Tuesday, February 9, 2016

WANAFUNZI NAKAPANYA TUNDURU WAISHI KWA HOFU KUTOKANA NA KUSUMBULIWA NA HOMA YA MATUMBO

Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Said Thabit Mwambungu.


Na Steven Chindiye,
Tunduru.

WANAFUNZI wanaosoma katika shule ya Sekondari Nakapanya Wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, wanaishi kwa hofu kutokana na kusumbuliwa na ugonjwa wa homa ya matumbo ambayo imezuka shuleni hapo.

Hayo yalibainishwa na wananafunzi hao, walipokuwa wakizungumza na mwandishi wa habari hizi na kuongeza kuwa, hofu hiyo imetokana na wenzao 56 kuanza kuugua ugonjwa wa kuharisha mfululizo.

Walisema kufuatia mlipuko huo, timu ya wataalamu wa afya kutoka hospitali ya wilaya hiyo ikiongozwa na Kaimu mganga mkuu wa wilaya, Dkt. Bernad Mwamanda walienda huko na kutoa huduma kwa wagonjwa walioathirika ambapo pamoja na mambo mengine, timu hiyo pia ilichukua sampuli kwa ajili ya kwenda kufanyia uchunguzi zaidi ili kuweza kutafuta na kupatikana ufumbuzi wa tatizo hilo.


Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na maofisa tabibu wa kituo cha afya  Nakapanya, ambako wanafunzi hao walienda kupatiwa matibabu walifafanua kwamba wanasumbuliwa na ugonjwa wa Amiba, ambao chanzo chake ni kula au kunywa maji yaliyochanganyika na kinyesi.

Kufuatia kuwepo kwa taarifa  za kuzuka kwa ugonjwa huo, Dkt. Mwamanda alitumia nafasi hiyo kuwaasa wananchi wa wilaya ya Tunduru kujenga mazoea ya kunywa maji yaliyochemshwa, pamoja na kutunza vyanzo vya maji vilivyopo katika maeneo yao ili waweze kujikinga na magonjwa ya mlipuko yanayoweza kujitokeza katika maeneo yao.

Aidha Dkt. Mwamamnda aliwaagiza waganga, mabwana afya, mabibi afya pamoja na Watendaji wa vijiji na kata kwa ujumla wilayahi humo kujenga ushirikiano na wananchi katika maeneo yao, ikiwemo kutoa elimu ya afya ili wakati wote walinde usalama wa afya zao.

Hata hivyo aliongeza kuwa katika utekelezaji wa majukumu hayo, pia wahimize wananchi kuchemsha maji ya kunywa mara kwa mara na kutunza vyanzo hivyo na endapo wasipozingatia hayo, watakuwa katika hatari ya kuugua magonjwa ya homa za matumbo.

No comments: