Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
JAMII hapa nchini, imetakiwa kuacha tabia ya kuwatumikisha
watoto wadogo kwa kuwapa ajira ambazo zinawarudisha nyuma kimaendeleo, badala yake
ihakikishe inawapa ulinzi na haki zao za msingi sambamba na kuwapeleka
shule ili waweze kusonga mbele kimaendeleo.
Rai hiyo ilitolewa na Ofisa ustawi wa jamii wilaya ya Mbinga,
Davina Maketta anayeshughulikia kitengo cha watu wenye ulemavu wilayani humo,
alipokuwa akifungua kongamano la kupinga ukatili kwa wanawake na watoto walio chini
ya umri wa miaka mitano, ambalo liliandaliwa na Chama Cha Walemavu Tanzania
(CHAWATA) tawi la Mbinga wilayani humo.
Alifafanua kuwa ni kweli hivi sasa jamii inakabiliwa na wimbi
kubwa la ongezeko la watoto wa mitaani, linalotokana na yenyewe kushindwa
kuwapatia mahitaji muhimu, hata hivyo inatakiwa isitumie nafasi hiyo kuwakandamiza
watoto hao kwa kuona kama ni watu wasiostahili kuishi vizuri kama wenzao.
Mbali na agizo hilo, Maketta amewataka wazazi wilayani humo
kujiepusha kuzaa watoto wengi kwa kuwa huchangia kutowapatia
mahitaji yao ya msingi na matokeo yake wazazi mwisho wa siku, hujikuta
wakielemewa na mzigo mkubwa wa kutunza watoto hao jambo
ambalo pia linasababisha ongezeko la kaya maskini kwa baadhi ya familia zenye
idadi kubwa ya watoto.
Kwa mujibu wa takwimu zilizopo wilayani Mbinga, inakadiriwa
kuwa na watoto zaidi ya 100 wa mitaani wenye umri kuanzia miaka saba hadi
18 wanaoishi katika mazingira magumu, bila ya uangalizi mzuri wa wazazi
wao mbali na wale waliopelekwa katika vituo vya kulelea watoto yatima na
wenye mahitaji maalumu.
Maketa alisema kwamba uzazi wa mpango, unasaidia kupata idadi
ndogo ya watoto ambao wazazi na walezi watakuwa na uwezo wa kuwahudumia kwa
kuwapatia mahitaji ya lazima, lakini hali hiyo ni tofauti kwa
familia zenye watoto wengi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa CHAWATA tawi la Mbinga wilayani
humo, Martin Mbawala ametoa wito kwa jamii kuhakikisha kwamba inasaidia kutoa
uangalizi wa kutosha kwa watoto wanaozagaa hovyo mitaani, badala ya
kuwanyanyapaa na kuwaita majina mabaya ambayo yanasababisha watoto hao mwisho
wa siku, kuathirika kisaikolojia na kuamua kushiriki katika matendo maovu.
Mbawala alieleza kuwa kuna baadhi ya watu wamekuwa ni chanzo
cha kuongezeka kwa watoto wa mitaani, wanapowaona badala ya kuwaita ili
kufahamu chanzo cha tatizo walilonalo huishia kuwapa manyanyaso na kuwaita
majina ambayo hayapendezi hata kidogo kuitwa binadamu.
No comments:
Post a Comment