Na Bashir Yakub,
HAKIMILIKI katika
masuala ya ardhi, huhusisha umiliki wa ardhi
zenye hati. Umiliki huu hutoa wajibu na haki
fulani kwa mmiliki katika ardhi husika, na sio rahisi kudai
kwamba una hakimiliki katika ardhi kama hauna
hati.
Aidha tumezoea
kuona hati zilizo na jina la mtu mmoja
mmoja. Hii ni hata kwa wanandoa ambao
hudai mali husika zinatokana na jasho lao wote.
Lakini je unajua kuwa inawezekana hati
miliki ikawa na majina ya wanandoa wote
badala ya kuwa na jina la mmoja tu hasa baba ambao
ndio wengi hupenda majina yao yaonekane hapo
?. Jambo hili linawezekana na linaruhusiwa.
1. HAKIMILIKI YA
PAMOJA KUONDOA MGOGORO.
Kutoelewana ambako
mara kadhaa hutokea baada ya kifo cha
mmoja wa wanandoa, kunaweza kuondolewa
na umiliki wa ardhi wa pamoja. Ikiwa una
wasiwasi juu ya mustakabali wa mali
hasa ardhi huko mbele, ni vyema basi
ukachukua hatua ya kusajili kwa umiliki wa
pamoja.
Kama kiwanja / nyumba
ina hati yenye majina mawili, la baba na mama halafu
mmoja wao akafariki itakuwa ni vigumu ndugu
au mwingine yeyote mwenye nia mbaya kudai
umiliki wa kiwanja / nyumba hiyo.
Lakini hali itakuwa
tofauti iwapo hati ina jina la mmoja
na huyo huyo mmoja ndiye aliyefariki. Hivyo pale
pote ambapo ndugu walidhulumu mali za marehemu
hasa ardhi, ni pale ambapo kuna jina la
mmoja.
Mara nyingi fitina
huingia pale penye mwanya wa kufanya hivyo. Sio
rahisi fitina kuingia pasipo na mwanya. Kuweka majina
ya wanandoa wote kwenye hati za ardhi
ni hatua ya kuziba mwanya wa fitina.
Itawezekanaje ndugu au
mwingine mwenye nia ovu kudai umiliki wa ardhi
ya marehemu huku akijua kuwa, hati husika inalo
jina la mke pia. Sio rahisi hata kidogo.
Lakini pia umiliki
wa pamoja huondoa mgogoro pale panapokuwa
na talaka. Swali la kujiuliza je, mwanandoa fulani
amechangia chochote katika kupatikana kwa mali
huwa halipo ikiwa majina yote mawili
ya wanandoa yameonekana kwenye hati.
2. KUMILIKI ARDHI
PAMOJA KATIKA NDOA YA MKE ZAIDI YA
MMOJA.
Suala la kuwa na
hati yenye majina ya wanandoa wote ni pana.
Tunaposema wanandoa wote hatumaanishi mme na mke
mmoja tu, kinachomaanishwa hapa ni kwamba
inawezekana kuwa na hati yenye jina la
mme pamoja wake zake wawe wawili,
watatu n,k.
Kifungu cha 161 ( 1
) cha Sheria namba 4 ya ardhi
kinasema kuwa, pale ambapo mwanandoa anapata
hakimiliki ya ardhi iliyosajiliwa kwa jina
lake na mke wake au wake zake
itajengwa dhana ya kisheria kwamba
wanandoa hao wanamiliki ardhi hiyo kwa
pamoja.
Kifungu kinaonesha wazi
kutambua hakimiliki ya ardhi inayohusisha mitala.
3. KILA MWANANDOA
ATAPEWA HATI YAKE.
Majina ya wanandoa
yanapokuwa yameingizwa yote kwenye hati, basi ni
haki ya kila mwanandoa ambaye jina
lake limeingia kupata nakala yake ya hati.
Kwa hiyo mwanaume atamiliki hati yake
halikadhalika mwanamke au wanawake nao
watamiliki hati yao kila mmoja yake.
Hii ni
tofauti na hati inapokuwa na jina
la mtu mmoja tu ambapo huyo huyo ndiye
humiliki hati hiyo.
4. KUGAWANA ARDHI
INAYOMILIKIWA KWA PAMOJA.
Hati inapokuwa na
majina ya wanandoa wote sio lazima iwe
imeeleza nani anamiliki wapi mpaka wapi. Kutokana
na hilo mmoja wa wanandoa anaweza kuomba
iwekwe mipaka au ijulikane nani
anamiliki nini japo hati ni moja.
Katika kulifikia
hilo maombi maalum inabidi yapelekwe
kwa kamishna wa ardhi kwa ajili ya
kutambulisha nani anamiliki nini katika ardhi
hiyo, liwe jengo, nyumba, shamba au vinginevyo.
Kifungu cha 162 ( 1
) cha sheria ya ardhi kinasema kuwa,
maombi yaliyopo katika fomu maalum
yatawasilishwa kwa msajili kwa ajili ya
kugawa nani anamiliki nini.
Haki ya maombi
haya ni ya mtu yoyote kati ya wale
ambao majina yao yanaonekana kwenye hati.
Hili litafanyika
kwa kuzingatia sheria nyingine kama sheria
ya ndoa ( The law of marriage Act).
MWANDISHI WA
MAKALA HAYA NI MWANASHERIA NA MSHAURI
WA SHERIA KUPITIA GAZETI LA
SERIKALI LA HABARI LEO KILA
JUMANNE, GAZETI JAMHURI KILA JUMANNE NA
GAZETI NIPASHE KILA JUMATANO.
0784482959, 0714047241 bashiryakub@ymail.com
No comments:
Post a Comment