alipokuwa
kwenye kikao maalumu, katika kata ya Ruanda na uongozi wa kampuni ya Tancoal
Energy ambao ndio wamiliki wa mgodi huo, wakiwemo na baadhi ya wananchi wa kata
hiyo wakijadili juu ya athari mbalimbali zitokanazo na mgodi huo.
Ngaga alisema kuwa ulipuaji wa baruti unaofanywa na kampuni
hiyo unahatarisha usalama wa wananchi wanaoishi jirani na mgodi, hivyo kuna
kila sababu ya kuchukua jitihada ya kunusuru hali hiyo ikiwemo kufanya taratibu
za kuwahamisha kwenda maeneo mengine ili wasiweze kuathirika.
“Ulipuaji huu unafanywa kwa kishindo kikubwa kiasi ambacho hata
majengo ya shule hii na baadhi ya nyumba za wananchi, hutikisika na kujenga
nyufa ambazo baada ya miezi michache mbele endapo hali hii itaendelea kufanyika
huenda zikabomoka”, alisema Ngaga.
Awali akichangia hoja katika kikao hicho, Diwani wa kata ya
Ruanda Edimund Nditi alisema kuwa watoto wanaosoma katika shule hiyo ya msingi
wakati ulipuaji huo unapofanyika, hulazimika kukatisha masomo yao darasani na
hukimbia kutoka nje ya madarasa yao wakihofia majengo wanayotumia kusomea
huenda yakabomoka kutokana na kuwa katika hali mbaya.
Alisema kuwa athari za mazingira hata kwa walimu
wanaofundisha katika shule hiyo ni kubwa, na kwamba serikali inapaswa kuingilia
kati ili kuweza kunusuru hali hiyo.
“Mheshimiwa Mkuu wa wilaya, suala la kuwahamisha hawa wananchi
ni muhimu lifanyike ili kuweza kunusuru makazi na maisha ya watu wanaoishi
katika kijiji hiki, athari za mazingira zitokanazo na shughuli zinazofanywa na
mgodi ni kubwa mno”, alisema Nditi.
John Nyimbo Mwenyekiti wa kijiji cha Ntunduaro alisema kuwa uwekezaji
unaofanywa na kampuni hiyo, hauna tija katika jamii kutokana na hali ya
ulipuaji wa miamba unaofanywa huathiri makazi ya watu.
Naye Kamishina msaidizi wa madini kanda ya ziwa Nyasa mkoani
Ruvuma, Fredy Mahobe alithibitisha juu ya milipuko hiyo na kueleza kuwa
inatokana na uwingi wa baruti zinazoingizwa kwenye miamba mgodini na
kulipuliwa.
Mahobe alifafanua kuwa Tancoal Energy hutumia kiasi cha tani
mbili za ulipuaji, ambacho ni kikubwa na huathiri mazingira ya maisha ya
wananchi wanaozunguka mgodi huo.
Kamishina huyo alieleza kwamba hali hiyo husababisha
mtetemeko kuwa mkubwa na kuwafanya wananchi waishi kwa hofu, kutokana na nyumba
zao kujengwa chini ya kiwango wakihofia kubomoka.
Aidha kikao hicho kimefanyika kufuatia agizo lililotolewa na
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo alipokuwa katika ziara
yake ya kikazi Januari 12 mwaka huu hapa mkoani Ruvuma, alipotembelea mgodi huo
na kujionea changamoto mbalimbali.
Profesa Muhongo aliagiza kwa kumtaka Mkuu wa wilaya ya
Mbinga, Ngaga akae na uongozi kampuni hiyo inayozalisha makaa ya mawe katika
mgodi wa Ngaka wakiwemo baadhi ya wananchi na uongozi wa kata hiyo, ili waweze
kujadili changamoto zilizopo mbele yao na kuzifikisha ngazi ya juu serikalini
ili ziweze kufanyiwa kazi.
No comments:
Post a Comment