Na Steven Augustino,
Tunduru.
DEREVA mmoja wa kampuni ya Synohdryo, inayojenga barabara kiwango
cha lami kutoka Tunduru mjini kwenda tarafa ya Nakapanya wilayani humo mkoa wa Ruvuma,
amefariki dunia baada ya kusombwa na maji.
Dereva huyo ambaye hufahamika kwa jina la, Ally Ramadhani
(31) mzaliwa wa mkoa wa Tanga alikumbwa na mkasa huo Februari 25
mwaka huu, majira ya saa 11.30 jioni wakati akiwa anaoga katika eneo la mto
huo.
Taarifa za tukio hilo zinasema kuwa marehemu huyo alienda
kuoga katika mto Muhuwesi, baada ya muda wa kazi kwisha na kwamba aliteleza na
kutumbukia mtoni hatimaye kusombwa na mkondo mkali wa maji na kumpeleka kusikojulikana.
Mashuhuda wa tukio hilo walisema kwamba baada ya kuanguka na
kutumbukia mtoni, marehemu alisikika akiomba msaada wa kuokolewa lakini kutokana
na wenzake walikuwa hawajui kuogelea waliogopa kujitosa majini, ambapo baadaye
kutokana na kukosa msaada wa kuokolewa alizama katika maji na hakuonekana
tena, jambo ambalo liliwawia vigumu kumuokoa.
Diwani wa kata ya Muhuwesi Nurdin Mnolela, amethibitisha
kuwepo kwa tukio hilo na kwamba baada ya taarifa hizo kumfikia yeye kwa kushirikiana
na uongozi wa serikali ya kijiji, waliitisha mkutano wa dhalura na
kukubaliana kuanzisha msako wa kuutafuta mwili wa marehemu huyo.
Mnolela alifafanua kuwa licha ya kazi hiyo kuwa ngumu,
kutokana na wananchi kutokuwa na ujuzi wa kupiga mbizi, zoezi hilo litawachukua
muda mrefu kuupata mwili wa marehemu Ramadhani.
Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Ruvuma, Zuberi Mwombeji amekiri
kutokea kwa tukio hilo na tayari amekwisha tuma kikosi cha vijana kutoka katika
jeshi hilo, ili kwenda kushirikiana na wananchi hao katika kuutafuta mwili huo.
No comments:
Post a Comment