Na Mwandishi wetu,
Songea.
UCHAGUZI Mkuu wa serikali ya wanafunzi wa chuo kikuu cha Mtakatifu Joseph tawi la Songea mkoani Ruvuma, umeshindwa kufanyika kwa kile kinachodaiwa kuwa uongozi husika wa chuo hicho umekuwa ukiingilia na kutaka kupanga safu ya uongozi wanaoutaka wao, huku wanachuo wakishindwa kuwa huru kuchagua kiongozi wanayemtaka.
UCHAGUZI Mkuu wa serikali ya wanafunzi wa chuo kikuu cha Mtakatifu Joseph tawi la Songea mkoani Ruvuma, umeshindwa kufanyika kwa kile kinachodaiwa kuwa uongozi husika wa chuo hicho umekuwa ukiingilia na kutaka kupanga safu ya uongozi wanaoutaka wao, huku wanachuo wakishindwa kuwa huru kuchagua kiongozi wanayemtaka.
Kufuatia kuwepo kwa hali hiyo, kumesababisha vurugu za hapa
na pale katika eneo hilo la chuo, ambazo zilipelekea mmoja wa viongozi wa chuo
hicho ambaye ni mtawa aliyefahamika kwa jina moja la Magdalena, raia wa kutoka
nchi ya India kunusurika kipigo kutoka kwa wanafunzi wakati alipokuwa akitangaza
uchaguzi huo hautafanyika.
Habari zaidi kutoka kwenye chuo hicho zinaeleza kuwa, mapema
miezi mitatu iliyopita wanafunzi wa chuo hicho walitangaziwa kuwa mwanachuo
yeyote anayetaka uongozi achukue fomu ya kugombea, na hili lilitokana baada ya
uongozi uliokuwa madarakani kuisha muda wake wa utawala.
Wanachuo hao ambao waliomba majina yao yahifadhiwe,
waliwaambia waandishi wa habari kuwa baadaye mchakato wa kuwapata viongozi
uliendelea ambapo wagombea walijitokeza na kuanza kufanya kampeni za kuomba
wachaguliwe kwa nafasi walizoomba.
Waliongeza kuwa siku chache zilizopita baadhi ya majina ya
wagombea yalikatwa na uongozi wa chuo cha Mtakatifu Joseph na kuletwa majina
mengine ya wanachuo ambao hawakuomba kugombea, jambo ambalo lilianza kuleta
mgogoro na vurugu baina ya wanachuo na uongozi wa chuo ambao unatuhumiwa
kuwapangia safu viongozi wanaowataka wao.
Siku ilipowadia ya kufanya uchaguzi Februari tatu mwaka huu,
ndipo mtawa Magdalena aliitisha mkutano wa wanachuo wote na kuwatangazia kuwa
uchaguzi wa serikali ya wanachuo umefutwa hadi pale watakapotangaziwa tena na kwamba
mchakato huo unapaswa kuanza upya, ndipo vurugu hizo zilipoanza kujitokeza.
“Mara baada ya kiongozi huyu kutangaza uchaguzi umefutwa,
wanachuo tulishindwa kujizuia, lengo letu tulitaka tupate ufafanuzi juu ya
sababu za msingi za kufutwa kwa uchaguzi huu”, walisema wanachuo hao.
Walisema kuwa kutokana na kuwepo kwa migogoro ya mara kwa
mara kwenye chuo hicho, baadhi ya wanachuo wameonyesha kusikitishwa kwa
mwenendo mzima wa uongozi husika ambao ndio unadaiwa kuwa chanzo cha migogoro
na wameiomba serikali kuona umuhimu wa kuingilia kati, ili kuweza kumaliza hali
hiyo isiweze kuendelea kujitokeza mara kwa mara.
Pamoja na mambo mengine, wanachuo waliojitokeza kuwania
nafasi mbalimbali za uongozi zilizotangazwa kuwa ni; kwa nafasi ya urais wa
serikali ya wanafunzi alikuwa John Zabron na Jonas Kawelela, makamu wa rais George
Ngao na Veronica Lusagira.
Kadhalika kwa majina mawili ya wagombea yaliyokatwa na
uongozi wa chuo na wanafunzi hao kuanza kuzua tafrani kuwa ni; Jonas Kawelela
ambaye inadaiwa jina lake liliondolewa na uongozi huo kwa madai kuwa alifeli
somo moja na badala yake nafasi hiyo ilichukuliwa na Silvester Joseph, pia kwa
nafasi ya makamu wa rais jina la Veronica Lusagira liliondolewa kwa madai kuwa
tangu alipojiunga na chuo hicho miaka miwili iliyopita alikuwa bado hajasajiliwa.
Wanachuo kadhaa walichukuliwa na jeshi la Polisi mkoani Ruvuma,
kwa lengo la kwenda kuwahoji kufuatia kuwepo kwa vurugu hizo ambazo zilitishia
uvunjifu wa amani katika eneo la chuo hicho.
Kwa upande wake Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Zuberi
Mwombeji ambaye hakutaja majina ya waliohojiwa amethibitisha kutokea kwa tukio
hilo na kueleza kuwa wanachuo hao baadhi yao walikamatwa, walihojiwa na
kuruhusiwa kurudi chuoni kwao ambapo Polisi wamefungua jalada la uchunguzi
kuhusiana na tukio hilo.
Hata hivyo kiongozi mmoja wa chuo hicho, aliyejitambulisha
kwa jina la Dkt. Katayi alipohojiwa kwa njia ya simu juu ya sakata hilo
alieleza kwa kifupi kwamba uchaguzi huo ulisitishwa, kutokana na baadhi ya
wagombea kutotimiza vigezo husika na akaishia kukata simu.
No comments:
Post a Comment