Saturday, February 27, 2016

MKURUGENZI HALMASHAURI YA SONGEA ASIMAMISHWA KAZI KWA UBADHIRIFU



Na Kassian Nyandindi,
Songea.

MKURUGENZI  Mtendaji Halmashauri ya wilaya ya Songea mkoani Ruvuma, Sixbert Valentine Kaijage amesimamishwa kazi, kwa sababu ya kushindwa kusimamia kikamilifu miradi ya maendeleo ya wananchi na kuisababishia serikali hasara kubwa kutokana na miradi husika katika wilaya hiyo, kutokamilika kwa wakati na kujengwa chini ya kiwango.

Benson Mpesaya ambaye ni Mkuu wa wilaya ya Songea, alisema kuwa Mkurugenzi huyo alienda kuaga Ofisini kwake na kusema kuwa amepewa barua kutoka Wizarani, juu ya kusimamishwa kazi ili apishe uchunguzi kuanzia siku ya Jumatano Februari 24 mwaka huu.
Sixbert Valentine Kaijage.

Mpesya alifafanua kuwa kwa mujibu wa sheria ya utumishi wa umma, mtumishi yeyote akibainika kufanya ubadhirifu au kukiuka taratibu za kiutumishi anasimamishwa kazi hadi pale uchunguzi utakapokamilika na endapo akibainika kuwa amehusika katika tuhuma zinazomkabili, huchukuliwa hatua za kisheria kwa mujibu wa kanuni za utumishi wa umma.

Aidha baadhi ya Madiwani ambao waliomba majina yao yasitajwe, walisema katika vikao vya baraza la madiwani katika Halmashauri hiyo walibaini kuwepo kwa ubadhirifu wa fedha katika miradi ya maji, barabara na ujenzi wa majengo.


Walisema kuwa miradi hiyo imejengwa chini ya kiwango, ambapo shilingi milioni 700 zilizotolewa na aliyekuwa Naibu Waziri wa maji wa serikali ya awamu ya nne Amosi Makala, zilikuwa zifanye kazi ya kujenga miradi ya maji katika vijiji vitano zinadaiwa kutafunwa na vigogo wa halmashauri hiyo.

Imeelezwa kuwa kila kijiji walipatiwa shilingi milioni 100 kwa ajili ya kufanya kazi hiyo ambavyo ni Mpitimbi, Magagula, Parangu na Matimila na kwamba katika fedha hizo ilitakiwa pia zitumike kukarabati visima 13 na kuchimba visima 6 vya maji ya mtiririko.

Katika kazi hiyo hakuna mradi uliokamilika hata mmoja kwa zaidi ya miaka mitatu  sasa, ambapo wakandarasi waliojenga miradi hiyo ni wafanyakazi wa halmashauri hiyo ambao wana kampuni za mifukoni, kwa kushirikiana na Ofisi ya maji mkoa huku wakitumia jina la kampuni ya Kipera kinyume cha kanuni na sheria za nchi.

Kutokana na ubadhirifu huo kamati ya maji ya halmashauri hiyo, ilifanya ukaguzi wa miradi yote na kubaini kuwa imejengwa chini ya viwango na vijiji vingine haikujengwa kabisa, ndipo wajumbe wa kamati husika kutoka baraza la madiwani walilazimika kuitisha ripoti ya fedha ambayo ilionekana kuwa fedha zilizotumika ni shilingi milioni 700 na salio lililobaki kwenye akaunti ya maji benki ni shilingi milioni 73 ambazo ni za mradi wa maji taka.

Mbali na miradi hiyo ya maji mnamo mwezi Novemba mwaka jana, halmashauri iliendesha zoezi la mnada wa magari chakavu ambapo watumishi wa halmashauri hiyo akiwemo Mkurugenzi Kaijage, walijipatia magari kwa bei ndogo na kulipa fedha tofauti na ile waliyoshinda katika mnada.

Inadaiwa kuwa Kaijage, anadaiwa kujipatia gari aina ya Toyota Land Cruiser kwa shilingi milioni 1,200,000 ambalo lilitakiwa liwepo kwenye orodha ya magari yanayotakiwa kuingizwa kwenye mnada, ambapo gari hilo halikuingizwa huku Mkaguzi wa ndani aliyefahamika kwa jina la Njegeni naye alinunua gari Mitsubishi Pikapu kwa bei ya mnada aliyoshinda shilingi milioni 7,000,000  na fedha alizolipa ni shilingi milioni 2,000,000 tu kinyume na bei halali aliyopaswa kulipa.

Baraza la Madiwani la awamu iliyopita kabla ya kuvunjwa kwake, walimtaka Mkurugenzi huyo kusitisha zoezi la mnada wa magari ya halmashauri hadi baraza jipya litakapoanza kazi yake, agizo ambalo Mkurugenzi  huyo alilipuuza na kuamua kufanya mnada huo kinyume na matakwa husika huku akijua kwamba baraza likiwa limevunjwa na jumla ya magari saba walijiuzia katika mnada huo.

Hivi karibuni baraza la Madiwani wa halmahauri ya wilaya ya Songea, liliwasimamisha na kuwafukuza kazi Mhandisi wa maji John Undili na mhandisi wa ujenzi Daudi Basilio, ambao wanadaiwa kutumia vibaya madaraka waliyonayo na kumshauri Mkurugenzi Kaijage kuidhinisha malipo hewa kwa kazi zisizofanyika.

No comments: